Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kazi ya Moloko ilikuwa moja tu!

Jesus Moloko 1 Year Jesus Ducapel Moloko

Tue, 16 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mpira umebadilika kwa kasi katika miaka ya karibuni. Kuna wajanja wamekuja wameubadili mpira. Majuzi nilimuona kijana mpya wa Simba, Saleh Karabaka akijaribu kutokea upande wa kulia ingawa anatumia mguu wa kushoto. Alinifurahisha.

Kwa sasa tumefika huko. Tukiachana na habari ya kwamba kipa lazima aweze kutumia miguu yake vyema pengine kuliko mikono. Tukiachana na habari ya kwamba mabeki wa kati wanaweza kucheza watatu. Tukiachana na habari kwamba mabeki wa kati lazima wajue kupiga pasi kutokea nyuma na sio kubutua.

Sasa hivi pia tuna habari ya mawinga kubadilisha matumizi ya nafasi zao kutegemea na miguu yao. Wale wanaotumia miguu ya kushoto wanakwenda upande wa kulia. Wale wanaotumia miguu ya kulia wanakwenda upande wa kushoto.

Mpaka sasa tuna mawinga wengi ambao wameshindwa kuifanya kazi hii kwa ufasaha. Wengi zaidi tunao Tanzania, lakini wapo wageni ambao wameshindwa pia kuifanya kazi hii kwa ufasaha licha ya kulipwa pesa nyingi.

Lengo kubwa la anayecheza upande wa kulia kutumia mguu wa kushoto ni kupunguza krosi na kumtaka aingie ndani na mpira. Anapoingia ndani na mpira anajikuta katika wakati mzuri kwa sababu mpira unakuwa katika upande wa kushoto na lango linakuwa kulia kwake.

Hii inamfanya aweze kupiga krosi nzuri lakini pia inamfanya aweze kufunga mwenyewe au kupiga pasi ya mwisho ufasaha zaidi huku akitumia nguvu zake zilezile za mguu wa kushoto. Upande wa pili unapaswa kuwa na ufasaha huohuo.

Hata hivyo, mpaka leo mawinga wetu wameshindwa kubadilika. Kuanzia wale wanaocheza timu kubwa hadi wale waliopo mtaani. Wanaocheza kulia ni walewale wanaotumia mguu wa kulia na wanaocheza kushoto ni walewale wanaotumia mguu wa kushoto.

Unajua kwanini? Wengi wao hawajiamini kwenda pembeni na kisha kuingia katikati. Wanaamini katika kwenda katika kibendera na kupiga krosi, basi. Hawa ndio mawinga wa kizamani ambao wameshindwa kubadilika kutokana na mabadiliko ya mchezo wenyewe.

Rafiki yangu Jesus Moloko anatumia mguu wa kulia na anakwenda upande wa kulia. Anachoangalia ni kupiga krosi tu, basi. Mambo mengine yanampa shida. Rafiki yake Tuisila Kisinda naye ni hivihivi tu. Anakwenda kulia kujaribu kupiga krosi.

Jose Luis Miquissone huwa anajitahidi kutokea kulia, lakini mchunguze rafiki yangu mwingine, Farid Mussa. Farid hana raha akicheza upande wa kulia, lakini huo ndio ulipaswa kuwa upande ambao angesumbua watu kwa kiasi kikubwa.

Anajisikia raha zaidi akicheza kushoto kwa sababu lengo lake kuu ni krosi. Wagunduzi wa staili hii kina Lionel Messi waliileta kwa lengo la kumfanya winga afunge zaidi na sio kuwa mpiga krosi tu. Winga wa kulia anayetumia mguu wa kushoto pindi akikatiza katikati anakuwa katika nafasi nzuri ya kupiga shuti linalozunguka (curving) na kufunga.

Huo upande kina Bukayo Saka, Riyad Mahrez, Mohamed Salah wameutendea haki kwa kiwango cha juu. Na hata sasa Mohamed Kudus wa West Ham United na timu ya taifa ya Ghana ameutendea haki vya kutosha. Kazi imebaki kwa wachezaji wetu. Ni mawinga wanaoutumia mguu wa kulia na wanacheza upande wa kulia.

Huku kushoto ungeweza kuchukua mifano ya wengi lakini tunawaona kina Gabriel Martinelli na Marcus Rashford ambaye wakati mwingine anacheza upande huo. Sadio Mane akiwa na Liverpool alikuwa anacheza upande huo. Thierry Henry alikuwa akitamba kwa upande huo.

Ukigeuka unapata faida kubwa ya kuendelea kutumia mguu wa kulia kuliko kwenda katika kibendera na kupiga krosi kwa kutumia mguu dhaifu wa kushoto. Hapa nchini mtu ambaye alituonyesha matumizi sahihi ya kuicheza nafasi hiyo akitumia mguu mwingine ni Emmanuel Okwi.

Sawa, alikuwa mzuri akitokea kulia lakini alikuwa mzuri zaidi akicheza kisasa na kutokea kushoto. Mabeki wa kulia walikuwa wanapata wakati mgumu kumkaba kwa sababu wakati anakokota walikuwa hawajui anatokea upande gani, lakini pindi ambapo angepata nafasi ya kugeuka alikuwa anajua nini cha kufanya. Angeweza kufunga kwa urahisi au kupasia kwa urahisi.

Kuanzia huku chini tuwafundishe vijana mabadiliko ya mpira wa kisasa. Ukienda kutazama mechi za vijana unakuta maisha ni yaleyale ya kizamani. Makocha bado wanafundisha mawinga kupiga krosi na sio kufunga. Mpira umebadilika.

Wachezaji wa mwisho mwisho kucheza nafasi hizo kwa ufasaha walipaswa kuwa kina Mrisho Ngassa au Saimon Msuva. Zamani hawa jamaa walikuwa wanatumia miguu ya kulia na walikuwa wanacheza upande wa kulia. Walifanya vyema, lakini katika dunia ya kisasa walipaswa wachezaji wa kutokea kushoto.

Winga pekee ambaye nadhani alikuwa mbele ya muda ni Edibily Lunyamila. Ameacha mpira zamani lakini alikuwa mbele ya muda kwa sababu alikuwa winga anayeingia ndani akitokea katika pande zote ambazo angejipanga mwenyewe.

Angeweza kutokea kulia akapiga chenga na kuingia ndani kufunga au kupiga pasi ya mwisho kwa mtu mwingine. Angeweza pia kutokea kushoto na akalifanya jambo hilo kwa ufasaha. Nadhani Edibily alikuwa mbele ya muda. Amefanya mambo ambayo hata mawinga wa sasa wanashindwa kufanya.

Tuwafundishe vijana wetu mabadiliko ya soka kama tunataka kuwatafutia soko la kisasa nje ya nchi. Mchezo wenyewe umebadilika kwa kasi, lakini sisi inaonekana tunayapokea mabadiliko kwa taratibu. Haipaswi kuwa hivi.

Ianzie kuwafundisha katika kujiamini katika kukaa na mpira na kupunguza watu. Kila kitu kitawezekana. Kuwahi kupiga krosi ni uoga tu wa maisha ambao kina Saka hawana. Mawinga siku hizi ni wafungaji wazuri kuliko kuwa wapiga krosi wazuri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live