Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaze atua Yanga na mambo matano

8b5e9373c639897bd281c2a75df9ae8a Kaze atua Yanga na mambo matano

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Yanga, Cedrick Kaze ana kazi ya kufanya na ametaja baadhi ya mambo muhimu katika kuisaidia timu hiyo kufi kia malengo yaliyokusudiwa.

Akiwa safarini kutua Dar es Salaam kujiunga na Yanga kocha huyo aliyetarajiwa kutua jana usiku alizungumzia mipango yake na mambo atakayofanyia kazi mitaa ya Jangwani na Twiga, Kariakoo.

Kitu cha kwanza alisema amedhamiria kuifanya Yanga icheze soka la kuvutia baada ya kushindwa kufanya hivyo karibu misimu miwili mfululizo licha ya kufanya vizuri katika baadhi ya mechi.

“Nitahakikisha mimi na wachezaji tunatoa burudani ya soka la kuvutia na kurejesha heshima kwa mashabiki wetu,” alisema.

Yanga iliyokuwa inacheza soka la kuvutia ilikuwa chini ya Kocha Hans Pluijm na ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu. Jambo la pili alisema atarudisha furaha ili mashabiki wanakwenda uwanjani basi warudi na nyuso za furaha wakicheza na ikiwezekana watoke wakiimba nyimbo za shangwe.

“Nawahakikishia mashabiki wa Yanga watakuja kwenye mechi na kurudi wakiwa wamefurahi huku wakiimba,” alisema Kaze kwenye mahojiano na Wasafi Fm.

Jambo la tatu alisema kuna kitu anakuja kukifanyia kazi baada ya kutazama mechi karibu zote za Ligi Kuu, za kirafiki hadi zile za msimu uliopita za Yanga.

Alisema ana wazo la kufanya kuiwezesha timu hiyo kurudi katika ubora wake na kufanya vizuri katika mechi zake zijazo. Huenda pia katika hili ameona uwezo wa wachezaji wake hivyo, atatumia mbinu zake kuwapandisha wale walionekana kutokuwa na kiwango kuwa bora zaidi.

Jambo la nne ameomba ushirikiano kutoka kwa mashabiki na viongozi wa klabu hiyo kuwa na umoja na mshikamano ili waweze kufanya mambo makubwa yaliyokusudiwa.

Na mwisho alisema hataki kuihakikishia timu hiyo kuwa anakuja kuipa taji kwani yote ni mipango ya Mungu. Kocha huyo anatarajiwa kuchukua mikoba ya Zlatko Krmpotic aliyefungashiwa virago kutokana na uongozi kutoridhishwa na mfumo wake katika timu.

Kibarua cha kwanza cha kocha huyo ni mchezo ujao dhidi ya Polisi Tanzania utakaochezwa Uwanja wa Mkapa Oktoba 22, mwaka huu baadaye kuna Biashara na KMC kabla ya kuja kukutana na watani wa jadi Simba Novemba 7, mwaka huu

Chanzo: habarileo.co.tz