Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karihe aahidi mabao Mashujaa FC

Karihe Pic Data Seif Karihe.

Mon, 29 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji mpya wa klabu ya Mashujaa FC, Seif Karihe, amesema atahakikisha anapambana kuipatia timu yake mabao mengi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano mingine ili ifanye vizuri msimu unaotaraji kuanza hivi karibuni.

Karihe, alisema amefurahi kujiunga na klabu hiyo yenye mashabiki wanaoipenda timu yao na kwa kushika nafasi ya tatu ya timu zilizoingiza watazamaji wengi msimu uliopita.

Akizungumza akiwa kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, Karihe aliyejiunga akitokea Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja, alisema anaamini bado atakuwa na uwezo uleule wa kufunga mabao na kwa sababu amekutana na wachezaji bora kwenye kikosi hicho.

"Mimi ni mshambuliaji, kazi yangu kubwa ni kufunga, na kila ninapokwenda huwa naacha alama, hata Mtibwa Sugar pamoja na kwamba imeshuka daraja lakini nilifunga mabao mengi, nimejiunga hapa na kukuta hali ya kambi ni nzuri, ushirikiano na wachezaji wenzangu uko vizuri hiyo imenifanya nizoee mazingira kwa haraka, tuseme ukweli tu kuwa hakuna ugeni kwenye mpira, wachezaji mkishakutana hata kama hamjawahi kuonana hata siku moja, haichukui hata masaa mengi, tayari wote mnakuwa kama mmezaliwa pamoja," alisema mchezaji huyo ambaye pia huichezea Zanzibar Heroes.

Alisema kitu kingine kitakachomfanya kuwa na mzuka wa kufunga ni aina ya mashabiki wa Mashujaa ambao wanaipenda mno na kuishangilia timu yao kwa mbwembwe kila inapocheza hasa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Lake Tanganyika.

"Nimeona mashabiki wana mzuka kweli na timu yao, wana moyo na timu yao, hata nilipoona Mashujaa wanashika nafasi ya tatu kwa kuingiza mashabiki wengi uwanjani nyuma ya Simba na Yanga sikushangaa ni kitu kizuri sana, hii inatuongezea moyo hata sisi wachezaji kupambana," alisema

Karihe pia amewahi kuzichezea klabu za Mafunzo FC ya Zanzibar, Ruvu Shooting, Azam FC, Lipuli, Mbeya City na Dodoma Jiji kabla ya kujiunga na Mtibwa Sugar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live