Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaze alaumu washambuliaji

Cd2bc491db8a9377ec362e6813959b80 Kaze alaumu washambuliaji

Fri, 19 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Yanga, Cedric Kaze amewatupia lawama washambuliaji wake kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ulioisha kwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Kagera Sugar uliofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam juzi.

Hiyo ni sare ya tatu mfululizo kwa Yanga baada ya kufanya hivyo dhidi ya Mbeya City kwa bao 1-1 kabla ya kukutana na Tanzania Prisons waliopatga matokeo kama hayo pia.

Kaze alisema kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar wachezaji wake walitengeneza nafasi nyingi ambazo walikosa umakini wa kuzitumia kufunga, pia muda mwingi walikuwa hawashuki kwenda kuwasaidia walinzi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kaze alisema kitendo cha kushindwa kushuka kuwasaidia walinzi kwenye mchezo huo kilisababisha wapinzani wao muda mwingi kucheza kwa uhuru na kulisakama lango lao na kufunga mabao.

“Ulikuwa mchezo mgumu kwetu, muda mwingi tulikuwa tunafanya kazi kubwa ya kutafuta mabao ya kusawazisha na makosa yake walifanya wachezaji wangu wanaocheza sehemu ya ushambuliaji walikuwa hawashuki kuja kutoa usaidizi kwa mabeki.

“Kutokana na changamoto hiyo wapinzani wetu walikuwa wanatushambulia kwakuwa walikuwa wanapita eneo la katikati kwa uhuru kwa sababu muda mwingi tulikuwa na pengo kubwa,” alisema.

Alisema kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi wanaenda kujipanga vyema kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Mtibwa Sugar kesho kuhakikisha wanapata ushindi utakaorejesha morali yakuendelea kupambana na michezo mingine iliyosalia.

Naye kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime aliwapongeza wachezaji wake kwa kucheza soka la kuvutia muda mwingi na kuahidi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo.

“Mchezo ulikuwa mzuri kwangu, wachezaji walicheza kwa kuelewana zaidi na wapinzani wetu muda mwingi walikuwa wanapata shida kupoka mipira, imenifurahisha kikubwa tunaenda kujipanga na mechi ijayo,” alisema Maxime.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kuendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza michezo 20, huku wapinzani wao Kagera Sugar wakisalia nafasi ya 10 wakiwa na pointi 24 walizozikusanya kwenye michezo 20.

Chanzo: habarileo.co.tz