Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kaseja: Sijastaafu kucheza soka

Juma K Juma Juma Kaseja

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kula vizuri, kupumzika kwa wakati, mazoezi ndiyo siri pekee ya kipa mkongwe nchini Juma Kaseja kukaa golini kwa miaka mingi na hadi sasa bado ana uwezo huo ingawa amepumzika kwa muda.

Katika soka la Bongo na hata Afrika basi jina la Kaseja wengi wanalifahamu kutokana na uwezo wake wa kukaa langoni hasa alikuwa Simba na Taifa Stars timu ambazo amezitumikia kwa miaka mingi.

Kaseja miongoni mwa wachezaji wenye misimamo yao alizungumza mambo mbalimbali katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa mambo aliyoyazungumzia ni suala la kustaafu ambalo linazungumzwa juu yake ambapo yeye anasema;

"Mwaka jana sijacheza tangu nilipomaliza ligi na KMC niliona nisichanganye mambo ya usajili maana mkataba wangu ulimalizika na nilikuwa naenda kusoma, niliporudi kwenye kozi Mecky Mexime aliniita nikamsaidie Kagera Sugar, majuzi juzi nimecheza mechi ya Samakiba mashabiki wameniambia nirudi kucheza.

"Sasa nimewaachia kazi mashabiki nirudi ama niendelee na shughuli zangu zingine, lakini mimi sijawahi kutangaza rasmi kustaafu kucheza, mwili wangu unaniruhusu kucheza maana bado nina nguvu na ubora wa kucheza.

"Nikipata nafasi ya kucheza nitacheza, nikikosa ndipo nitatangaza rasmi, mimi ni kama Zlatan, De Brune leo anacheza huku anasoma, hivyo unaweza ukaniona hata msimu ujao nipo uwanjani nacheza.

"Najiamini kuwa nacheza kwasababu nazingatia mambo muhimu kama kula, mazoezi, kupumzika ndo vitu ambavyo vinanifanya niwe hivi, cha kwanza kabisa ni chakula, usizungumze mazoezi kabla hujazingatia mlo wako ukoje, maana wengine kwenye suala la kula hawazingatii."

SIMBA 2, YANGA 2

Kaseja amecheza timu nyingi tangu aanze kucheza soka la ushindani kama Moro United, Mtibwa Sugar, Simba, Yanga, Mbeya City, Kagera Sugar na KMC lakini Simba na Yanga ni timu ambazo amezichezea mara mbili kwa vipindi tofauti, yaani kila timu ameichezea awamu mbili.

"Nimecheza Simba 2003 hadi 2007 nikaenda Yanga, nikarudi tena Simba 2009 hadi 2013 nikaondoka tena kwenda Yanga, Simba sikufikisha miaka 10 maana kila timu nimeichezea mara mbili.

"Maisha yetu yanategemea mpira, mpira ndiyo kila kitu sina kazi nyingine yoyote zaidi ya mpira, hivyo mpira ndiyo unaendesha maisha yangu na familia yangu ambao ni wazazi, ndugu zangu, mke na watoto.

"Niliangalia baadhi ya waliotangulia kucheza mpira baada ya mpira maisha yao yanakuwaje, yakanipa funzo nikahisi si jambo baya kutoka sehemu moja kwenda nyingine kupigania mkate wangu, hivyo sio kitu kibaya ndio maana nilitoka Simba na kwenda Yanga."

"Simba niliondoka kwa amani na bahati nzuri mchakato wa kwenda Yanga baadhi ya viongozi wa Simba walikuwa wanajua, nilipata ofa niliyopewa Yanga walisema kwa pesa wanayokupa wao sisi hatuna na hatuwezi kukupa, walilidhia japo iliwauma kwani nilikuwa mchezaji tegemeo na kipenzi cha watu lakini hakukuwa namna yoyote ya kunizuia," anasema na kuongeza

"Ni miaka mingi na kwa kipindi kile ilikuwa ni pesa nyingi sana, nadhani kwa msimu ule ndiyo wachezaji walianza kusajiliwa kwa Dolla nilipewa Dolla 30,000 msimu wa 2007 ligi ilivyogeuka kuchezwa katikati ya msimu."

KILICHOMPATA YANGA

Kaseja anasema maisha ndani ya Yanga hayakuwa ya furaha kwake ambapo anaeleza;

"Nilipata wakati mgumu nilipokuwa Yanga nilionekana kama mamluki, hata nikicheza na kufanya makosa ya kawaida ya kimchezo walichukulia kama makusudi, kwa kweli ilinikosesha raha lakini niliumbwa mwanaume na mwanaume ni kupambana, ninachoshukuru msimu nilioenda Yanga ndiyo walichukuwa ubingwa.

"Bao ambalo liliihakikishia Yanga kuchukuwa ubingwa nilifunguka mimi pale CCM Kirumba dhidi ya Toto African, tulishinda bao 2-1, nilifunga moja na lingine nilidaka penalti ambayo ningeshindwa tungetoka sare na wasingetangaza ubingwa siku hiyo, Yanga walitangaza ubingwa kabla ya mechi tano kumalizika.

"Bao nililofunga kwanza siku hiyo mvua ilinyeesha sana, nilidaka nikapiga kaunta attack kipa wa Toto African akajaribu kurudi nyuma kudaka mpira ukamtoa likawa bao.

"Pia mechi ya Mtani Jembe uliibua maneno mengi sana, mchezo wa mpira ni wa makosa, nilifanya kosa nikaruhusu bao niliambiwa nimefungisha makusudi, wengi waliniosapoti ni wale hasa wanaonifahamu namna ninavyocheza na kuamini katika ubora wangu na utaratibu wa maisha na kazi yangu, tofauti na mashabiki wanamfahamu Juma, iliniuma ila sikuvunjika moyo.

"Nilisaini mkataba wa mwaka mmoja tu hivyo ulivyomalizika nikaamua kuondoka, kiukweli sikuwa na furaha ya kuendelea kuwepo Yanga hivyo nilirudi Simba, hakukuwa na tatizo maana niliaga vizuri."

KURUDI YANGA

Anasema kuwa baada ya kumaliza mkataba Simba alipata ofa tena Yanga wakati huo Yanga ikiwa na kocha mpya Ernie Brants na walikuwa wanajiandaa na michuano ya CAF.

"2014 nilienda Yanga ambako sasa awamu hii sikumaliza muda wa mkataba wangu na hakukuwa na hofua kama ile mara ya kwanza ambapo waliona nawahujumu, alikuwepo kocha Brants alihitaji kipa mzoefu timu ilikuwa inakwenda kwenye michuano ya kimataifa.

"Bahati mbaya Brants alifukuzwa baada ya kufungwa na Simba kwenye Mtani Jembe, akaja kocha mwingine Marcio Maximo, lakini ishu ambayo ilinifanya niondoke Yanga ni kuwa kinyume na makubaliano ya mkataba juu ya pesa ya usajili , tulikubaliana kupewa kwa awamu mbili.

"Wakati nasaini mkataba huo ambao ulikuwa wa miaka miwili wenye thamani ya Sh 40 milion nilipewa 20 milioni huku nyingine 20 milioni makubaliano yalikuwa ni kulipwa Januari 15, muda ulipita hadi kufikia Mei, nikiuliza kukawa hakuna majibu ya moja kwa moja ndipo nilipoamua nikae pembeni kwani tayari kwenye mkataba kulikuwa na kipengele hicho cha kukamilishiwa pesa yangu kwa muda huo.

"Mwanasheria wangu akasoma vipengele vya mkataba na kuona mkataba umevunjwa, wakati kesi inaendelea waliingiza ile pesa 20 milioni na kuieleza mahakama kuwa niwalipe faini ya Sh 300 milioni ingawa sasa pesa waliingiza wakati tayari mkataba umevunjwa yaani iliingizwa kinyume na makubaliano, kesi ilienda na kuisha kuwa kila mtu aendelee na maisha yake." anasema Kaseja

PESA YA YANGA YAMTOKEA PUANI

Anaeleza; "Kesi iliisha kwa hivyo ambavyo iliisha kwa vile tayari wao waliishaingiza pesa na haikurudishwa, ila kula jasho la watu sio sahihi kwani itakuhumuku kwani kuna vitu vingi vilikuja kunitokea baadaye nikahisi ni ile pesa ya watu niliyokula pasipo kuifanyia kazi.

"Ilikuwa haki kimkataba ila haikuwa haki kwa vile sikumalizia kazi yao, hivyo yaliyokuwa yananitokea niliamini ndio adhabu yake ila nilimshukuru Mungu tu na ambaye anajua ni Mungu kwani ndiye anayelipa kwa kiasi gani, sikupaswa kuumia sana kwani niliamini kuna jasho nilikula ambalo halikuwa si yangu na baadaye mambo yalikaa sawa."

TANZANIA ONE Simba ndiyo timu inayoongoza kwa kutoa makipa wanapewa jina la Tanzania One ukianza kwa Idd Pazi, Mohamed Mwameja, Kaseja na sasa Aishi Manula, Kaseja anasema sababu.

"Kwanza hakuna mtu anayejipa jina zaidi ya mashabiki tu, hiyo ilikuwa ni baada ya kufanyakazi nzuri hivyo waliona nastahili kuitwa Tanzania One, nilichogundua kipa anayecheza Simba anacheza muda mrefu ukianza na Pazi, Mwameja, mimi na Manula, ukicheza muda mrefu unapata na nafasi ya kucheza Taifa Stars, hivyo unakuwa bora zaidi."

SHIDA YA MAKIPA

Kaseja kwasasa anasema kipa wa Yanga Djigui Diarra ndiye kipa bora ukiachana na Manula ambaye kwa sasa ni majeruhi akitoa sababu zake kuwa;

"Ubora wake uko juu, na mpira wa sasa ni wa kisasa unahitaji kipa anayeweza kucheza kwa miguu na mikono, ndiyo maana inatoa picha halisi ya kuona Diarra ana uwezo mkubwa na bora kwasasa,"

Kaseja pia anawataka wachezaji hasa makipa kuacha kutumia zaidi mazoezi ya mitandaoni na kuona kazi ya ukipa ni nyepesi bali waingie uwanjani.

"Utandawazi ni mzuri ila kuna nafasi umewaharibu watu, kuna vijana wanaamini wakiingia Youtube wakiona wanavyofanya mazoezi makipa basi wanadhani nao wanaweza kufanya vile.

"Kuna wadogo zetu wanaamini ukifanya vile unaweza kuwa bora lakini ni kwamba mitandaoni hawawezi kukuwekea kila kitu, ile ni elimu hawawezi kutoa elimu bure maana nao wanalipia kwa kwenda shule kujifunza, huko wanaweka vitu vya sekunde tu ambavyo havikufundishi.

"Anaweka kidogo ili uone apate watu, rai yangu watoke kwenye mitandao waingie viwanjani, wafanye mazoezi, mazoezi ya makipa ni magumu sana na yanahitahi muda, watambue na kuheshimu hiyo nafasi kwa kuipa muda wa ziada wa kufanya mazoezi," anasema na kuongeza;

"Makipa wanakaa muda mrefu nadhani ni kwasababu ya eneo tunalocheza linakuwa dogo kulitazama lakini ni kubwa kwa kulitumia, mafunzo ya makipa ni magumu ndio maana mara nyingi wanakuwa imara muda mrefu, misukosuko ni mingi mno.

"Naweza kufanya mazoezi ya wachezaji wa ndani kwa wiki nzima tangu wanaanza hadi wanamaliza lakini mchezaji wa ndani hawezi kufanya mazoezi ya makipa hata aina moja hawawezi kumaliza. Kuna aina ya kuanguka, kuruka, kudaka na mengine.

"Nimecheza ndani sana kama kiungo, kama hujaambiwa kuwa yule ni kipa huwezi kuamini, maana ni nafasi ambayo naimudu zaidi na ninaicheza vizuri sana." anasema

UKOCHA

"Mimi nimesoma ukocha kwa ujumla, cha kwanza najifunza ukocha kutaka kujua pale ambapo makocha walikuwa wanatufundisha kuwa zoezi hili lina maana gani, na si kwamba najifunza ukocha ili kuwa kocha tu hapana, nataka kujua ndio maana nimeanza kozi hizi huku nikiwa nacheza.

"Hivyo nilikuwa najua kuwa kocha akitaka kufundisha mazoezi fulani najua kabisa, hivyo hata mapungufu yangu niliweza kuyarekebisha mapema."

"Sasa hivi nasomea Leseni A, nipo darasa moja na akina Seleman Matola, Zubeiry Katwila, Habibu Kondo, ni leseni kubwa kwa Afrika, unaweza kuwa kocha mkuu timu yoyote ya Ligi Kuu nasoma pia ukocha wa makipa.

"Lengo kubwa ni kupata uelewa kwanza ili unapozungumza mpira unazungumza vitu unavyovielewa, hata ikitokea kozi ya makocha wa viungo pia nitasoma maana nataka kuujua mpira vizuri.

"Lakini unaweza ukawa kocha ama usiwe kocha maana mimi naamini Mungu ndiye anayempangia kila fungu mwanadamu."

Chanzo: Mwanaspoti