Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaze: Tutahakisha Mayele anatwaa tuzo mfungaji bora

Mayele Caf.jpeg Fiston Mayele

Thu, 8 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla watapambana kumsaidia straika na kinara wa mabao hadi sasa Ligi Kuu, Fiston Mayele kuhakikisha anafikia malengo yake ya kutwaa tuzo ya kiatu cha mfungaji bora.

Kaze amesema hayo leo wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini hapa wakati akielezea maandalizi yao ya mwisho kuelekea mchezo wao wa kufunga msimu huu 2022/23 dhidi ya Tanzania Prisons.

Amesema wanafahamu upinzani ulivyo hadi sasa, hivyo wataangalia kadri ya uwezo wao kumsaidia nyota huyo aliyekosa tuzo hiyo msimu uliopita kutokosa tena heshima hiyo msimu huu.

"Kuanza kwake kesho uwanjani huenda ikawa hivyo na sisi benchi la ufundi na wachezaji tutapambana kumfanikishia lengo hili aweze kufunga mabao na kutwaa tuzo hii" amesema Kaze.

Hata hivyo ameongeza kuwa wamejipanga kupata ushindi kwenye mechi hiyo ili kuendana na tukio lao la kupokea kombe jipya na kwamba wamekuwa na mafanikio mazuri kwa misimu miwili mfululizo wakitwaa ubingwa.

Kuhusu wachezaji watakaokosa mechi hiyo ni Jesus Moloko mwenye kadi nyekundu na Bernard Morison na Khalid Aucho wenye kadi za njano na kwamba wengine wako fiti kwa mapambano.

Mayele hadi sasa ana mabao 16 akimuacha mpinzani wake bao moja, Saido Ntibazonkiza anayecheza Simba na kufanya vita kuwa nzito baina ya wawili hao.

Straika huyo wa DR Congo katika mechi iliyopita dhidi ya Mbeya City waliyotoka sare ya 3-3 hakuwepo na sasa tayari amewasili jijini Mbeya na ameungana na wenzake kikosini kwa ajili ya mechi ya kesho.

Pia msimu uliopita ilishuhudiwa Mayele akikosa tuzo hiyo dakika za mwisho huku George Mpole aliyekuwa akiichezea Geita Gold akitwaa kwa mabao 17 akimuacha bao moja na sasa staa huyo ameanza vita mpya na Ntibazonkiza wa Simba.

Ntibazonkiza alifikisha idadi hiyo baada ya juzi kufunga mabao matano kwenye ushindi wa 6-1 dhidi ya Polisi Tanzania na kuwa mchezaji pekee aliyeweka rekodi ya kufunga hatitriki mbili ligi kuu hadi sasa.

Kwa upande wake straika wa Yanga, Chrispin Ngushi amesema wao kama wachezaji wameona ushindani wa kiatu cha mfungaji bora na kwamba wanaendelea kumpa moyo mwenzao Mayele lakini kumsaidia ili kufikia malengo.

"Sisi tunajipanga kushinda mechi hiyo na timeliona suala la ufungaji bora na tunaendelea kumpa moyo na tutashirikiana kuhakikisha anapata tuzo hii" amesema Ngushi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: