Wakati Ligi Kuu Bara ikifikia tamati leo na kusubiriwa kufahamika timu zitakazomaliza kwenye nafasi ya 13 na 14 ili kucheza play-off huku upepo ukiziangukia KMC na Mbeya City, mabingwa Yanga wamejiandaa kufanya pati la maana jijini Mbeya watakapokabidhiwa taji lao leo.
Yanga imetetea taji mapema ikiwa na mechi mbili mkononi na jioni ya leo itakabidhiwa Kombe Jipya kabisa lililotambulishwa juzi jijini Dar es Salaam kabla ya kujumuisha na mashabiki wao mkoani hupo na kuanza safari ya kupeleka shangwe jijini Dar kuanzia saa 3 asubuhi ya kesho.
Yanga itakabidhiwa taji mara baada ya pambano lao dhidi ya Tanzania Prisons litakalopigwa kuanzia saa 9:30 alasiri kwenye Uwanja wa Sokoine, likiwa ni taji la 29 kwao tangu kuanza kwa Ligi ya Bara mwaka 1965 na sherehe za kulitembeza kombe zitafanyika kuanzia Uwanja wa Ndege mara timu itakaporejea kutoka Mbeya kwa kutumia basi la wazi lililopo njiani kwa sasa kutoka Uganda.
Achana na pati hilo la Yanga la kusherehekea ubingwa huo kwa kutumia basi maalumu kama ilivyokuwa msimu uliopita walipokabidhiwa pia taji jijini Mbeya baada ya kuvaana na Mbeya City na kutoka nao sare ya 1-1, pazia la ligi linamalizwa leo kwa timu 16 kutupa karata ya mwisho ya msimu.
Kwa siku 298 sawa na miezi zaidi ya 11 tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu, Agosti 15, ligi hiyo itafikia tamati huku tayari bingwa na washindi wa nne kwenye msimamo sambamba na timu mbili za kushuka daraja zikiwa zimefahamika mapema.
Yanga imetwaa ubingwa ikifuatiwa na Simba, kisha Azam na Singida Big Stars inayoshiriki msimu wa kwanza zikimaliza kwenye Nne Bora na kukata tiketi ya michuano ya CAF kwa msimu ujao, huku Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zikishuka rasmi daraja kwenda Ligi ya Championship.
Yanga inashuka uwanjani kuvaana na Prisons ikiwa tayari ina taji baada ya kukusanya pointi 75, ikifuatiwa na Simba yenye piointi 70 itakayomalizana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, huku Azam ikiwa na kazi ya kuisindikiza salama Polisi Tanzania baada ya kushuka daraja.
VITA IPO HAPA
Ukiacha mechi za kukamilisha ratiba kwa vigogo Simba, Yanga na Azam, utamu wa ligi umehamia eneo la kati na kule mkiani ambapo timu zinapambana kumaliza pazuri ili ziwepo msimu ujao, lakini pia kuzikomba mamilioni ya fedha zinazotolewa na wadhamini wa matangazo ya TV, Azam Media.
Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa mwaka juzi baina ya TFF na Azam Media bonasi kwa mabingwa ni Sh 500 Milioni, huku itkayomaliza nafasi ya pili itakomba Sh250 Milioni na wa tatu italamba Sh225 Milioni wakati ile ya nne itavuna Sh200 Milioni.
Timu itakayomaliza nafasi ya tano itazoa Sh65 Milioni, wakati ya sita itabeba Sh60 Milioni, huku ya saba itapewa Sh55 Milioni na timu itakayomaliza ya nane itaambulia Sh 50 Milioni na kwa sasa .Namungo ipo nafasi ya tano na pointi 39, huku Geita ikiwa ni ya sita na alama 37, Prisons ya saba na alama 37, Ihefu ya nane na pointi 36, Kagera Sugar ya tisa na pointi 35 na Dodoma Jiji nafasi ya 10 na alama 34.
Timu hizo zote tayari zimejihakikishia kubaki Ligi Kuu msimu ujao bila kujali matokeo ya leo, hata hivyo kazi ipoa kwa timu nne za Coastal Union iliyo nafasi ya 11 na pointi 33, Mtibwa Sugar ya 12 na pointi 32, Mbeya City ya 13 na alama 31 na KMC ya 14 na pointi 29. Hizi zinapambana kukwepa kucheza mechi za mtoano 'Play off kuchujana kabla ya kwenda kukutana na Mashujaa.
Mtanange wa nguvu zaidi kwa funga dimba la leo ni utakaozikutanisha Mbeya City na KMC kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga kwani atakayepigwa moja kwa moja ataangukia kwenye kucheza Play off.
Kama mechi hiyo itamalizika kwa sare basi KMC itakucheza Play off, lakini wakati kipute hicho kikiendelea kila timu itakuwa inaziombea Coastal na Mtibwa zipoteze mechi zao kwani zikishinda, City na KMC Play off itazihusu moja kwa moja bila kujali matokeo yao.
Mtibwa itakuwa Manungu, Turiani kumenyana na Geita Gold iliyo salama, huku wenyeji wakihitaji ushindi ili kubaki ligi kwa msimu ujao kwani itafikisha alama 35 ambazo si City wala KMC itaweza kuzifikia bila kujali matokeo yao, pia kama Mtibwa itapata sare italazimika kuziombea KMC na City zitoke sare na hapo ndipo itajikwamua kutocheza mtoano.
Kwa upande wa pia itakuwa uwanja wa Uhuru ikipepetana na Simba, Ushindi pekee ndio utakaowapa Wagosi wa Kaya uhakika wa kusalia Ligi Kuu lakini matokeo mengine yataifanya kulazimika kuziombea dua mbaya Mtibwa, Mbeya City, na KMC.
WASIKIE HAWA
Baadhi ya makocha wa timu hizo akiwamo Hans Pluijm wa Singida, kila mmoja amesema kiu yao ni kumaliza msimu kwa heshima, ingawa wamekiri ulikuwa mchakamchaka wa aina yake hadi kufikia hapo walipo.
Pluijm, ambaye timu yake itavaana na Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi, kiu yake ni kuona wanamaliza ya tatu kwa kuipiku Azam iliyopo juu yake kwa sasa kwa tofauti na pointi mbili. Azam ina pointi 56 kwa sasa na Singida 54 na matokeo ya ushindi kwa Wauza Alizeti na Azam ikipoteza inaweza kuwapandisha hadi nafasi ya tatu.
“Katika siku nne tumekuwa na safari ndefu kuja Lindi, lakini tumejipanga kupata matokeo mazuri ili kumaliza katika nafasi ya tatu.Najua Namungo ni timu nzuri tunaamini itakuwa mechi nzuri,lazima tupambane kwa kila hali ili tushinde na nawaamini vijana wangu,” alisema Plujm, huku nahodha msaidizi wa timu hiyo, Amissi Tambwe alisema anaamini utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Namungo.
“Sisi upande wetu tumejiandaa vizuri ila ilikuwa safari ndefu sana kutoka Singida mpaka Ruangwa tumekuja kutafuta pointi tatu tangu mwanzo wa ligi ilikuwa kushiriki mashindano ya Kimataifa na sasa tunaitafuta nafasi ya tatu,”alisema mshambuliaji huyo ambaye amewahi kuichezea Yanga.
Kocha wa Mbeya City, Abdalah Mubiru alisema hawataki kuangalia kilichotokea katika mchezo uliopita kwani mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwao baada ya awali kuchemsha mwishoni dhidi ya Yanga kwa kuongoza mabao 3-0 na yote kurudishwa na mechi kuisha kwa sare ya 3-3.
"Kila mmoja wetu anahitaji ushindi katika mchezo wa dhidi ya KMC ndio maana tumehamasishana na kupeana nguvu kwaajili ya kujitoa kwa nguvu ili kupata alama tatu," alisema Mubiru.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema ishu ya historia na rekodi havina nafasi kwake na hawawezi kucheza kwa kuangalia hilo, bali hitaji lao ni kushinda mechi hiyo.
“Ni mechi ya mwisho ambayo kila mmoja anataka heshima, hatujapoteza mechi katika michezo minne tuliyocheza hivyo lazima tuhitimishe kwa kuwapa raha mashabiki wetu,” alitamba Baresi, huku kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze alisema baada ya sare waliyopata mchezo uliopita leo watakuwa tofauti kutokana na mastaa wao kupata muda wa kupumzika na kufanya mazoezi.
Yanga inatarajiwa kushusha mziki kamili baada ya Mayele pamoja na kina Yannick Bangala, Kennedy Musonda sambamba na kocha Mkuu, Nasreddine Nabi kuifuata timu baada ya kukosekana kwenye mechi iliyopi dhidi ya Mbeya City.
Ratiba ilivyo
Azam v Polisi TZ (Azam Complex)
Ihefu v Kagera (Highland Estate)
Mbeya City v KMC (Nelson Mandela)
Mtibwa Sugar v Geita Gold (Manungu)
Namungo v Singida BS (Majaliwa)
Ruvu Shooting v Dodoma Jiji (Jamhuri)
Simba v Coastal Union (Uhuru)
TZ Prisons v Yanga (Sokoine)