Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Keane: Ferguson aliniita akiwa na barua ya kunifukuza Man U

Skysports Roy Keane Sir Alex Ferguson 4765796 Roy Keane na Sir Alex Ferguson

Thu, 11 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Nahodha wa zamani wa Manchester United aliyekuwa kiungo mtata kabisa katika soka la England, Roy Keane amezungumzia alivyotimuliwa na kutupiwa virago Old Trafford baada ya kutibuana na kocha Sir Alex Ferguson.

Akizungumza na redio ya mtandaoni ya kituo Sky Bet, Keane amesema Fergie pamoja na mtendaji mkuu wa klabu wakati huo, David Gill walikutana naye Novemba 2005 na kuzungumza mambo ya kawaida, lakini mwisho wa siku walikuwa na barua ya kumtimua kikosini.

Nyota huyo aliyejipatia umaarufu enzi hizo kutokana na uchezaji wake wa nguvu, rafu na wakati mwingine ngumi mkononi, anasema anaamini kocha huyo alimuondoa kikosini bila kumtendea haki na mpaka leo hajui kosa alilomtendea ilhali alikuwa mwaminifu aliyeshirikiana na wachezaji wenzake.

Kwani ilikuwaje? Akizungumzia dakika za mwisho, Keane anahisi alichofanya na kufikia kuwakera mabosi - Feguson na Gill ni kitendo cha kwenda katika runinga ya klabu (MUTV), ambapo aliwashambulia wachezaji wenzake kutokana na mchezo uliopita.

Katika mchezo huo, Manchester United ilipokea kichapo cha mabao 4-1 kutoka kwa Middlesbrough - mchezo ambao nahodha huyo hakucheza.

Anasema huenda uamuzi wa kubwatukia mastaa wenzake kupitia runinga ya klabu uliwaudhi mabosi, ambapo Ferguson alianza kwa kumtoza faini ya Pauni 5,000 kabla ya kumuitishia kikaoni akiwa na Gill na kuvunja mkataba wake.

Keane anasema hana tatizo na klabu kumvunjia mkataba, lakini shida aliyoiona ni namna ilivyomuandalia mazingira ya kuondoka klabuni wakati akiwa amekitumikia kikosi hicho kwa muda mrefu (miaka 12) na kukiletea mafanikio makubwa England na Ulaya.

"Siku zote sina shida wakati klabu inapomwambia mchezaji (aondoke klabuni) - soka ni mchezo tunaocheza," anasema. "Kama wewe mtangazaji (Ian Wright - nyota wa zamani wa soka) mabosi wako hawakukuketisha chini na kufanya mazungumzo (ni bahati mbaya), lakini mimi angalau (walifanya). Hiyo ni heshima (walinifanyia).

"(Lakini) nilipoitwa kwenye kikao na Sir Alex Ferguson na David Gill kabla sijaketi walikuwa tayari wameandaa taarifa. Hii ndiyo shida yangu. Tayari walikuwa wameandaa taarifa, na walikuwa nayo muda mrefu."

Baada ya kuondoka Man United, Keane alicheza Celtic kwa nusu msimu 2006, lakini awali alifanya mazungumzo na Everton, Bolton pamoja timu zingine juu ya uwezekano wa kuhamia.

Anasema: "Everton ingekuwa chaguo zuri wakati huo na nilikuwa namheshimu sana (kocha) David Moyes, lakini nilihisi nisingeweza kujiunga na timu nyingine ya England."

Nyota huyo aaliifungia Man United mabao 51 na kutoa asisti 478 katika michezo ya mashindano kati ya 1993 na 2006, huku akishinda makombe saba ya Ligi Kuu England, manne FA na moja Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku akichangia vyema historia ya klabu 1999 iliposhinda mataji matatu kwa mpigo.

Nini kilifanya astaafu ghafla? Ingawa inaelezwa nyota huyo alikumbwa na mshtuko pamoja na msongo wa mawazo baada ya kuondoka Man United kiasi cha kutocheza vizuri alikokwenda, lakini jeraha alilolipata akiwa Celtic ndilo lilikatisha ndoto zake.

Keane anadai aliumia ligameti na madakrati walimshauri ni vyema akastaafu soka na kujikita katika mambo mengine nje na uchezaji.

Chanzo: Mwanaspoti