Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila, amesema kikosi chake kitaendelea kufanya mazoezi ya nguvu katika kipindi cha siku 20 ambacho Ligi Kuu Tanzania Bara imesimama kwa ajili ya kupisha kalenda ya kimataifa.
Ihefu FC ilianza msimu mpya kwa kufungwa na Geita Gold FC na mechi yake ya pili ikapata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbarali.
Katwila amesema lengo la kutosimamisha mazoezi ni kujiandaa na ushindani mkubwa uliopo na anataka kuona kikosi chake kinapata matokeo chanya katika kila mechi.
“Hii ligi msimu huu ina tofauti kubwa na msimu uliopita, ukiangalia timu zote zimejipanga vizuri na kila mtu anahitaji kufanya vizuri, tunahitaji kujiweka sawa kwa kufanya maandalizi mazuri kabla ya ligi kurejea kwa mara nyingine,” Katwila amesema.
Ameongeza anafahamu mechi ihayofuata dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma haitakuwa rahisi kwa sababu ya ubora wa wapinzani wao.