Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kazi ipo, Mrithi wa Lomalisa na upepo wa Wakongomani

Boka Chadrack Boka

Tue, 21 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Yanga kwa sasa wana raha mara mbilimbili, mojawapo ikiwa ni kutokana na kufanya vizuri kwa timu yao na pili mchakato wa kuboresha kikosi chao umeanza kwa ajili ya msimu ujao.

Rais wa Yanga, Hersi Said ameonakana DR Congo kwa ajili ya kumalizana na baadhi ya wachezaji ambao kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amewapendekeza katika ripoti yake ikiwemo beki wa kushoto ili kuongeza ufanisi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ni kwamba, miongoni mwa wachezaji ambao wamemfanya Hersi kwenda DR Congo ni pamoja na Chadrack Boka anayetajwa kuwa miongoni mwa mabeki wa maana wa kushoto nchini humo, na amekuwa akifanya vizuri akiwa na FC Saint Eloi.

Kama vigogo wa Yanga watamalizana na Mkongomani huyo huenda msimu ujao akarithi mikoba ya Joyce Lomalisa ambaye anaweza kuondoka Jangwani ili kumpisha beki huyo anayeonakana kuwa na vigezo ambavyo Gamondi anavihitaji kulingana na ripoti yake.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Jangwani imeonekana kuwa ni nyumbani kwa wachezaji Wakongomani na wamekuwa sehemu muhimu katika ujenzi wa kikosi hicho ambacho kwa sasa ni tishio sio tu Afrika Mashariki, bali Afrika katika mashindano mbalimbali.

Msimu uliopita Yanga ilicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na Wakongomani watano akiwemo Fiston Mayele ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo kutokana na namna alivyomudu kutupia mabao katika mechi za mashindano.

Kuonyesha kuwa Jangwani ni nyumbani kwa wachezaji wa Kikongomani hawa hapa baadhi yao ambao walifanya vizuri kwa nyakati tofauti wakiwa na timu hiyo miaka ya karibuni.

HERITIER MAKAMBO

Julai mosi, 2018 mshambuliaji huyo alijiunga na Yanga akitokea FC Saint Eloi wakati huo, timu hiyo ilikuwa ikipitia kipindi kigumu kiuchumi, lakini nyota huyo alionyesha thamani yake uwanjani.

Makambo ambaye alikuwa maarufu kwa staili yake ya ushangiliaji kwa kubana mikono ‘kuwajaza’ katika msimu wa kwanza Jangwani (2018/2019) alimaliza ligi akiwa kinara wa mabao kwa timu hiyo akitupia kambani mara 19, akizidiwa kete na Meddie Kagere (Simba) aliyefunga 23 katika vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Kutokana na hali ngumu ambayo Yanga ilikuwa ikipitia mshambuliaji huyo alisajiliwa na Horoya ya Guinea kwa dau la Dola 100,000 akitokea Yanga na akiwa huko mambo yalimwendea kombo na kurejea Jangwani, Agosti 2021, lakini hata hivyo hakufanya vizuri. Kwa sasa yupo Libya anacheza soka la kulipwa akiwa na Al Murooj.

FISTON MAYELE

Anatajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji bora zaidi wa Kikongomani kuwahi kucheza soka la kulipwa Tanzania katika miaka ya karibuni. Mayele alicheza kwa mafanikio Yanga misimu miwili (2021/22 na 2022/23) na mbali ya kutwaa mataji kama vile Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), alikuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na staili yake ya ushangiliaji ya kutetema iliyoteka na kuanza kutumika katika sehemu mbalimbali kwenye matukio ya burudani ikiwamo shuleni, kanisani na hata bungeni. Hakika alipendwa.

Miongoni mwa mabao yake yanayokumbukwa wakati akicheza soka la kulipwa nchini ni pamoja na lile la mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani zao, Simba SC, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa wakati huo alikuwa akijipambanua kabla ya kujichotea umaarufu baadaye. Katika mechi 54 Mayele akiwa na jezi ya Yanga aliifungia mabao 50.

TUISILA KISINDA

Huyu ni Mkongomani mwenye bahati zaidi ya kucheza fainali ya michuano ya kimataifa kuliko yeyote aliyepita Yanga.

Japokuwa ilikuwa katika awamu yake ya pili kucheza Yanga, msimu uliopita Kisinda alicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilipoteza kwa kanuni dhidi ya USM Alger iliyokuwa ikinolewa na aliyekuwa kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha. Msimu huu Tuisila amecheza fainali hiyo akiwa na RS Berkane ya Morocco ambayo itacheza dhidi ya Zamalek. Nyota huyo ambaye anasifika kwa kasi, alifanya vizuri Yanga katika awamu yake ya kwanza msimu wa 2020/21 akitokea AS Vita ya DR Congo.

MUKOKO TONOMBE

Tonombe ambaye alijiunga na Yanga 2020 na kuichezea kwa miaka miwili hadi 2022, alikuwa miongoni mwa viungo wa nguvu. Jamaa alijua kukata umeme kwelikweli, lakini siku zote Waswahili husema “muda ni ukuta ukishindana nao, utaumia.” Wakati wake ulipofika aliondoka kama ilivyokuwa wachezaji wengine.

Pamoja na kufanya kwake mazuri akiwa na Yanga, Mukoko alikuwa katika wakati mgumu na hilo ni miongoni mwa matukio ambayo bado yapo kichwani mwake kwani ilikuwa Julai 2021 ambapo aliigharimu timu na kupoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba. Kiungo huyo alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya nahodha wa Simba, John Bocco. Wapo ambao waliamini kwamba lilikuwa ni tukio la kawaida la kimpira, lakini wengine walimshutumu kwa dhana tofauti.

SHAABAN DJUMA

Akiwa katika ubora wake hakuna ambaye hakuwa akimuongelea beki huyo wa kulia mwenye uwezo mkubwa wa kupandisha mshambulizi. Changamoto aliyokuwa nayo ilikuwa ni katika kuzuia. Mchezaji huyo alitua Jangwani 2021 na kuondoka 2022.

Kuna kipindi alikuwa akidaiwa kuongezeka uzito, jambo ambalo lilikuwa likiathiri kiwango chake kiasi cha mabosi wa timu hiyo kufikiria mpango mbadala ili kuboresha eneo hilo. Ni kati ya wachezaji wazuri wa Kikongomani ambao wamepita Yanga.

YANNICK BANGALA

Julai 2022, Yanick Bangala alitangazwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/2022. Mkongomani huyo alikuwa katika kilele cha ubora wake na alitoa zaidi ya asilimia 80 ya ubora wake katika kikosi cha kocha Nasreddine Nabi na kutwaa ubingwa wa ligi.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Bangala aliwashinda Wakongomani wenzake Fiston Mayele ambaye alikuwa akicheza naye katika kikosi cha Yanga na beki wa Simba, Henock Inonga, waliokuwa pia wanagombea tuzo hiyo. Ndani ya msimu huo, Bangala pia alikomba tuzo ya kiungo bora wa ligi. Kwa sasa anaendelea kutesa akiwa na Azam FC huku akitumika zaidi katika nafasi ya beki wa kati ambayo pia anaimudu.

JESUS MOLOKO

Ndiye Winga ambaye alikuwa na makali zaidi katika kikosi cha Yanga kabla ya kutua kwa Pacome Zouzoua (Muivory Coast) na Maxi Nzengeli (Mkongomani) ambao walihatarisha nafasi yake hadi kuonyeshewa mlango wa kutokea kutokana na kutokuwa na nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza. Moloko ambaye aliichezea Yanga kwa miaka mitatu kwa sasa ni mchezaji wa Al-Sadaqa ya Libya.

PAPY TSHISHIMBI

Kiungo huyo alijiunga na Yanga Juni 2018 akitokea Mbabane Swallow, ni miongoni mwa viungo waliotikisa Ligi Kuu Bara, lakini majeraha ndio yaliyokuwa yakimtibulia kuna kipindi alikuwa akivaa kitambaa cha unahodha kwenye kikosi. Tshishimbi aliondoka Yanga 2020 na kurejea zake nyumbani, DR Congo akajiunga na AS Vita Club kabla ya kurejea tena nchini, lakini safari hii akatua zake Ihefu na sasa yupo Tabora Utd.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: