Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaze awashukia wachambuzi wa soka

Ba0dbda0379bc477e937013a1586eb79 Kaze awashukia wachambuzi wa soka

Mon, 22 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Yanga, Cedric Kaze amewashukia wachambuzi wa mpira wanaobeza mbinu anazowapa wachezaji wake baada ya kutoka sare michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga kabla ya kupata ushindi kwenye mchezo uliopita wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi, ilipitia kwenye kipindi kigumu baada ya kupoteza pointi sita kwa kutoka sare dhidi ya Tanzania Prisons, Mbeya City na Kagera Sugar.

Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, Kaze alisema alikuwa hafahamu utamaduni wa mpira wa Tanzania lakini wiki iliyopita alijifunza mambo mengi.

“Ndani ya hiyo wiki moja nimejifunza mengi kuliko miezi mingi niliyomaliza hapa Tanzania, wakati timu yangu inapitia kipindi kigumu kama mtu anayeumwa anashindwa kupumua watu wanafurahia na wanataka waende wakamshambulie.”

“Watu wanajiita wachambuzi wa mpira wanaongea maneno ya kubeza mbinu zangu, ukinibeza mimi hamna shida, lakini nataka kuwaambia kwamba nimejifunza kwenye hii wiki na sikufika hapa kubadilisha utamaduni wangu au mtazamo wa watu,” alisema Kaze.

Kocha huyo alisema mchezo uliopita wa Yanga na Mtibwa Sugar ulikuwa na ushindani mkubwa na umeongeza morali na wachezaji wake ambao watakuwa na utulivu kwakuwa wametoka kwenye kipindi kigumu.

“Mtibwa ni timu yenye ushindani, kabla ya mchezo tulikuwa tunajua matokeo yatakuja kupatikana kipindi cha pili baada ya wachezaji kuchoka, kikubwa nashukuru wachezaji wangu hizi pointi tatu zitawapa nguvu kujipanga na michezo ijayo,” alisema Kaze.

Katika mchezo huo bao pekee lililowapa ushindi Yanga liliwekwa kimiani na Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Deus Kaseke.

Alipachika bao hilo dakika ya 73 akimalizia pasi iliyopigwa na Tuisila Kisinda, bao lilomfanya kocha Kaze kushangilia.

Kaze pia aliwapongeza wachezaji wake kwa kuendelea kusimama kwenye msingi wa nidhamu ya kujilinda na kutoruhusu mabao mengi kufungwa kwenye michezo yote mitatu waliyoambulia sare.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Hitimana Thiery alikubali matokeo ya mchezo huo na kuelekeza kwamba wachezaji wake walifanya makosa yaliyowafanya wapinzani wao kutengeneza nafasi na kupata bao la ushindi.

“Nakubali matokeo na nawapongeza wapinzani kwakucheza kwa malengo, tulitengeneza nafasi hatukuweza kuzitumia lakini wapinzani wetu walionekana bora kwa kutumia nafasi moja waliyopata,” alisema Thiery

Ushindi huo unawafanya Yanga kufikisha pointi 49 wakiendelea kuongoza ligi, huku Mtibwa Sugar ikibaki nafasi ya 11 na pointi 23 baada ya kucheza mechi 20.

Chanzo: habarileo.co.tz