Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Karata ya kwanza Afrika ni leo

Senegal Karata.jpeg Senegal watakua na kibarua kizito mbele ya England

Sun, 4 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Itakuwa pale Al Bayt Stadium maeneo ya Al Khor, kilomita 44 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Doha saa 4:00 usiku, wakati mwamuzi wa kati kutoka El Salvador, Ivan Barton atakapojaza hewa kwenye mapafu yake na kuruhusu ipite hadi kwenye filimbi itakayosikika katika masikio ya wachezaji ghali kutoka Afrika na England walioshuhudia Malkia Elizabeth II, akizikwa siku chache zilizopita.

Muda huo joto litakuwa likisoma kati ya nyuzi 35 hadi 40, huku mashabiki wasiopungua 35,000 wakiwa uwanjani kushuhudia mechi ya kihistoria ya hatua ya 16 bora ya michuano hii kati ya England na Senegal.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana katika historia ya soka na England ilifuzu hatua hii baada ya kumaliza kundi ikiwa kinara kwa alama saba wakati Senegal ilimaliza ikiwa na alama sita.

Senegal itakuwa ndio timu ya kwanza kutoka Afrika kutupa karaka yake katika hatua hii na inahitaji kushinda ili kufikia rekodi yao ya kucheza robo fainali kwenye mashindano ya mwaka 2002 ambapo iliitoa Sweden kwenye 16 bora kabla na kuambulia kichapo cha bao 1-0 kwenye hatua ya robo fainali dhidi ya Uturuki.

England ambayo michuano ya mwaka 2018 kule nchini Urusi iliishia hatua nusu fainali, imekuwa ikipambana sana kuhakikisha inaifikia rekodi yake ya mwaka 1966 ambapo ilishinda taji hili baada ya 2014 kuishia hatua ya 16 bora.

Senegal italazimika kucheza bila ya staa wao Idriss Gana Gueye ambaye amepata kadi tatu za njano kwenye mechi tatu za hatua ya makundi, England itamkosa Ben White aliyerudi England kutokana na sababu binafsi.

Sadio Mane ambaye alitajwa kwamba huenda angekuwepo kwenye hatua hii, naye hatokuwepo kwenye kikosi cha Senegal kwani bado hali yake sio nzuri.

Kikosi cha England kinachoweza kuanza Jordan Pickford, Trippier, Stones, Maguire, Shaw; Rice, Bellingham, Henderson; Rashford, Kane, Sterling.

Kikosi cha Senegal kinachoweza kuanza ni Eduardo Mendy, Sabaly, Koulibaly, Diallo, Jakobs; Ciss, P. Gueye; P. Sarr, Ndiaye, I. Sarr; Dia.

Mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora kwa siku ya leo itakuwa kati ya Ufaransa na Poland ambapo mvuto zaidi unaonekana kwa Roberto Lewandowski na Kylian Mbappe.

Mastaa hao ambao ni miongoni mwa mastraika bora barani Ulaya ndio wanaonekana kunogesha na kuvutia mashabiki wengi kutamani kuitazama mechi hiyo itakayopigwa katika dimba la Al Thumama chini ya mwamuzi Jesus Valenzuela kutoka Venezuela.

Ufaransa ndio bingwa mtetezi wa michuano hii na inataka kuepukana na rekodi mbaya ya mabingwa watetezi ambao asilimia 90 huwa wanaishia hatua ya makundi ama 16 bora.

Ufaransa ni miongoni mwa timu zilizofanikiwa kufuzu mapema kwenye hatua ya 16 bora ya mashindano haya baada ya kushinda mechi zote mbili za mwanzo za makundi, tofauti na ilivyokuwa kwa Poland ambayo ilifuzu kwenye mechi ya mwisho baada ya Saud Arabia kupoteza.

Chanzo: Mwanaspoti