Zikiwa zimesalia siku mbili kufanyika kwa Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga katika Uwanja wa Mkapa ulinzi umeanza kuimarishwa uwanjani hapo.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Afisa habari wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda amesema tayari wamezungumza na watu wa ulinzi na usalama kwa ajili ya kuweka usalama kwenye mchezo huo ambao huudhuriwa na mashabiki wengi ndani na nje ya nchi.
"Hadi sasa tumezungumza na watu wa ulinzi juu ya kudhibiti matukio mbalimbali kwenye mchezo huo mkubwa Afrika Mashariki na kati," amesema Boimanda.
Kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani amesema "Kutakuwa na mialiko ya watu maalumu ambao watapewa kadi kwa mtu husika na watoto nao wataingia kwa kutumia kadi."
Yanga itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa unaoingiza mashabiki 60,000 na kutokana na wingi wa mashabiki, ulinzi huimarishwa ili kuepuka vurugu na mambo mengine ya kiusalama.