Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kasi ya Mayele gumzo Kombe la Shirikisho Afrika

Mayele Caf.jpeg Straika wa Yanga, Fiston Mayele

Sat, 20 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Fiston Mayele ameendelea kuwasha moto kwenye michuano ya CAF msimu huu akiwa amefunga jumla ya mabao 13, yakiwamo saba ya mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na sita ya Kombe la Shirikisho akiifikisha Yanga fainali na kasi hiyo imemshtua kiungo mkabaji Mnigeria, Morice Chukwu.

Kiungo huyo wa Rivers United iliyong'olewa na Yanga kwenye robo fainali, alisema straika huyo kutoka DR Congo anatisha kwa aina ya uchezaji wake na kukiri ni mchezaji balaa zaidi kwa aliowahi kukutana nao kwenye michuano ya Afrika na kumtabiria kufika mbali ikiwamo kubeba tuzo ya CAF.

Nahodha msaidizi wa mabingwa wa Nigeria, alikutana na Mayele kwenye mechi mbili za robo fainali na straika huyo alifunga mara mbili ugenini na Chukwu alisema anaiona Yanga ikiandika historia Afrika kwa kubeba taji msimu huu huku Mkongoman huyo kufunika zaidi kwani ana kasi mno.

Akizungumza kiungo huyo anayevaa jezi namba 11 alisema Mayele ni kama anawatoa somo kwa wachezaji wa Afrika kwa aina ya uchezaji unaompa tumaini kocha na mashabiki kwa muda wowote kuwa ushindi utapatikana bila kujali ugumu wa mchezo.

"Namna ya ufungaji atazidi kufika mbali, ana kasi mjanja na nguvu pia hachoki haraka, hivyo kuwapa kazi mabeki wa timu pinzani kama alivyotupa sisi nyumbani, ila kwa Yanga mabeki wao na ni wazuri wanacheza kwa akili na nguvu, kitu kinachoibeba timu kufika mbali zaidi," alisema Chukwu na kuongeza;

"Yanga ina bahati kubwa kupata kikosi imara kama kile hata tulipocheza nao tuliwaona wachezaji namna walivyo bora na uwezo wa tofauti na ninaiona fainali ikiwa njema kwa upande wao," alisema Kiungo Morice.

Kwa upande mwingine beki wa Marumo Gallants, Mpho Mvelase alikiri wamezidiwa na Yanga juzi walipofungwa nyumbani kwao mabao 2-1 na kukiri Mayele ndiye aliyewang'oa michuanoni kwa jinsi alivyocheza huku akisema anatamani kuja kuichezea timu hiyo akiiipa nafasi ya ubingwa wa CAF.

"Nimeikubali sana Yanga kwani ni timu yenye wachezaji na ubora bila kusahau washambuliaji wakali akiwamo yule namba 9 (Mayele) walitutoa jasho mwanzo mwisho wa mchezo na wakicheza hivi basi wataweka rekodi mpya Afrika na Tanzania kwa kutwaa ubingwa wa CAF," alisema Mvelase.

Marumo ilikuwa haijapoteza mechi yoyote nyumbani msimu huu kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lakini mabao ya Mayele na Kennedy Musonda yalowatibulia na Yanga kusonga mbele ikitinga fainali na sasa itavaana na USM Alger ya Algeria kati ya Mei 28 na Juni 3.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live