Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasongo: Ratiba, kanuni bado tatizo Ligi Kuu Bara

Tplboard Kasongo Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo

Mon, 12 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Bara imemalizika juzi Ijumaa huku Ligi ya Championship na First League zenyewe zilimalizika mapema. Yanga ni mabingwa, JKT Tanzania na Kitayosce zenyewe zilipanda kushiriki ligi kuu msimu ujao kutokea Champioship huku Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zikishuka daraja.

Yamefantika mahojiano maalumu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo ambaye ameelezea mambo kadhaa ya namna msimu wa 2022/23 ulivyokuwa kwao.

RATIBA

Anasema suala la ratiba bado ni changamoto kwao ingawa changamoto hiyo sio kubwa ukilinganisha na misimu ya nyuma.

"Ratiba ndiyo kila kitu kwenye ligi zetu, kuanzia klabu, Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hii inasaidia kurahisisha shughuli zetu za kila wakati, ratiba ni kipaumbele namba moja, tunalazimika kuwa na ratiba ambayo ina tija katika usimamizi na ufanisi wa michezo yetu yote kwa ligi zote.

"Miongoni mwa vitu ambavyo vinatupa kazi ngumu sana katika usimamizi na uendeshaji wa ligi zote ni ratiba, ni ngumu kwasababu ratiba itakayotangazwa iweze kupendezwa na kila mdau ambao ni klabu.

"Tupo kwenye uwiano mzuri isipokuwa kwenye zile ambazo zimeshindikana ndio utaona ratiba haijawa ratiba. Pia lazima utoe ratiba ambayo inaakisi ushiriki wa timu zetu michuano ya CAF, unapofikia hilo eneo mara nyingi ratiba zetu ndiyo hufikia kwenye changamoto kubwa.

"Huwa tunajipangia ratiba yetu kuwa lazima ligi ianze lakini huwa hatujui kitatokea nini kwenye michuano ya CAF ama FIFA, changamoto kubwa ni ratiba yetu ya michezo ya ndani kuakisi na ratiba za CAF ili kutoa nafasi kwa timu zetu zinazoshiriki michuano hiyo ikiwemo muda mdogo wa kwenda kucheza mechi nyingine."

Vipi kuhusu maboresho ya ratiba; "Wadau wengi wanasifikia ratiba haina viporo, sasa changamoto ni pale ambapo timu zinasubiriana, mnaposubiriana ligi inachukuwa muda mrefu na timu zinakaa muda mrefu hazichezi.

"Tunaangalia ni namna gani timu inaweza kukaa muda mchache bila kucheza, mfano mzuri hii ratiba ya kucheza fainali ya CAF ilibidi Yanga tuwasubiri kucheza raundi zilizobaki, msingi wake mkubwa kuondoa viporo vinginevyo timu zingine zingekuwa zimemaliza ligi hivyo kusingekuwa na usawa na tungetengeneza viashiria vya upangaji matokeo.

"Timu zetu kwa asilimia kubwa hazina uchumi mzuri, sasa tunajaribu kuangalia namna gani tunaweza kusaidia kama timu ina mechi mbili ama tatu labda Kanda ya Ziwa basi imalize mechi zote, ingawa mwisho wa siku huwezi kufanya kwa klabu zote hapo lazima sasa wengine waumie, kikubwa tunashukuru ushirikiano wa klabu maana wanakubali utekelezaji wa ratiba hata kama kuna changamoto."

MSIMU ULIVYOKUWA

Kasongo anafafanua namna msimu ulivyokuwa upande wao; "Kiukweli tumeenda vizuri pamoja na changamoto za ratiba, lakini upande wa msimu katika maeneo yote tukianza udhamini wametutendea haki, yale yote tuliyokubaliana kwenye mkataba wameyafanya kwa uweledi mzuri sana na wametimiza.

"Fedha zimetumwa kwa wakati kwa klabu, bodi na TFF wametuwezesha kwa wakati, wamefanyakazi kubwa sana, wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu, tumekuwa karibu sana na ligi zetu zote, tulianza msimu kwa kufungia viwanja vingi sana, kwa kuona ni namna gani tunatimiza kiu ya wadau wetu kwa kuona michezo inachezwa kwenye viwanja vizuri." anasema na kuongeza;

"Pia kutimiza takwa la Club License na hadi sasa uwanja mmoja wa Ruvu Shooting ulifungiwa na walituambia wana mpango mkubwa na uwanja wao, hivyo mechi 15 hawakucheza kwao, lengo ni kukidhi matakwa ya kikanuni. Hivyo hakukuwa na malalamiko kwa klabu juu ya kupata matokeo mabovu kutokana na viwanja."

KANUNI

Kasongo anaeleza kwamba suala la kanuni limekuwa changamoto kubwa kwa klabu, wachezaji na wadau wa soka nchini huku akifafanua pia matatizo yaliyojitokeza Ligi ya Championship huku baadhi ya viongozi wakifungiwa akiwemo Yusuph Kitumbo (aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Tabora) na kocha Ulimboka Mwakingwe.

Pia malalamiko ya Pamba FC juu ya Kitayosce kumtumia mchezaji aliyekuwa na kadi tatu za njano ilipocheza na Fountain Gate FC. Kwamba yote hayo ni matatizo ya kikanuni.

"'Huwa tunatoa semina nyingi za kujengenea uwezo kwa viongozi wa klabu, wadau tukiamini kanuni ndio msaafu kwa kila kitu, ila nilichogundua ni kwamba hayatoshi, hivyo tunapitia Ligi Kuu Tv ambayo huchambua mambo ya kanuni kila wiki, ili kuelemishana ili kupunguza makosa ya kikanuni, lengo letu ni kufikia makosa sifuri ya kikanuni kwa wachezaji, mashabiki na viongozi.

"Ni kama ilivyotokea ishu ya viongozi wa Gwambina juu ya kufungiwa uwanja wao na Kamati ya Leseni, kamati ilijiridhisha kuwa uwanja haukidhi, watambue Kamati ya Leseni ni chombo ambacho kinasimamiwa na FIFA wala hakiingiliwi na TFF ama Bodi ya Ligi, hivyo wakipitisha wao kwenu ni ruhusa kutumika.

"Kamati hiyo ikiteuliwa na Rais wa TFF na kupitishwa na Mkutano Mkuu basi hakuna chombo kitakachoingilia kwani wao wanasimamiwa na FIFA.

Kuhusu sakata la Kitumbo, Kitayosce na Fountain Gate, Kasongo anafafanua; "Kamati ya Maadili ina mamlaka ya kuadhibu timu. Kuna kamati mbili kwa nne za haki na zinajitegemea, Kamati ya Maadili ina Kamati ya Rufaa ya Maadili na Kamati ya Nidhamu ina Kamati ya Rufaa ya Nidhamu.

"Masuala ya mpira yanamalizwa na mahakama za kimpira ambazo ni Kamati ya Nidhamu ama Kamati ya Maadili ambavyo ndivyo vyombo vya haki. Kila kamati ina Mwenyekiti na Makumu wake na nawe wanasheria waliothibitishwa.

"Kuhusu Kitayosce na Fountain Gate kwenye masuala ya rushwa, wengine wameenda mbele kwanini Bodi ya Ligi kupitia Kamati ya Saa 72 hawajachukuwa hatua na wamekaa kimya, lile shauri lilivyotokea Fountain Gate walilalamika TFF ambao waliwasilisha Kamati ya Maadili.

"Na likiwa kwenye mahakama hizo hakuna chombo chochote kinachoweza kuingilia

jambo hilo, lilisikilizwa na kutolewa maamuzi, labda yatolewe na maelezo na si vinginevyo, ndio maana hatujafanya lolote maana kile ni chombo ambacho tupo chini yao. Hata kama kamati imekosea kutoa uamuzi hatuwezi kubadilisha"

Kuhusu Pamba kukimbilia FIFA, Kasongo anasema; "Hilo jambo lilikuwa Kamati ya Saa 72, ilijadili na kutoa maamuzi, changamoto iliyojitokeza kwenye maamuzi ya kamati nafikiri ni mgongano wa kanuni mbili zinazoelezea kitu kimoja.

"Kuna kanuni inaeleza kwamba malalamiko yoyote ya mchezo kutoka kwa mlalamikaji yatawasilishwa kwa kamishina wa mchezo kimaandishi na kusainiwa na mtoa malalamiko na yatawasilishwa Bodi ya Ligi pamoja na viambatanisho vyote vya ushahidi ndani ya saa 24.

"Pia mlalamikaji anaweza kuwasilisha malalamiko moja kwa moja Bodi ya Ligi ndani ya saa 72, hapo sasa kamati itaangalia malalamiko hayo yalipaswa kuwasilishwa kwa kutumia kanuni ipi, maamuzi ya Pamba yalitolewa na ile kanuni ya kuwasilisha ndani ya saa 24.

"Ni jambo ambalo tunapaswa kurekebisha kwa hizi kanuni zinazofanana ili kila mmoja apate haki yake, Pamba nafasi pekee ilikuwa ni kuomba marejeo ya hukumu yao vinginevyo waende FIFA kama walivyofanya, FIFA watasikiliza wataomba kanuni zetu na kutoa maamuzi yao." anasema Kasongo na kwamba tayari wamepata wadhamini wawili wa Ligi ya Championship na First League msimu ujao

UTALAWA/SOKA LA VIJANA

Anasema msimu ujao wamepanga kuweka mkazo maeneo mawili; "Utalawa na soka la vijana, ni eneo muhimu sana, tunaka viongozi wenye sifa, uzoefu na maadili mazuri, ambao watakuwa na mipango mizuri kuanzia miundombinu yao, wataliendelea vizuri soka la vijana.

"Wanaojua sheria na mambo muhimu, hivyo msimu ujao tutaangalia sana suala hilo kama utekelezaji wa club Lisencing na CAF walikuja kutoa mafunzo hayo kwa klabu, tulikuwa miongoni mwa nchi 17."

CAF MSIMU UJAO

"Yanga wametufanya kusogea renki za CAF tupo nafasi ya sita, tumejihakikisha kupelekea timu nne tena msimu ujao. Kwa mafanikio hayo kwetu ni namna gani tutahakikisha kutunza nafasi hizo nne na hata kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Singida Big Stars ni wageni kwenye mashindano haya lakini jambo pekee wanatakiwa kufanya maandalizi kwa maana ya usajili mzuri, ukiwa na timu bora unafanya vizuri pamoja na kuwa na rasilimali pesa ya kutosha.

"Mashindano ni magumu, yanahitaji pesa kwa ajili ya usafiri wa ndege ambao ni ghali, kulipa posho na mishahara kwa wakati kwa wachezaji wao, hivyo wajipange vizuri." anasema Kasongo

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: