Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karia: Nitagombea tena TFF

Wallace Kariaaaaa.jpeg Karia: Nitagombea tena TFF

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: Mwananchi

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kuwa atawania tena Urais wa Shirikisho hilo kwa awamu mbili zijazo akimaanisha kuwa anaweza kuhudumu katika nafasi hiyo kwa miaka nane zaidi baada ya awamu ya sasa kumalizika.

Karia aliyasema hayo jana wakati alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), yaliyopo Tabata Relini, Dar es Salaam jana.

"Wakati ule tunaingia hakukuwa na ukomo.Tukasema tunavyoingia tuweke ukomo wa uongozi, unajua katiba yetu ya nchi haimzuii Mbunge kugombea ni hadi achoke mwenyewe, watu wamchoke au Mungu amchukue.

"Sisi tukaweka ukomo na bahati nzuri wakati sisi tunaweka ukomo na wakubwa Fifa na CAF nao wakaweka ukomo baaada ya kuona Blatter (Sepp), aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na Hayatou (Issah) walikaa muda mrefu. Kuna wakati ilifika kiongozi kutokana na umri mpaka kwenye mechi anasinzia.

"Sikujali upya wangu, lakini niliona kuna haja ya kuibadilisha katiba tuliyoikuta ya TFF, kawaida katiba zetu huenda miaka minne minne na sisi tukasema tuweke vipindi vitatu vya uongozi kama ambavyo Fifa na CAF walifanya kwa hiyo hili lilikuwa la kwanza kulifanyia kazi hasa kupitia kile kipengele cha utawala bora.

"Mimi ni kiongozi, mwaka jana nimetimiza miaka 60 kwa hiyo kwa maana umri wa kustaafu kiserikali nimeshafikisha, sasa kutokana na katiba mpya ambayo tuliibadilisha hiki ni kipindi changu cha kwanza kati ya vitatu, nazungumza hivi kisheria hata Infantino (Gianni, Rais wa Fifa) hiki ni kipindi chake cha pili.

"Mungu akinipa uhai nitakapomaliza vipindi vyangu vitatu sitaendelea tena nitamuachia mtu mwingine," anasema Karia.

Karia anasema kuwa kinachompa hamu ya kuendelea kuongoza shirikisho hilo ni kukamilisha yale ambayo ameyaanzisha ili kutengeneza mazingira mazuri kwa yule atakayemuachia kijiti.

"Wakati naingia nilikuwa na vipaumbele ambavyo niliviita 'first eleven' (11 ya Karia) ambavyo ni utawala bora, usimamizi wa fedha, maendeleo ya ligi, soka la wanawake na ufukweni, mafunzo na ujenzi wa uwezo, miundombinu na vifaa, udhamini na masoko, soka la vijana, ushirikiano wa wadau, uimarishaji mifumo ya kumbukumbu na ufanisi wa waamuzi.

"Yale ambayo tumepanga, tumeyagusa yote. Mengine yalikuwa kwenye malengo ya muda mfupi na mengine ya muda mrefu. Kiujumla tuliyopanga kufanya hadi sasa tumeyatimiza kama asilimia 70 hivi na yale ya muda mrefu tunajitahidi tuweze kuyamalizia tukipata nafasi," alisema Karia.

Chanzo: Mwananchi