Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaze hajutii kutemwa Yanga

B545da4432051d7e65184dc8854e7f97.jpeg Kaze hajutii kutemwa Yanga

Wed, 10 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Yanga aliyetimuliwa, Cedrick Kaze amesema hajutii kitendo hicho kwani ni kitu cha kawaida kwa makocha duniani kote.

Kaze alisema hayo jana baada ya uongozi wa klabu hiyo kutangaza kumtupia virago yeye pamoja na benchi lote la ufundi kufuatia matokeo mabaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Timu hiyo katika mechi sita ilizocheza tangu kuanza kwa mzunguko wa pili, imeshinda moja tu na kutoka sare nne na kufungwa moja. Kaze alipozungumza na gazeti hili jana, aliushukuru uongozi wa klabu hiyo kwa kumpa nafasi ya kufundisha timu hiyo na kushauri kocha ajaye apewe muda zaidi.

Kaze alisema kilichotokea ni jambo la kawaida kwenye mchezo wa soka ingawa uongozi umeshindwa kuvumilia upepo mbaya ambao unapita ndani ya klabu hiyo.

“Sina wakumlaumu katika hili sababu kufukuzwa kwa makocha ni jambo la kawaida duniani kote, isipokuwa najivunia mafanikio niliyopata katika siku 142 ambazo nimekaa Yanga.”

“Nimefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi na kuiacha Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, haya kwangu ni mefanikio makubwa sana,” alisema Kaze.

Kocha huyo raia wa Burundi alisema katika miezi mitano aliyohudumu Yanga, amejifunza mambo mengi na kuujua ukubwa wa timu aliyokuwa akiifundisha pamoja na kiu ya mashabiki na wanachama wake.

Alisema pamoja na changamoto nyingi alizokutana nazo wakati timu inapitia kwenye kipindi kigumu, anajivunia kuwapa furaha mashabiki na wanachama wao, kwani alijitahidi kurudisha furaha iliyokuwa imepotea kwa misimu mitatu nyuma.

Kaze alisema hawezi kusema kinachoisumbua Yanga, isipokuwa anaushauri uongozi kumpa muda kocha atakayekuja kuchukua nafasi yake sababu ana amini kosa lililomuondoa hapo ni kukosa muda wa kuijenga timu.

Alisema wakati anajiunga na Yanga aliikuta timu ipo kwenye ligi hivyo isingekuwa rahisi kurekebisha kila kitu wakati ligi ikiendelea ingawa kwa kiasi fulani alijitahidi kuweka sawa baadhi ya mambo kitu kilichochangia kupata matokeo hayo waliyoyapata.

“Naondoka nikiwa sijutii maamuzi yangu ya kuja kuifundisha Yanga na zaidi natembea kifua mbele sababu rekodi yangu ni nzuri niliyoiacha hapa katika hiyo miezi mitano niliyohudumu hapa Yanga,” alisema.

Rekodi za Kaze tangu alipojiunga na Yanga, ameiongoza timu hiyo kwenye michezo 18 katika ligi, ameshinda michezo 10, ametoka sare michezo saba na kufungwa mchezo mmoja.

Pia aliiongoza mechi nne visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na Yanga kufanikiwa kuibuka mabingwa. Inaelezwa kwamba kuna uwezekano uongozi wa Yanga ukamtangaza Mecky Maxime au kumrudisha Juma Mwambusi katika nafasi ya kocha msaidizi wakati huu ukipambana kumsaka mrithi wa Kaze

Chanzo: www.habarileo.co.tz