Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaseja apangua penalti, Taifa Stars yafuzu makundi Kombe la Dunia

74806 Kaseja+pic

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kipa Juma Kaseja ameonyesha umahiri wake wa kudaka penalti baada ya kuokoa penalti moja na kuiongoza Taifa Stars kuitoa Burundi kwa penalti 3-0 baada ya mechi hiyo kumalizika kwa sare 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Ushindi huo unaifanya Taifa Stars kufuzu hatua ya makundi ya kuwania kutinga fainali za Kombe la Dunio zitakazofanyika mwaka 2022 nchini Qatar.

Katika dakika 90 za mchezo huo wa marudiano baina uliochezwa uwanja wa Taifa, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 huku mchezo wa awali uliochezwa jijini Bujumbura ambapo pia walitoka sare hivyo kufanya timu hizo kuwa na idadi sawa ya magoli.

Baada ya dakika 90 kumalizika, timu hizo ziliongezwa dakika 30 na kumfanya zichezwe dakika 120 ili kumpata mshindi ambapo pia kwa dakika hizo za nyongeza hakupatikana mbabe hadi ilipopigwa mikwaju ya penalti.

Zikiwa zimekaribia dakika chache kumalizika kwa mchezo huo, Burundi walifanya mabadiliko ya kipa ambapo alitoka Ndikumana Justin na kumwingiza Jonathan Nahimana anayeidakia KMC pamoja na Kaseja.

Makipa hao wote wawili wa timu moja walikaa langoni lakini Kaseja alikuwa mwiba kwao kwani aliokoa penalti zote zilizopigwa na Burundi na kufanya Stars ifuzu hatua hiyo kwa penalti 3-0.

Pia Soma

Advertisement

Panalti za Stars zilipigwa na Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michael wakati penalti zilipanguliwa na Kaseja ambaye ni mtaalamu wa kupangua penalti kwa makipa nchini.

Katika mechi hiyo, timu zote mbili zilifanya mabadiliko machache kwenye vikosi vyao vilivyoanza kutoka katika vile ilivyokuwa kwenye mechi ya kwanza kule Burundi.

Kwa upande wa Stars, Hassan Kessy na Iddi Selemani 'Nado' walianza kuchukua nafasi za Himid Mao na Haruna Shamte wakati upande wa Burundi, kipa Ndikumana Justin, Amissi Mohamed na Fiston Abdulrazack walianza badala ya Kwizera Pierre, Jonathan Nahimana na Bimenyimana Caleb.

Burundi walionekana kuwa na hesabu za kushambulia zaidi kwani walianza na kikosi chenye wachezaji watano ambao kiasili ni washambuliaji nao ni nahodha Saido Berahino, Cedric Amissi, Fiston, Amissi na Kanakimana Bienvenu.

Kiu yao ya kusaka mabao walianza kuionyesha dakika ya kwanza tu ya mchezo baada ya kufanya shambulizi kali langoni mwa Stars kupitia kwa Kanakimana lakini shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango.

Shambulizi hilo la Burundi lilikuwa ni la kulipa lile la Stars ambalo Hassan Dilunga alipoteza nafasi muhimu ya kuipatia bao la kuongoza baada ya kupiga shuti lililombabatiza beki wa Burundi, Nsabiyumva Fredric.

Baada ya hapo ni Stars ambayo ilikamata mchezo kwa kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi na kutengeneza nafasi ambazo hazikutumiwa vyema na safu yake ya ushambuliaji, kumaliza mechi mapema.

Kama washambuliaji wa Stars wangekuwa makini, mashambulizi matatu yaliyofanyika ndani ya muda wa dakika nne yangezaa angalau bao moja.

Mashambulizi hayo ni lile la dakika ya nne lililofanywa na Saimon Msuva ambaye alijaribu kulazimisha kupenya kuingia kwenye lango la Burundi lakini beki, Nsabiyumva aliokoa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Dakika mbili baadaye, Dilunga alipiga shuti lililookolewa na mabeki wa Burundi na kuzaa kona ambayo iliunganishwa kwa kichwa na Mbwana Samatta lakini mpira huo ulitoka nje.

Kana kwamba haitoshi, katika dakika ya nane ya mchezo, Samatta alimpenyezea Msuva krosi nzuri ambayo wakati mshambuliaji huyo akiwa kwenye harakati za kuimalizia, kipa Ndikumana aliwahi na kuidaka krosi hiyo.

Mashambulizi ya Stars yaliendelea mfululizo langoni mwa Burundi ambayo ilionekana kucheza kwa nidhamu kubwa katika safu yake ya ulinzi ambayo ilihakikisha haifanyi makosa ambayo yangepelekea kuruhusu bao.

Hata hivyo juhudi za Stars zilizaa matunda dakika ya 29 ya mchezo baada ya kupata bao la kuongoza kupitia Samatta.

Samatta alitumia vyema mpira wa kona uliochongwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' kuunganisha kwa kichwa na kuiandikia Stars bao la kuongoza.

Baada ya kuingia bao hilo, kasi ya Stars ilionekana kupungua tofauti na ilivyokuwa dakika za mwanzo za mchezo jambo lililowapa mwanya Burundi kurudi mchezoni na kuanza kupishana na wenyeji hao.

Makosa ya safu ya ulinzi ya Stars katika kuwadhibiti washambuliaji wa Burundi, yaliwazawadia bao la kusawazisha wapinzani wao dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.

Bao hilo lilifungwa na Fiston ambaye aliunganisha vyema pasi ya Kanakimana aliyemtoka Tshabalala upande wa kushoto.

Sare hiyo ya bao 1-1 ilidumu hadi mwamuzi Norman Matemera kutoka Zimbabwe alipopuliza kipyenga cha kuashiria mapumziko.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Kessy alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea faulo, Amissi.

Wachezaji wa Stars mara mbili walimlalamikia mwamuzi Matemera ikiwa ni madai ya penalti moja likiwa ni lile la dakika ya 11 ambapo Dilunga aliangushwa na Nsabiyumva na mwamuzi huyo kuamua kona na mara ya pili ilikuwa ni kupitia shambulizi la Msuva ambapo ilionekana kama beki Nshimihirimana David amenawa ndani ya eneo la hatari.

Stars waliingia kipindi cha pili wakiwa na kasi kama ile waliyoanza nayo kipindi cha kwanza lakini bado utulivu safu ya ushambuliaji ilikuwa ni tatizo kutokana na nafasi zilizokuwa zikipotea.

Dakika ya 60, ilionekana kama Nshihirimana amenawa mpira wakati alipokuwa kwenye jitihada za kuokoa krosi ya Tshabalala lakini licha ya malalamiko ya wachezaji wa Stars, mwamuzi aliamuru kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mnamo dakika ya 61, Stars ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Dilunga nafasi yake ilichukuliwa na Farid Musa.  Stars waliendelea kushambulia zaidi kupitia pembeni mwa uwanja lakini idadi kubwa ya krosi walizopiga ziliokolewa na walinzi wa Burundi.

Kutokana na majeraha ya beki wao Racanamwo Joel, Burundi walilazimika kumfanyia mabadiliko dakika ya 66 nafasi yake ilichukuliwa na Ngando Omar ambapo dakika mbili baadaye nahodha wao Saido alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kessy.

Stars ilifanya mabadiliko ya mwisho dakika ya 70 na 72 kwa kuwatoa Tshabalala na Abubakar Salum nafasi zao zilichukuliwa na Gadiel Michael na Shaban Chilunda.

Kwa upande wa Burundi, dakika ya 78 walimtoa Fiston aliyeumia na nafasi yake ilichukuliwa na Bimenyimana Caleb huku dakika ya 86 walimtoa Kanakimana na kumuingiza Shasir Nahimana.

Stars waliendelea kumiliki mpira na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo hayakuzaa mabao.

Kwa upande wa Burundi wenyewe waliamua kucheza kwa kutumia mbinu ya kufanya mashambulizi ya kustukiza langoni mwa Stars ambayo yalionekana tishio mno kwa wenyeji.

Miongoni mwa mashambulizi hayo ni lile la dakika ya 89 ambapo Shasir alimtengea pasi nzuri Caleb ambaye alipiga shuti lililookolewa kwa ustadi na Juma Kaseja na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Licha ya mwamuzi wa mezani Brighton Chimene kutoka Zimbabwe kuongeza dakika nne, mechi hiyo ilimalizika kwa sare hiyo ya bao 1-1 na hivyo kulazimika mechi hiyo kwenda dakika 30 zanyongeza ili kumpata mshindi kufuatia timu hizo mechi ya kwanza kumalizika kwa sare kama hiyo jijini Bujumbura.

 

Stars

Juma Kaseja, Hassan Kessy, Mohamed Hussein, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Iddi Selemani, Abubakar Salum, Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Hassan Dilunga.

Burundi

Ndikumana Justin, Diamanti Ramazani, Racanamwo Joel, Nsabiyumva Fredric, Nshihirimana David, Bigirimana Gael, Amissi Cedric, Kanakimana Bienvenu, Berahino Saido, Abdulrazack Fiston, Amissi Mohamed

 

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz