Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Juma Kaseja ambaye kwa ni kocha wa makipa Kagera Sugar, anafurahishwa na utendaji kazi wa Djigui Diarra na Aishi Manula, huku akiwataka walio nyuma yao kukaza buti.
Kaseja alisema hayo kwenye hafra ya tuzo za msimu huu, zilizofanyika Tanga, aliwachambua Diarra na Manula kwamba wameacha gepu kubwa dhidi ya makipa wengine, kulingana na viwango vyao vya kuzisaidia timu zao.
"Kiukweli Diarra simdai, kwani amefanya kazi kubwa kuna wakati nafurahia kumuona anavyodaka vivyo hivyo na kwa Fiston Mayele ambaye kiwango chake kimekuwa msaada mkubwa kwa Yanga.
"Kwa upande Manula ni kipa mzuri sana na umri wake unamruhusu kufanya makubwa zaidi kwenye soka, wengi wanajiuliza kwa nini haendi kucheza nje, nafasi ya kipa siyo rahisi ingawa kwangu naona anastahili kabisa ni suala la muda na nafasi,"alisema.
Kuhusu yeye kucheza alisema bado anaona anaweza akadaka vizuri, lakini ameamua kukaa pembeni na kuwapisha wengine kuonyesha vipaji vyao, kwani kila kitu amekifanya haoni kipya.
"Ipo hivi kuna wakati unakifu, nikiendelea kufanya sioni jipya, watakaokuja ndio wataonekana wana mapya na yangu ya zamani, hivyo nipo mulemule kwani kwa sasa ni kocha wa makipa," alisema.
Kwa upande wa Manula aliwahi kusema alikuwa anamfuatilia Kaseja na alijifunza mambo mengi kutoka kwake "Kaseja ni kipa mwenye nidhamu ya juu na kazi yake, nakumbuka wakati naitwa Stars nilikuwa mdogo hivyo nilikuwa najifunza vitu vingi kwake."