Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ken Gold FC bado mbili, TMA Stars mwendo wameumaliza

Kengold Pic Ken Gold FC bado mbili, TMA Stars mwendo wameumaliza

Sun, 14 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya TMA Stars inaifanya Ken Gold FC kuhitaji alama mbili pekee katika mechi mbili za Championship zilizosalia ili kupanda daraja moja kwa moja kwenda Ligi Kuu Bara baada ya kudumu katika ligi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini kwa misimu minne.

Timu hiyo imesaliwa na mechi dhidi ya Polisi Tanzania FC na FGA Talents ambazo itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya ambako kama itashinda zote itafikisha alama 70 ambazo haziwezi kufikiwa na Pamba Jiji, Mbeya Kwanza na Biashara United Mara ambazo nazo zinawania kupanda.

Kama itashinda mechi moja kati ya hizo itafikisha alama 67, ambazo zinaweza kufikiwa na Pamba Jiji FC endapo wana TP Lindanda watashinda mechi zao mbili zilizosalia hivyo kutoa nafasi kwa timu hizo mbili kupanda Ligi Kuu Bara moja kwa moja.

Pia Ken Gold ikipata alama mbili kwa maana ya kutoka sare mechi zote itafikisha alama 66 ambazo haziwezi kufikiwa na Biashara United Mara na Mbeya Kwanza.

Pamba Jiji ikishinda mechi zake zilizosalia inafikisha alama 67, Mbeya Kwanza itafikisha 65 na Biashara 65 ambapo kwa sasa kinara ni Ken Gold akiwa na pointi 64, Pamba 61, Biashara United Mara 59, sawa na Mbeya Kwanza baada ya timu zote kucheza mechi 28.

Katika mchezo wa leo dhidi ya TMA Stars ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, bao ambalo lilipeleka furaha kwa Ken Gold na kufuta kabisa matumaini ya Arusha kupata hata nafasi ya kupanda daraja kupitia hatua ya mtoano (play-offs) lilifungwa katika dakika ya 44 na mchezaji William Edger.

TMA Stars imebakiza mechi mbili dhidi ya Pamba Jiji FC na Copco FC ambapo kama itashinda itafikisha alama 60 ambazo ili kupata nafasi ya kucheza play-offs lazima moja kati ya Biashara United au Mbeya Kwanza ipoteze mechi zilizosalia.

Chanzo: Mwanaspoti