Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kauli ya kwanza ya Dube baada ya kutua Yanga

Dube 1170x650 (1).jpeg Kauli ya kwanza ya Dube baada ya kutua Yanga

Mon, 8 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji Prince Mpumelelo Dube maarufu Mwana wa Mfalme, ni mali yetu kwa miaka miwili baada ya kusaini mkataba wa kuitimikia Young Africans SC.

Dube raia wa Zimbabwe, ana uzoefu na soka la Tanzania akiwa amecheza hapa nchini kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2020 hadi 2024.

Mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kucheza kutokea pembeni kushoto na kulia sambamba na namba tisa, mara ya kwanza anacheza Ligi ya Tanzania alitokea Highlanders ya kwao Zimbabwe.



Kuna mengi Wananchi wanayasubiri kutoka kwa Mwana wa Mfalme na hapa mwenyewe amefunguka mengi katika mahojiano maalum aliyoyafanya na YANGA APP muda mfupi baada ya kusaini mkataba.

YANGA APP: Unajisikiaje kuwa mchezaji wa Young Africans?

PRINCE DUBE: Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu, nimefurahi sana, unajua Yanga ni timu kubwa, kila mchezaji anatamani kucheza timu kama Yanga, hivyo nimefurahi sana, nataka nianze nikutane na wachezaji wengine, unajua hapa Kuna wachezaji wakubwa na Mimi muda mrefu sijacheza.

YANGA APP: Unasema kila mchezaji amekuwa na ndoto ya kucheza timu kubwa kama hii, je na wewe ilikuwa ndoto yako kucheza Yanga?

PRINCE DUBE: Nimekuwa nikitamani kucheza timu kubwa kama hapa Tanzania na nje ya nchi hii lakini kwa Tanzania nilikuwa nataka kucheza Yanga, kama mtu angeniuliza nataka kwenda wapi ningechagua Yanga.

YANGA APP: Kwa nini Yanga? Kwa sababu timu kubwa au kuna vitu vingi umeviona hapa?

PRINCE DUBE: Nimependa jinsi wanavyofanya mambo yao, mashabiki, unajua ukiangalia timu inavyocheza kuna kitu unakiona mbele ndio maana kila mchezaji anatamani kucheza timu kama hiyo.

YANGA APP: Unataka kupata mafanikio gani hapa Yanga ndani ya uwanja na nje ya uwanja?

PRINCE DUBE: Mimi kwanza nataka kushinda makombe, unajua kama mchezaji sio vizuri unashinda tuzo binafsi hivyo ni muhimu kushinda kombe kama timu, hivyo nadhani hii ndiyo nafasi naweza kushinda makombe hayo.

YANGA APP: Uko tayari kiasi gani kucheza Yanga ukizingatia kwamba umesema hapa kuna wachezaji wakubwa?

PRINCE DUBE: Nipo tayari sana tu, nishakaa muda mrefu sijacheza, hivyo huu ndio muda wangu kuonekana na kufurahia mambo mbalimbali, nimekuja hapa sio kushindana na mtu bali nimekuja kuongeza nguvu katika timu kusaidia kushinda mechi na kushinda makombe.

YANGA APP: Nieleze kwa ufupi sana ilivyokuwa safari yao kuja Yanga

PRINCE DUBE: Nimepita kwenye kipindi kigumu sana, watu walikuwa wanasema Dube anaenda Yanga, lakini muda wote huo nilikuwa sichezi huku nikitamani kuja hapa Yanga nicheze Mpira.

YANGA APP: Unawaambia nini mashabiki wa Yanga?

PRINCE DUBE: Mimi nataka kusema watusapoti muda wote kwa sababu kuna kipindi tutapitia wakati mgumu sana, naomba kuwe na sapoti na muda wote nitakapokuwa uwanjani nimevaa hii jezi nitafanya mambo yangu Kwa kutumia nguvu zangu zote kwa asilimia 100 kuwapa furaha mashabiki wetu.

Unajua nilipokuwa njiani kuja Yanga Kuna watu walikuwa wananitumia meseji kunipa moyo na wengi walikuwa mashabiki wa Yanga, hivyo nataka kulipa kile walichokuwa wakinipa, mimi ni straika najua watu wanataka kuona nikifunga, naomba Mungu anipe nguvu nifunge watu wafurahi mambo yaendelee.

YANGA APP: Umewahi kufanyiwa mahojiano na vyombo vingi vya habari hapa Tanzania ukitaja wachezaji uliotamani kucheza nao akiwemo Aziz Ki na Chama, wengine ni kina nani?

PRINCE DUBE: Ukiangalia pale Yanga kuna wachezaji wengi wakubwa sana kama unavyosema Aziz Ki, Chama, Pacome, Aucho, Mudathir, Nzengeli, kila mchezaji wa Yanga ni mkubwa na natamani kucheza nao, nilitaka kuja Yanga kufurahia baada ya kupitia kipindi kigumu sana, sasa hivi akili yangu ipo katika kufurahia mpira tu na mtu yoyote afurahi.

YANGA APP: Unadhani hii itakuwa timu ya aina gani kutokana na unavyoiona?

PRINCE DUBE: Ni timu ambayo italeta ushindani ikiwemo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wachezaji wengi Wana uzoefu wakiwa wameshacheza Ligi ya Mabingwa, mimi nimcheza japo sio sana, nipo hapa kwa ajili ya kuungana nao kusaidia timu isonge mbele tushinde.

YANGA APP: Una neno lolote Kwa viongozi na mashabiki wa Yanga?

PRINCE DUBE: Nataka kusema asante sana kwa kuniamini mabosi wa Yanga kunileta hapa hasa Rais Hersi amekuwa na mimi tangu siku ya kwanza, amenisapoti naona kuna viongozi wengine wamenisapoti, hivyo nashukuru kuwa hapa, nimekuja kufanya kazi.

YANGA APP: Unazungumza Kiswahili kilichonyooka, ushakuwa Tanzania?

PRINCE DUBE: Hapana, nimejifunza TU, nimekuwa na marafiki wananifundisha, unajua hapa Tanzania Kingereza sio sana, hivyo nimejifunza Kiswahili mpaka sasa najaribu kuongea kidogokidogo.

YANGA APP: Dube karibu sana Yanga

PRINCE DUBE: Asante sana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live