Ligi Kuu inatarajiwa kurudi Ijumaa, lakini katika mechi za awali za raundi tano, Yanga imekuwa gumzo kwa soka lake la pasi nyingi na umiliki wa mipira, lakini hakuna aliyekuwa anaijua siri ya utamu huyo wa Vijana wa Jangwani.
Unabisha nini? Katika mechi mbili za mwisho dhidi ya Azam na Ruvu Shooting, Yanga ilifunga mabao yake mawili kwa kila timu ikipiga pasi zaidi ya 20 kabla ya kuzamishwa nyavuni na kuwadatisha mashabiki wao, huku sifa kubwa zikienda kwa viungo Yannick Bangala na Khalid Aucho.
Maelewano ya viungo hao wawili waliosajiliwa msimu huu sambamba na jeshi zima la Yanga limekuwa likileta burudani kwa mashabiki wa klabu hiyo na wapenzi wengine wa soka wanaopenda pira sambusa linalochanganywa na udambwidambwi wa kampa...kampa tena...!
Hata hivyo, Mwanaspoti katika fukuafukua yake, imebaini mipasi yote ile huwa inasukwa kutoka wapi na benchi la ufundi la klabu hiyo.
Ukweli ni kuwa ushirikiano nzuri wa benchi hilo chini ya Kocha Nasreddine Nabi na Msaidizi wake, Cedrick Kaze ndio kinachoifanya Yanga icheze soka tamu na la kuvutia msimu huu, ikizifunika timu nyingi, huku maujuzi ya Pep Guardiola, Jurgen Klopp wanaokimbiza pale England na klabu zao za Manchester City na Liverpool yakitajwa.
Ipo hivi. Tangu Kaze atue Yanga yeye na Nabi walikubaliana kutafuta mbinu mbalimbali kutoka kwa makocha na timu kubwa duniani kisha kuzichakata na kuzifundisha kwa mastaa wao mazoezini kabla ya kuzionyesha hadharani katika mechi.
Mbinu za Man City chini ya Pep na zile za Mjerumani, Klopp anayeinoa Liverpool ni kati ya vitu wanavyovitumia Yanga kuwamaliza wapinzani wao kwa kucheza soka la kuvutia.
Kaze ndiye amekuwa kinara wa kuwasoma makocha hao wakubwa duniani, kisha kuziwasilisha kwa Nabi na kujipanga namna ya kuzishusha kwa mastaa wao wanaowatesa vilivyo wapinzani wao. uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaze alikiri yeye na Nabi hujifungia ndani na kusoma mbinu za makocha tofauti waliofanikiwa ulimwenguni akiwemo Klopp na Pep, kisha kuzitambulisha kwa wachezaji.
“Tunataka timu icheze vizuri na kisasa zaidi, hivyo lazima tuumize vichwa kusoma na kuwaangalia makocha bora waliofanikiwa ulimwenguni wanafanyaje,” alisema Kaze na kuongeza;
“Mfano Guadiola na Klopp, tunaangalia mbinu zao na kuangalia zitatusaidiaje kutokana na mahitaji ya mechi zetu na kuongeza ubora wa wachezaji wetu kila siku.”
Kaze aliongeza;“Sio kama tunakopi, hapana ila sisi tunazitambulisha mbinu zile na kuzifanya ziendane na mazingira na uwezo wa wachezaji wetu. Kazi kubwa tunaifanya kwenye mazoezi na kuwapa maelekezo jinsi tunataka kucheza kisha kusimamia kuhakikisha wanafanya hivyo.”
“Tunaanzia kwa kipa, mabeki, viungo hadi washambuliaji, kila eneo tunahakikisha linakuwa imara na kucheza mpira tunaoutaka. Kuna kipindi tunacheza uwanja mdogo, muda mwingine mkubwa, pia hufanya mazoezi katika viwanja vyote, kapeti na kawaida.” alifunguka zaidi kocha huyo wa zamani wa akademi ya Barcelona..
“Hata mazoezi ya misuli na mengine yote tunafanya kwa namna tutakavyoenda kucheza kwenye mechi inayofuata ambapo mifumo na mbinu zote tunazifundisha mazoezini hivyo tukienda kwenye mechi tunakuwa tumemaliza kila kitu na hiyo ndio siri ya ushindi,” alisema.
Aidha Kaze alizungumzia maandalizi ya mechi zao mbili zinazofuata dhidi ya Namungo Jumamosi hii na ule wa Mbeya Kwanza wa Novemba 30.
“Tunaenda kucheza mechi mbili mfululizo ugenini, tunaendelea kujiandaa kwa michezo hiyo kutokana na namna ya wachezaji wa timu hizo na viwanja tunavyoenda kuchezea,” alisema Kaze akisistiza wamejiandaa vyema.