Wakati wake unakuja ndicho alichosema nyota wa KRC Genk, Joseph Paintsil kuhusu mshambuliaji kinda wa Kitanzania, Kelvin John ambaye bado hajaanza kupata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Tangu apandishwe kikosi cha kwanza cha KRC Genk, Kelvin mwenye miaka 20 amepata nafasi ya kucheza mara moja tu na ilikuwa kwa dakika tisa, Machi 4,2022 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Ubelgiji 'Jupiler Pro' dhidi ya KAS Eupen.
Muda mwingi anautumia kwenye kikosi cha wachezaji wa akiba ambao nao kwa Ubelgiji wamekuwa wakicheza ligi yao ili kunoa makali yao.
"Hata mimi nilianza taratibu hadi sasa kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza kwenye kujitafuta ilibidi nitoke hadi kwa mkopo, nakumbuka namna ambavyo Samatta alikuwa akinijenga, alikuwa ndiye mfalme hapa, miaka imesogea na kile alichokisema kimetokea," alisema na kuongeza;
"Najua kuwa ni mchezaji mwenye kipaji kikibwa na wakati wake unakuja, naamini anaweza kufanya makubwa na hapa ni sehemu sahihi wake, wamepita wachezaji wengi wakubwa ambao wanafanya vizuri Ulaya."
Msimu uliopita ambao KRC Genk iliukosa ubingwa na kumaliza msimu wakiwa nafasi ya pili, Paintsil alicheza michezo 30 na kupachika mabao 14 na asisti 14 kwenye Jupiler Pro, hicho ni kiwango bora zaidi kwake.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ghana na Kelvin kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya msimu ujao wa 2023/24 ambapo watashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya huku Mbwana Samatta akirejea Fenerbehce baada ya mkataba wake wa mkopo kwenye klabu hiyo kumalizika.