Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kariakoo dabi ni zaidi ya pointi tatu

Simba X Yanga 1 Kariakoo dabi ni zaidi ya pointi tatu

Fri, 3 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dabi ya Kariakoo, Simba na Yanga kwa sasa zinatazamwa kibiashara zaidi, tofauti na mwanzo ambapo vita yao kubwa ilikuwa ni kuwania pointi tatu muhimu na kuwapa raha mashabiki wao, huku anayefungwa anataniwa.

Katika mjadala wa juzi Jumatano kwenye Mwananchi Space, uliyokuwa unasema Simba, Yanga zitumieje dabi ya Karikoo kibiashara, ilialika wadau mbalimbali ambao walilichambua hilo.

Kati ya wadau walioalikwa ni Makamu wa Rais wa Yanga SC Arafat Haji na Ofisa wa habari wa bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Karim Boimanda, ambao walilifafanua hilo kwa upana zaidi.

Boimanda alisema dabi ya Simba na Yanga ndio inayouza zaidi, akithibitisha hilo kwamba wanapigiwa simu kutoka nchi mbalimbali na Wanahabari, wakitamani kuja kuripoti mchezo huo, jambo wanaloliona linaleta taswira nzuri kwenye soka la Tanzania.

"Kama msemaji wa bodi ya Ligi nikiri kwamba mchezo wa dabi unauza, maana tunapigiwa simu kutoka nje kama Ujerumani, England, Afrika Kusini, Congo kuja kuuripoti mchezo huo na ndio maana unakuwa na maandalizi ya kipekee;

"Pia timu hizo zinaweza zikabuni namna ya kupata pesa zaidi kwa njia ya tiketi mfano Simba ina platnam, kuna VIP A, B, wanaweza wakaongeza C na zenyewe zikawa na kiasi ambacho kitaongeza pato lao, klabu hizo zina watu makini."

Kwa upande wa Haji, makamu Rais wa Yanga, alisema mwanzoni waliwekeza nguvu zaidi kwenye ushindani zaidi tofauti na kwa sasa jinsi ilivyo.

"Tumeanza kuwa na jicho la tofauti kama kutumia mitandao yetu ya kijamii ambapo tunashindana na timu kubwa Afrika kama Al Ahly tunashika nafasi ya pili hilo si jambo dogo;

"Tunawaza kufanya makubwa zaidi na tunatambua sisi ni klabu kubwa, zinazotakiwa kuwaza zaidi kwenye upande wa kutafuta kipato cha klabu, ukitaka kujua dabi hiyo ni kubwa ndio maana unakuta hata Mwanaspoti linauza sana kwenye mechi hizo, mashabiki wanakuwa wanataka kujua wachezaji wao wanawaza nini juu ya mechi."

Nje ya kauli hizo bado Mwananchi linakuonyesha namna ambavyo nje ya dakika 90 kuna pesa zinaingia kutokana na dabi.

MAUZO YA JEZI KUONGEZEKA Siku ambazo huwa kuna mechi kubwa kama hizi kila shabiki wa Simba na Yanga huwa anapenda kuingia uwanjani akiwa amependeza na jezi ya timu yake.

Hilo ni kwamba wanataka kuonyesha ni namna gani ambavyo wanasapoti timu zao na wanataka kupendezesha uwanja siku hiyo.

Gharama ya jezi inakadiliwa kufika sh 35000 (Elfu thelathini na tano) hivyo kama wakinunua wengi ni wazi kabisa biashara itakuwa nzuri mno.

Wakati huo huo hata wale watakaokuwa wameshindwa kufika kwenye maduka makubwa watapata maeneo ya uwanjani kwa sababu huwa zinauzwa.

MITANDAO YA JAMII KUONGEZA WAFUASI Hadi sasa Simba ndio kinara wa wafuasi kwenye mtandao wa Instagram ikiwa na 5.5 milioni huku Yanga ikiwa na 2.8 milioni hadi sasa.

Licha ya idadi hiyo bado wapo wafuasi wengine ambao huwa wanatembelea mitandao hiyo bila ya kuwafuata (follow) hivyo inaongeza idadi ya watu wanaowafatilia.

Kwa namna moja ama nyingine kwenye mechi kubwa kama hii ni lazima wafuasi watakaotembelea mitandao ya timu hizi itaongezeka kwa lengo la kuangalia nini ambacho kinaendelea.

Wingi wa mashabiki unatoa fursa kwa makampuni mengi kutaka kuingia mikataba na timu hizi kama ambavyo sasahivi inavyomwagika.

MAPATO YA UWANJANI KUONGEZEKA, MGAWANYO MKUBWA Msimu uliopita mechi ya dabi, iliyopigwa Aprili 16, 2023, Shirikisho la Soka Tanzania lilitoa taarifa za mapato ya mchezo huo, uliomalizika kwa Yanga kuchapwa mabao 2-0 na Simba.

Kwa mujibu wa TFF, mchezo huo jumla ya mashabiki 53,569 waliingia Uwanjani ambapo VIP A waliingia Watazamaji 340 kwa kiingilio cha sh. 30,000 na kupatikana jumla ya sh. 10,200,000, VIP B waliingia Watazamaji 4,160 kwa kiingilio cha sh. 20,000 ikapatikana jumla ya sh. 83,200,000, hivyo uliingiza jumla ya sh. 410,645,000.

VIP C waliingia watazamaji 2,004 kwa kiingilio cha sh. 15,000 na kupatikana sh. 30,060,000 wakati jukwaa la rangi ya Machungwa waliingia watazamaji 10,372 kwa kiingilio cha sh. 10,000 ikapatikana jumla ya sh. 103,720,000 na jukwaa la mzunguko waliingia Watazamaji 36,693 kwa kiingilio cha sh. 5,000 na kupatikana jumla ya sh. 183,465,000.

Mgawanyo wa mapato VAT Sh. 62,640.762.71, BMT Sh. 10,440,127.12 Gharama za tiketi Sh. 22,585,475 Uwanja Sh. 47,246,795.28 Gharama za mchezo Sh. 22,048,504.46 TFF Sh. 12,599,145.41 TPLB Sh. 25,198,290.81 FA Mkoa Sh. 18,898,718.11 Timu mwenyeji (Simba SC) Sh. 188,987,181.10

POSHO KUBWA KWA MASTAA Ni mchezo unaobeba neema kwa mastaa wa klabu hizo, kwanza zinawapa heshima ya kuonekana kwa ukubwa ndani na nje, ukiachana na hilo pia ni mechi inayoweza kuwang'oa wanaocheza chini ya kiwango.

Mchezo huo unakuwa na posho kubwa kwa wachezaji, ingawa inakuwa ni ngumu sana kuweka wazi, kama alivyowahi kusema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba SC Salim Abdallah 'Try Again'.

"Dabi ina msisimko mkubwa kwa mashabiki, ndio maana inakuwa na posho ya aina yake, lakini inakuwa ngumu kuitaja kutokana na kuwaepushia wachezaji usumbufu, mfano mwingine anakuwa anadaiwa basi ataanza kupigiwa simu."

Upande wa Yanga vile vile huwa wanaweka dau tofauti tofauti ili kuongeza morali kwa wachezaji wao.

MAMA NTILIE, BAR NI FURSA YA KIPEKEE Siku ya dabi nje ya uwanja vyakula huwa vinauzwa tofauti na siku zingine. Mama ntilie huwa wapo maeneo yote ya uwanja kuhakikisha wanauza chakula.

Vyakula ambavyo vinauzwa katika eneo hilo ni rafiki kwa bei zao kwa mashabiki kwani huwa zinauzwa sio juu ya sh 2500 sawa na bei za mtaani.

Mama ntilie maarufu katika uwanja wa Mkapa, Mama Mwajuma alisema katika dabi huwa anaongeza kiwango cha upikaji wake kwa sababu anajua ni siku anayouza zaidi.

"Siku hii huwa tunauza sana kwahiyo mimi kama nilikuwa nauza kilo tano kwa siku lakini katika mechi hizi inafika hadi kilo 10 au 12 na zinaisha zote,"alisema Mama Mwajuma.

Wakati huo huo licha ya watu wengine kuuza chakula bado huwa kuna biashara ya vinywaji ambapo bar zile za nje ya uwanja huwa zinajaza kabla na baada ya mchezo.

Mashabiki huwa wanakaa nje kwenye bar hizo kabla ya kwenda uwanjani wanapata vinywaji baridi na hata wakitoka basi huwa wanakuwa wanakaa hapo kuendelea kufurahia matokeo na wengine kujipoza na matokeo.

WENYE MAGARI YA BIASHARA,BAJAJI NA BODABODA KICHEKO Kwa hapa Dar es Salaam hakuna kingine kitakachokuwa kinaendelea siku hiyo zaidi ya watu wengi kwenda uwanjani kuangalia mchezo huo.

Wapo ambao watabaki nyumbani, bar na sehemu zingine kuangalia mechi laklini magari mengi, bodaboda na bajaji siku hiyo njia ni moja tu kwenda uwanjani kwenye dabi.

WACHUMI WATIA NENO Mchumi kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Abel Kinyondo alisema upande wa uchumi anatamani kuona mechi zote ziwe zinajaza kama ilivyo kwa Simba na Yanga zinavyokutana ila inakuwa ni tofauti.

Kinyondo alisema uchumi hauwezi kukua kwa siku moja tu ila kama mechi zote zikijaza basi ni rahisi kukua kwa sababu kutakuwa na usawa tofauti na sasa.

"Katika mechi 30 inajaza mechi moja tu ya dakika 90 halafu mechi zingine hazijazi, hii sio kitu kizuri hata kama watu wanafanya biashara katika siku hiyo ila inabidi ibadilike kwenye kukuza uchumi;

"Viongozi wa timu zingine wangejifunza kwanini hizi timu zinajaza, shida kwamba nao ni Simba na Yanga, pia wapo wana siasa ambao ni mashabiki wa wazi wa timu hizi hivyo siasa nayo imeingia katikati,"alisema Kinyondo.

Wakati huo huo upande wa mchumi, Oscar Mkude alisema mpira wa miguu nje ya burudani kwa sasa ni biashara na ndio maana uwekezaji mkubwa.

Mkude alisema mpira ni uchumi na mchezo wa watani wa jadi uchukuliwe kwa ukubwa zaidi kwa sababu ushindani wao umekuwa endelevu.

"Ukiangalia Kenya na hata Uganda mechi za watani wa jadi haziwi kwa ukubwa kama ambavyo ipo hapa uwanja kujaa na hata ile hali ya kuendelea kushinda imepungua;

"Mechi hizi pia nje ya yote yanatoa fursa zingine kwa vijana kuutumia kuwekeana ahadi mbalimbali na wanapata pesa."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: