Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kealey:Mbongo anayeubonda kama Alves Australia

Alavesssssss Kealey:Mbongo anayeubonda kama Alves Australia

Mon, 27 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Inawezekana hii ikawa ni mara yako ya kwanza kumsikia beki wa kulia wa Macarthur FC, Kealey Adamson anayecheza soka la kulipwa Australia.

Kama ni hivyo basi huyu naye ni Mtanzania anacheza timu hiyo na Charles M’Mombwa ambaye amekuwa akiitwa mara kwa mara kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Wawili hao ni marafiki na huenda mbeleni wakawa wanapanda ndege pamoja kwa safari za kuja Tanzania kwa ajili ya kuitumikia Stars.

Kwa nini? Kealey licha ya kuzaliwa na kukulia Australia anatambua asili yake ni Tanzania (mzazi wake mmoja) na yupo tayari kupokea wito wa kuichezea Stars.

Kealey mwenye miaka 21 ni kati ya wachezaji vijana ambao wanaonekana kuwa na vipaji vikubwa na ndiyo maana Macarthur FC iliamua kumsajili na kumpa nafasi kiasi cha kumtazama kama Dani Alves wao kutokana na uwezo wake wa kupandisha mashambulizi na kuzuia, anaweza kucheza beki zote, kulia na kushoto.

Msimu huu, Kealey katika A-League licha ya ugeni wake kwenye kikosi hicho, alipata nafasi ya kucheza michezo 12, ametoa asisti moja huku akionyeshwa kadi tatu za njano, alimelisaidia chama lake kufika katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa ligi hiyo kutokana na mfumo wao ulivyo.

Mfumo wa Ligi ya Australia ni tofauti na Tanzania, wenyewe wanacheza kawaida kisha wale wababe waliomaliza msimu katika zile nafasi za juu, wanacheza mchujo wa kuniwa ubingwa huo, sasa chama la Kealey na M’Mombwa lilishia nusu fainali walitandikwa mabao 4-0 dhidi ya Sydney hata hivyo nao walipoteza katika fainali mbele ya Central Coast Mariners.

Kuhusu utayari wake wa kuichezea Taifa Stars na msimu ulivyokuwa huyu hapa Kealey anafunguka; “Ni suala la kusubiri kwanza na kuona nini kitatokea mbeleni lakini kwangu sioni tatizo kwa sababu najua Tanzania ni nchi nzuri na watu wake wamekuwa na upendo siku zote na hilo nimekuwa nikiliona pale na huwa naenda kwa ajili ya mapumziko,”

Kinda huyo anasema msimu huu ilikuwa ni fursa nyingine kwake akiwa na Macarthur FC moja ya klabu kubwa nchini humo.

“Tulipambana kwa namna ambavyo iliwezekana lakini haikuwa bahati yetu kuchukua ubingwa, msimu ujao itakuwa nafasi nyingine, hivyo tunatakiwa kusahau kilichopita na nguvu na mawazo yetu kuelekeza mbele,” anasema na kuongeza;

“Binafsi nashukuru kwa benchi la ufundi kwa nafasi ambayo nimepata kwa sababu ni kitu ambacho kila mchezaji amekuwa akihitaji, mpango wangu ni kuendelea kujitoa na kujituma kwa ajili ya timu, pia nashukuru na mashabiki kwa kuniunga mkono, amekuwa nyuma yangu na kwa timu kwa jumla.”

Kwa upande wake, M’Mombwa amemwagia sifa kinda huyo kwa kusema anatakiwa kuendelea kupambana huku akiamini kuwa kila kitu kinawezekana.

“Ni mchezaji mwenye kipaji, nakubali uwezo wake, anatakiwa kuendelea kupambana kwa sababu kwanza bado ni mdogo, ananafasi ya kuonyesha zaidi.”

Kealey ambaye anavalia jezi namba 20, alianza maisha yake ya soka katika timu ya vijana ya Sydney baada ya kukomaa alipandishwa kikosi cha kwanza lakini kwa bahati mbaya hakuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Ndipo alipofanya maamuzi magumu ya kujiunga na Macarthur FC.

Huyu ni Mtanzania wa tatu kucheza ligi kuu nchini humo kwa msimu ulimalizika siku chache zilizopita, ukiachana na M’Mombwa ni Nestory Irankunda ambaye msimu ujao atashuhudiwa akiichezea Bayern Munich ya Ujerumani.

KOCHA AFUNGUKA

Kocha wa Kitanzania, Emanuel Saakai ambaye anaishi na kufanya kazi nchini humo, amemuongelea Kealey kwa kumfananisha na beki wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa la Brazil, Dan Alves kwa kusema anamwona mbali miaka michache ijayo.

Saakai anaamini Kealey ni kijana mwenye kipaji kikubwa na aliliona hilo tangu akiwa na timu ya vijana ya Sydney.

“Kiukweli ni mchezaji mzuri ambaye anaweza kufiti katika soka la kisasa ambalo linawataka mabeki wa pembeni kuwa na uwezo wa kushambulia katika maeneo ya pembeni hata kuchezesha timu ikihitaji eneo la kiungo,” anasema na kufafanua;

“Nimeona siku hizi wapo mabeki wa pembeni ambao hutumika katika maeneo ya kiungo wakati timu ikiwa inajenga mashambulizi yake.”

Licha ya kutopata nafasi wakati akiwa na Sydney, Kealey alitwaa ubingwa wa Australia Cup akiwa na timu hiyo, 2023.

Chanzo: Mwanaspoti