Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karihe anastahili saluti pale Yanga

Karihe Pic Data Karihe anastahili saluti pale Yanga

Fri, 29 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mchezaji yeyote anaweza kutengeneza jina lake kutokana na mafanikio yake ambayo amekuwa akiyapata akiwa uwanjani.

Hili ni jambo la kawaida kwa wanasoka, kuna wengine wana majina makubwa, lakini wengine majina yao ni ya katikati lakini kuna sehemu wanakuwa wameshaweka heshima.

Wanasoka wengi wanapimwa kutokana na namba, yaani anafanya kitu gani akiwa uwanjani, amefunga mabao mangapi, ametoa pasi ngapi za mabao, na mambo mengine mengi ambayo yanatokea uwanjani.

Ni ngumu kumpata mchezaji mwenye kila kitu uwanjani, anajua kufunga anajua kuokoa, anajua kakaba anajua kutoa pasi za mabao, huyu ni ngumu kumpata, lakini ni rahisi kumpata mwenye jambo moja ambalo analifanya kwa umakini mkubwa na kupata mafanikio.

Tanzania kuna mshambuliaji mzaliwa wa Zanzibar anaitwa Seif Karihe, huyu ni kati ya wachezaji wakongwe kwenye soka lakini haimbwi sana ingawa namba zake zinazungumza kila sehemu ambayo amekanyaga.

Amewahi kuzitumikia timu kubwa hapa nchini ikiwamo Azam FC, Lipuli ya Iringa, Dodoma Jiji, Mbeya City, Mafunzo pamoja na Ruvu Shooting, kila sehemu akionyesha ubora wake.

Kote alipocheza amekuwa mchezaji mwenye heshima kubwa, lakini inawezekana akawa mchezaji mwenye rekodi ya kuionea Yanga zaidi kuliko timu nyingine zote ambazo amekutana nazo.

Sehemu nyingi ambazo Karihe amepita na kukutana na Yanga, amewatungua na sasa inaonekana kuwa ni kawaida yake kuitesa safu ya ulinzi ya timu hiyo kuanzia ile ya kina Kelvin Yondani hadi ya leo ya Dickson Job.

Katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopita wiki moja nyuma, Karihe alifunga bao pekee la Mtibwa ilipolala 4-1 kwenye Uwanja wa Chamazi dhidi ya Yanga na likatajwa kama kati ya mabao bora zaidi kwenye ligi hadi sasa.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 30, alifunga bao hilo katika dakika za mwisho kabisa za mchezo huo akipiga shuti la umbali mrefu, likamshinda kipa wa Yanga, Djigui Diarra na kujaa wavuni.

“Diarra ni kipa mzuri, nimemsoma, ana udhaifu wake kama kipa ndiyo maana umeona nimeweza kumfunga bila shida yoyote, hili ni jambo ambalo nimekuwa nikijifunza kila mara mazoezini,” alisema Karihe baada ya mchezo huu.

Lakini kumbuka, msimu uliopita mchezo ulioipa Yanga ubingwa ulikuwa ni kati yao na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, Diarra akiwa tena langoni kwenye mchezo muhimu.

Katika mchezo huu, Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-2, lakini pia moja kati ya mabao yaliyoonekana kuwa bora kwenye mchezo huu lilifungwa tena na Karihe katika dakika ya 67 na kama siyo ubora wa Yanga lingeweza kuwazuia kutangaza ubingwa siku hiyo.

Hii ina maana kuwa mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes ameingia miongoni mwa waliowahi kuifunga Yanga mabao mawili kwenye misimu miwili mfululizo na pia akiwa ameshamtungua kipa bora wa Yanga, Diarra mara mbili.

Jambo lingine la kufurahisha ni kwamba kwenye michezo yote miwili aliyoifunga Yanga, Wananchi walipata ushindi wa mabao manne.

Pamoja na hivyo, historia ya Karihe na Yanga inaonekana kuwa inatoka mbali, msimu wa 2017/2018, mshambuliaji huyo akiwa na Lipuli ya Iringa alizuia furaha ya mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao lililowafanya watoke sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku lile la Yanga likifungwa na Donald Ngoma.

Huu ulikuwa mchezo muhimu kwa Yanga kwenye Ligi Kuu na walitakiwa kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani, lakini mshambuliaji huyo akawatuliza maelfu ya mashabiki waliokuwa wamejaa kwenye dimba hilo.

Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola ambaye alimsajili Karihe akiwa na Lipuli, anasema: “Nimewahi kuwafundisha wachezaji wengi, unajua mimi nimefundisha timu kadhaa kwenye Ligi Kuu ukiachana na Simba ambapo nipo sasa, huko nyuma kuna wachezaji wengi nimewafundisha lakini Karihe ni mmoja kati ya wale wenye nidhamu ya hali ya juu, anapenda kusikiliza na wakati mwingine ukimtuma uwanjani anafanya kama unavyotaka.

“Kwenye hiyo sare ya bao 1-1, mimi ndiyo nilikuwa kocha wa Lipuli na siku kadhaa mbele tulikuwa na mechi nyingine dhidi ya Yanga, tulipoteza nafikiri lakini alionyesha kiwango cha juu sana licha ya kuwa hakufunga, ni kati ya wachezaji wazuri kwenye ligi yetu.”

Kama unafikiri ni mwisho, hapana, Desemba 2020 aliifungia Dodoma Jiji bao safi katika mchezo wa Ligi Kuu wakati Yanga iliposhinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mshambuliaji huyo alifunga bao lake hilo dhidi ya Yanga, baada ya aliyekuwa kipa wao, Metacha Mnata kuitema krosi ambayo ilipigwa na aliyekuwa winga wa Dodoma Jiji, Dickson Ambundo kabla hajatua Yanga.

Yanga ilifunga mabao yake kupitia Said Ntibazonkiza, Lamine Moro na Bakari Mwamnyeto. Kuonyesha kwamba ni mshambuliaji mwamba, pamoja na kwamba anaionea zaidi Yanga akiwa ameshaifunga mabao manne hadi sasa, anastahili maua yake.

Kwenye Ligi Kuu msimu huu amepachika mabao manne, huku timu yake ya Mtibwa Sugar ikiwa imefunga jumla ya mabao 14. Staa huyo anaonekana kuwa kwenye ubora mzuri ingawa timu yake ipo mkiani kwenye ligi ikiwa na pointi nane katika michezo 14 ambayo imecheza hadi sasa.

Chanzo: Mwanaspoti