Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ken Gold, City shoo shoo

Ken Gold Kileleni Ken Gold, City shoo shoo

Sat, 3 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Timu za Ken Gold na Mbeya City zimeshindwa kutambiana katika mchezo wa Championship baada ya kumaliza dakika 90 kwa sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

City ambao waliingia uwanjani wakikumbuka kipigo cha mabao 2-0 katika mechi ya raundi ya kwanza, walihitaji kulipa kisasi lakini hadi kumalizika kwa mchezo timu hizo zilitoshana nguvu.

Mbeya City ndio walitangulia kupata bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Mohamed Hajji ambaye amefikisha mabao matatu tangu atue kikosini hapo wakati wa dirisha dogo akitokea Mashujaa FC na kudumu hadi mapumziko.

Ken Gold waliamka kipindi cha pili na kushambulia zaidi na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 49 kupitia kwa Emanuel Mpuka.

Dakika ya 56 City ilijikuta pungufu baada ya mchezaji Maulid Shaban kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na mwamuzi Dany Warioba kutoka Mwanza.

Hata hivyo, licha ya kuwa pungufu walipambana kupata bao la pili lililofungwa na Adili Buha katika dakika ya 88, kisha Ken Gold ikasawazisha kupitia kwa Martin Kazila dakika ya 90.

Mchezo huo ulighubikwa na matukio kadhaa, ambapo shabiki wa Mbeya City ambaye hakujulikana jina alivamia uwanjani kutaka kumtembezea kipigo mwamuzi Warioba kwa kile kilichodaiwa kutoridhishwa na uamuzi wake kwa kadi nyekundu aliyompa Shaban.

Baada ya mchezo kumalizika, Polisi walilazimika kuwawekea ulinzi waamuzi kuanzia uwanjani na kusindikiza gari lao kutoka uwanjani kutokana na mashabiki waliokuwa wakizomea wakidai kutoridhishwa na uamuzi wao.

Matokeo hayo yanaifanya Ken Gold kuendelea kubaki kileleni kwa pointi 44 huku Mbeya City ikifikisha alama 35 ikiwa nafasi ya saba baada ya michezo 20.

Chanzo: Mwanaspoti