Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaseke ataka kusaini Simba

Kaseke Yanga Bye Bye Deus Kaseke

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Staa wa Singida Big Stars, Deus Kaseke amefichua jambo zito. Kumbe kuna wakati alitaka kutoroshwa na Simba.

Kaseke anacheka kisha anasema tukio la yeye kutaka kutoroshwa hatolisahau kwa sababu anakumbuka Yanga ilimtumia tiketi ya kwenda Dar lakini viongozi kadhaa wa Simba walitaka kumchukua uwanja wa Ndege.

Anasema alishangaa kujua watu wa mpira wanajua kila hatua ambayo anapiga kwani vitu vingine alikuwa anafanya bila kumuaga mtu yoyote.

“Nashuka tu kwenye ndege inaingia meseji whatsapp naangalia ni namuona (anamtaka kiongozi wa Simba) ananiambi nipite mlango wa nyuma maana Yanga wapo mlango wa mbele lakini mimi nilimwambia hata kama nipo nao sitosaini hadi niongee nae;

“Natoka nakutana na Yanga moja kwa moja tulienda pale Jangwani klabuni wakataka nisaini lakini mimi bado nikagoma.”

APAMBANISHWA NA MWALYANZI

Kaseke anasema kumbe licha ya Yanga na Simba kuonyesha kumhitaji bado timu hizo zilikuwa zinampigia hesabu mchezaji mwenzake Peter Mwalyanzi ambaye alikuwa nae Mbeya City.

Mshambuliaji huyo anasema wakati yeye anaingia usiku Mwalyanzi aliingia asubuhi akiletwa na Simba.

“Yanga ilinipeleka hotelini na baadae viongozi wake waliondoka lakini wakaja wa Simba, pale kumbe Yanga ilikuwa imewacha watu wake kwahiyo walipata taarifa;

“Zilikuja gari tatu na wakanichukua kwa kunificha na kunipeleka katika hoteli moja Sinza halafu wakaniacha na mlinzi.”

AWAPAMBANISHA SIMBA NA YANGA

Baada ya asubuhi kufika Kaseke alichukuliwa na kupelekwa tena Jangwani lakini akiwa njiani alipokea ujumbe mfupi wa(anamtaja kiongozi wa Simba) na kumuuliza anaenda wapi.

Hali hiyo ilionekana kuzidi kumshangaza Kaseke kwa sababu kila hatua ambayo ilikuwa inapigwa bado viongozi wa Simba walikuwa wanajua.

“Nilifika pale Yanga iliniwekea ela ndogo mimi niligoma kusaini nikatoka nje, kumbe Simba imeweka mtu nje kwahiyo nilivyotoka nikapokea simu ya marehemu Hans Pope akiniambia nitapata nyumba (Kupangiwa), gari, ofa ya maana na mshahara mzuri;

“Wakati naongea na Pope hapo hapo anatokea Nyika na kunisikia nikiongea kwahiyo aliponiuliza nini kinaendelea nilimwambia basi alilazimika kutoa ela yake mfukoni kwa sababu alisikia ambacho Simba iliniwekea.”

Kaseke anasema;”Nilisaini Yanga kwa wakati ule walikuwa wanatoa ela kwa mafungu lakini mimi walinipa kwa asilimia 80 kwahiyo ilibaki kidogo tu.”

YANGA YAACH ALAMA KWAKE

Kaseke bila kupepesa macho anasema katika maisha yake ya mpira Yanga imembadilisha hivyo imeacha alama kwa wakati wote.

Mshambuliaji huyo anasema sio sawa kuweka wazi lakini kwa sasa anaendesha maisha yake vizuri na kama ikitokea siku moja atapata nafasi basi atarejea.

“Naiheshimu Yanga na imenipa maisha mazuri, kuna vitu tofauti tofauti ambavyo vinaweza kukufanya usirudi lakini vinavumilika kwa sababu wapo watu ambao wanaharibu heshima ya mtu,”anasema Kaseke.

Kaseke anasema ameishi maisha mazuri akiwa na Yanga hivyo kuna vitu vingi ambavyo amevipata akiwa katika timu hiyo na anajivunia na hawezi kuacha kushukuru.

PLUIJM AMREJESHA SINGIDA BS

Kaseke ni kama vile anawezana na kocha Hans Pluijm wa Singida Big Stars kwani baada ya mkataba wake kumalizika mchezaji huyo kwa sasa yupo naye wakiendelea kufanya kazi pamoja.

Pluijm na Kaseke awali waliwahi kufanya kazi pamoja walipokuwa Singida Utd na awali Yanga.

Akizungumzia hilo Kaseke anasema yeye na kocha huyo inawezekana wanaendana katika vitu vingi ndani ya uwanja na ndio maana inakuwa ni rahisi kwake kumhitaji.

“Kocha anaona mimi nafaa kwenye timu yake na ndio maana ninapokuwa nae tunafanya kazi yetu vizuri hata kama haijachukua ubingwa basi tunakuwa sehemu nzuri kama hivi;

“Siri kubwa ya kufanya vizuri ni kuhakikisha unashinda mechi zako za nyumbani, ukifanya hivyo lazima uwe sehemu nzuri katika msimamo wa Ligi.”

SINGIDA APATA JERAHA LA KWANZA

Kaseke ni miongoni mwa wachezaji ambao siyo rahisi kupata majeraha na mchezaji huyo anaweka wazi kwenye maisha yake ya soka hajawahi kukaa nje ya uwanja kwa kuumia.

Mshambuliaji huyu ambaye alikaa kwenye kikosi cha Yanga misimu miwili, Yanga miwili, Singida mmoja na Yanga tena miaka mine kote huko hajawahi kuumia hadi msimu huu alipojiunga na Big Stars.

“Mungu ni mwema upande wangu kwa sababu huwezi amini mimi tangu nianze kucheza mpira sikuwahi kuumia yani hadi hapa juzi ndio nimeumia nikiwa na Singida;

“Nimekaa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja nikiwa hapa sasa na mimi nikisema fulani haipendezi, kikubwa Mungu ndio amenifanya nicheze kwa muda mrefu na lingine ni kujitunza vitu ambavyo havitakiwi kufanyika sana.”

SINGIDA HAKUNA PRESHA, TIMU INAPAMBANIWA

Kaseke anasema yupo Singida na kwa sasa akili yake yote ipo kwenye timu hiyo hivyo wanaipambania kuhakikisha inamaliza katika nafasi za juu.

“Nipo Singida maisha yangu yanaendelea, nacheza lakini pia napata kile ambacho ninakihitaji kwa wakati huu, kikubwa kilichobaki ni kuipambania timu na hapa hakuna presha,”anasema Kaseke.

Kiraka huyu anaongeza akisema siri kubwa ya kwao kufanya vizuri ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mechi zao za nyumbani na ndio kilichowabeba.

“Nenda kaangalie sisi mechi zetu za nyumbani matokeo yake yapoje ndipo utanielewa, tunataka tushinde kila mechi na hilo ikifanya timu yoyote ile lazima iwe nafasi za juu;

“Angalia hata Simba na Yanga mechi zao za nyumbani huwa wanafanyeje basi ndio maana kila siku zipo juu huko, nyumbani lazima washinde halafu ugenini wapambane kupata hata sare.”

Kaseke anasema timu yao ana imani itazidi kuwa bora kutokana na wachezaji ambao wanasajiliwa na namna ambavyo wanajituma ndani ya uwanja muda wote.

NAMBA 10 ANAIPENDA, KUSHOTO UHAKIKA

Kaseke ni mchezaji ambaye anaweza kucheza zaidi ya nafasi mbili ndani ya uwanja huku akimudu vyema namba 10, 7 na 11, aliweka wazi namba 10 anaipenda lakini 11 anakuwa balaa.

“Mimi nikicheza kushoto nakuwa huru hasa kwenye kutoa pasi za mabao, nikicheza namba 10 huwa nafunga sana kwa hiyo hizo namba mbili huwa nazipenda sana,” anasema Kaseke.

Kaseke anasema ;”Ikitokea nimepangwa sehemu nyingine yoyote nalazimika kucheza kwa sababu mimi ni mchezaji na lazima nitimize majukumu yangu.”

Mshambuliaji huyu kuna muda alilazimika kutumika kucheza kama kiungo mshambuliaji katika kikosi cha Yanga ilipotokea eneo hilo kuna shida.

AMTAJA MWAMBUSI

Mshambuliaji huyu amefundishwa na makocha mbalimbali katika Ligi Kuu Bara na Ligi Daraja la kwanza lakini hajawahi kuweka wazi yupi ni kocha wake bora kwa mara zote.

Mwanaspoti lilimfanya mchezaji huyu azungumze kwa kumtaja kocha wake bora kwa muda wote.

Kaseke anasema kwake yeye kocha wake bora wa muda wote ni Juma Mwambusi kwa sababu ndiye ambaye amemtoa katika maisha yake ya soka.

“Mimi nimetoka na Mwambusi chini na kuja nae juu kwahiyo lazima awe bora wakati wote kwangu, ni kocha mshindani ambaye hakubali kushindwa kirahisi,”anasema Kaseke.

ISINGEKUWA SOKA NI MWALIMU

Kaseke anasema isingekuwa soka leo hii angekuwa mwalimu wa shule ya msingi kwa sababu baad ya kumaliza elimu yake ya Sekondari alisomea ualimu.

Mshambuliaji huyu anasema alipomaliza shule Tanzania Prisons ilimtaka kumsajili moja kwa moja na kuweka ahadi ya kazi lakini alikataa kujiunga nayo kwa sababu na ndoto ya kucheza mpira.

“Nilisoma mwaka mmoja tu lakini nilikuwa naona kama nalazimishwa tu, shule ya msingi kusoma ualimu wake ilikuwa miaka miwili kwahiyo mimi nilisoma mwaka;

“Mzee wangu nilikuwa nagombana nae sana kwahiyo ikabidi bibi aingilie na kaka yangu ndio ikabidi aniache na baada ya mwaka (2011) ndio Prisons ikanitaka, nakumbuka ilitoka kupanda baada ya kushuka msimu wake wa nyuma.”

Kaseke anasema wakati huo kocha Jumanne Charle baada ya kumuona aliwaambia aende katika timu ya vijana huku wakimuweka katika uhakika wa ajira lakini hakuwa tayari.

“Baada ya hapo nikaenda zangu Polisi Iringa (Lipuli) baada ya hapo nikarudi Mbeya nikacheza Mbeya City ndipo maisha ya soka yanaendelea hadi sasa;

“Mzee anajivunia kitu ambacho anakiona sasa kupitia maisha yangu ya soka ambayo niliyonayo japo alikuwa hapendi nicheze mpira.”

Kaseke anaongeza akisema;”Baada ya maisha yangu ya mpira nikiona inatosha nitageukia zaidi kwenye upande wa Biashara.”

BAO LAKE BORA

Kaseke licha ya kuwa na misimu zaidi ya nane kwenye Ligi Kuu amelitaja bao moja tu kuwa ni analikubali katika maisha yake yote ya soka tangu aanze kucheza soka.

Mshambuliaji huyu anasema katika maisha yake yote ya soka hawezi kulisahau bao ambalo aliifunga Azam katika fainali ya kombe la Azam hadi leo.

“Ilikuwa ni fainali ile nakuambia zilipigwa pasi nyingi sana, nilimpa pasi Kamusoko yeye akampa Ngoma ambaye akamrudishia kisha akampa Msuva na mimi nilitokea kulia na kufunga;

“Nalikumbuka bao lile kutokana na namna ambavyo lilitengenezwa hadi nafunga.”

DABI YA SIMBA NA YANGA NOMA

Kaseke amecheza dabi ya kwanza akiwa na Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons lakini kwa muda mrefu amekuwa sehemu ya dabi ya Yanga dhidi ya Simba.

Kwa hapa nchini na Afrika Mashariki, dabi ya Simba na Yanga inatajwa kuwa tishio na hata yeye mwenyewe amekiri.

“Dabi ya Simba na Yanga ndio bora siku zote, kule ni dabi lakini ushindani unapotea tofauti na miaka ya nyuma, halafu huku huwezi kuzoea dabi;

“Nakuambia Simba na Yanga hata ucheze leo halafu ucheze na kesho kutwa hakuna mchezaji ambaye anapenda mechi hizo labda kama tupo tofauti.”

Kaseke anasema;” mechi za Simba na Yanga zinaweza kukubeba au kukupoteza kwahiyo zinavyokuja unaweza ukakuta unapotea moja kwa moja”.

HAPENDI TIMU NYINGI

Kaseke hadi sasa amecheza jumla ya timu nne tu ambazo ni Mbeya City, Yanga, Singida Utd na Singida Big Stars na ameweka wazi yeye sio muumini wa kucheza timu nyingi.

Mshambuliaji huyo anasema kama mchezaji ukicheza timu nyingi inakuwa ni ngumu kuheshimika kwa sababu kila mtu anakuwa amekuzoea.

“Ukicheza timu nyingi heshima inapotea kwa sababu kila mtu anakuwa amekuzoea na watakujua sana , mimi ikitokea nimemalizia hapa sio mbaya kwangu;

“Sina muda mwingi sana wa kucheza mpira kwa sababu nimeshatumika sana hapa kwenye Ligi.”

AFUNGUKA KUIKACHA SIMBA,YANGA KUMTOROSHA

Kaseke awali alipokuwa na Mbeya City alianza nayo ikiwa Ligi Daraja la kwanza mwaka 2012/2013 na alipanda nayo hadi Ligi Kuu akicheza hadi msimu wa 2014/2015.

Mshambuliaji huyo kwenye msimu wa 2014/2015 anasema kama angekuwa na mihemko basi angesaini Simba mapema lakini hakufanya hivyo.

“Ilikuwa dirisha dogo nakumbuka Simba ilinitumia tiketi ya ndege, alikuwa Kaburu lakini mimi niliwaambia siwezi kusaini kwa sababu timu ipo nafasi mbaya na walinielewa;

“Nilikuja hadi Dar na Yanga ilipojua nipo basi ilinifata hoteli moja pale Ubungo na kunipeleka kule Protea (Masaki) lakini bado nilikuwa na msimamo kwamba siwezi kusaini kwa wakati ule.”

Kaseke anasema kwa wakati ule kwenye vuta ni kuvute za timu hizo alijikuta akitengeneza Sh 5 milioni ikiwa kama ela tu ya mkononi ya kuondokea.

YANGA YAMKOMALIA

Licha ya Kaseke kuonyesha hayupo tayari kusaini labda kama familia yake itakubali basi Yanga iliamua kumtuma muwakilishi wake Ally Mayay ambaye wakati huo alikuwa kwenye kamati ya usajili Yanga (Sasa Mkurugenzi wa michezo nchini).

Kaseke anasema walipofika Mbeya, Mayay alikuwa na mkataba wake bado lakini hakuweza kusaini kwa sababu bado aliipa kipaumbele Simba kutokana na mazungumzo ya awali na Kaburu.

“Simba kwa sababu ndio ilikuwa ya kwanza kwangu nilikuwa naipa kipaumbele labda tushindwane kwenye mazungumzo kwahiyo bado nilikataa kusaini mkataba wa Yanga.”

Kaseke anasema Ligi ilipomalizika (2014) Azam nayo ilionyesha nia ya kumuhitaji lakini mazungumzo yao hayakuwa mazuri.

“Nakumbuka nilipigiwa simu na Kawemba (Saad) lakini mazungumzo yetu hayakuwa mazuri kwahiyo hatukukubaliana chochote kile badala yake nikaendelea na Yanga na Simba.”

YANGA ILIKUWA SEHEMU SAHIHI

Kaseke anasema licha ya Simba na Yanga kuhitaji huduma yake mwisho wa siku alipoona na Mwalyanzi anahusishwa ilibidi atulize kichwa na kuangalia sehemu ambayo ataenda kucheza mpira.

Mshambuliaji huyo ilibidi aichague Yanga kwa sababu wakati ule ilikuwa bado haina ushindani wa kutosha nay eye alihitaji sehemu ambayo itamvumilia.

“Kwahiyo hii nayo ni sababu ambayo ilinifanya nisaini Yanga, si unaona mwezangu hakucheza kwa muda mrefu pale kwa sababu hawakumvumilia;

“Naweza kusema kwa upande wangu Yanga ilikuwa sehemu sahihi sana kwangu.”

ALIKOTOKEA

Kaseke alianza kucheza soka katika timu ya Polisi Iringa baadaye Lipuli mwaka 2011/12 kisha baadaye alienda Mbeya City msimu wa 2012/2013 na kuipandisha Ligi Kuu.

Akiwa na Mbeya City alicheza hapo na baadaye alionekana na kuziingiza vitani Simba na Yanga kisha akasajiliwa na Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti