Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kelvin azidi kung'ara Ulaya

Kelvin Pic Mchezaji wa KRC Genk, Kelvin John

Tue, 9 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiwango cha mshambuliaji kinda wa Kitanzania, Kelvin John kimeendelea kupagawisha huko Ulaya kufuatia kutupia kwake bao moja kwenye mchezo dhidi ya MTK Budapest wa kuwania nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mbingwa Ulaya upande wa vijana wenye umri chini ya 19.

Mara baada ya mchezo huo ambao kikosi cha vijana cha KRC Genk kiliibuka na ushindi wa mabao 2-1 wakiwa ugenini huko Hungary, kocha Hans Somers alionyesha kuvutiwa na kiwango cha timu yake huku akiwataka wachezaji wake kutambua kuwa kazi bado haijamalizika.

“Tunapaswa kuona kuwa kazi imemalizika baada ya kuvuka hii hatua, ni mbaya kuona kazi imemalizika ilhali bado na ndio kwanza tumecheza mchezo mmoja tu. Kupata ushindi ugenini ni jambo zuri ambalo linatufanya kutanguliza mguu mmoja mbele lakini bado.”

Hans aliongea kwa kuwapongeza vijana wake kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wameifanya kwenye mchezo wa kwanza wa raundi ya pili, “Washambuliaji wetu walikuwa makini kwenye kutengeneza na kutumia nafasi, tulikuwa imara pia nyuma lakini kosa moja lilitugharimu na kuruhusu bao.”

Baada ya wiki ya kimataifa kupita, timu ya vijana ya KRC Genk itakuwa nyumbani Ubelgiji kuikaribisha MTK Budapest kwa ajili ya mchezo wa marudiano, Novemba 23.

Kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, timu ya vijana ya Genk ilivuka hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa jumla ya mabao 7-3 dhidi ya 1. FC Koln, ikumbukwe kuwa Kelvin alitupia mabao mawili kwenye mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Ujerumani.

Hans ambaye amekuwa akivutiwa na uchezaji wa Kelvin amekuwa akitoa nafasi kwa mshambuliaji huyo wa Kitanzania kucheza kwenye kikosi cha vijana wa umri wa juu zaidi miaka 21 ikiwa ni hatua ya kuendelea kumjenga kabla ya kuanza kutumika kwenye kikosi cha wakubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live