Rais wa Shirikisho la Kandanda Tanzania TFF, Wallace Karia amesema maneno ambayo yanaendelea katika mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari juu ya Udhamini wa GSM hayana afya na soka la Tanzania na yanashusha ari ya kuendelea kuwatafuta wadhamini wengine.
Ikiwa ni wiki moja pekee nyuma GSM ilisaini mkataba wa miaka miwili na TFF wenye thamani ya Sh 2.1 Bilioni wakiwa kama mdhamini mwenza kwenye Ligi Kuu Bara ambayo mdhamini mkuu ni NBC.
Amesema hayo wakati akijibu hoja za Waandishi wa Habari baada ya kutaka kujua kuhusu Udhamini wa GSM na mwingiliano kimasilahi kwenye ligi.
“Udhamini wao ni mzuri na sio wamiliki wa timu za Namungo, Coastal wala Yanga, kama ni hivyo basi Yanga wasingeifunga Coastal msimu uliopita lakini waliifunga,” alisema Karia na kuongeza;
“Nafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya klabu za Tanzania ili zipate udhamini, tunatafuta udhamini wa mabasi katika kampuni mbalimbali ili tu timu zipate usafiri.”
Naye Mkurugenzi wa uwekezaji GSM, Injinia Hersi Said alisema: “Sisi ni watu imara na hatuwezi kuyumbishwa na watu wengine, naahidi tupo katika hatua za mwisho kwenye kukamilisha mchakato huu.”
Hofu kubwa ya wadau wa soka nchini ni kuwa kunaweza kukawa na mwingiliano wa masilai baina ya mdhamini GSM na kujihusisha kwake kiutendaji katika klabu moja wapo nchini ambayo inashiriki Ligi Kuu, klabu ya Yanga.