Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anafahamu wazi kwamba kikosi chake ni lazima kifunge mabao ya kutosha kwa sababu ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu unaweza kuamriwa kwa tofauti ya mabao.
Licha ya kwamba inaingia wikiendi hii ikiwa nyuma kwa pointi mbili na nafasi ya tatu kwenye msimamo, Arsenal kwa sasa imekuwa na wastani mzuri wa tofauti ya mabao kwenye Ligi Kuu England.
Kikosi hicho cha kocha Arteta kimeshinda 6-0, 5-0 na 4-1 katika mechi zao tano za mwisho ilizocheza kwenye Ligi Kuu England na hivyo kuwa na jumla ya mabao 25-3 tangu mwaka huu ulipoanza.
Jambo hilo la tofauti ya mabao linawafanya kuwa juu ya wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa Liverpool na Manchester City, huku akiamini vita hiyo ya miamba watatu inaweza kuwa kali hadi mwisho na mshindi huenda akapatikana kwa kutazama kila kitu.
“Ndiyo, hakika,” alijibu Arteta alipoulizwa kama kufunga sana mabao kutakuwa na faida mwisho wa msimu.
“Kwanza unahitaji kushinda mechi, kisha unapaswa kuwa na njaa unapokuwa mbele ya goli la mpinzani. Hiki kinachofanyika kwa siku za karibuni ni kitu kizuri sana.”
Arteta anaamini kikosi chake kitaendeleza njaa ya kufunga mabao wakati kitakaposhuka uwanjani kuwakabili Sheffield United katika mchezo wa Ligi Kuu England utakaofanyika usiku wa Jumatatu (Machi 04).
“Kila timu tunaitazama kwenye uimara na udhaifu wake, na hapo tutaangalia tuchezeje mechi yetu.” alisema Arteta wakati akijiandaa kuikabili Sheffield United inayonolewa na Chris Wilder.
Arsenal itakuwa na mzuka wa kuwakaribisha kwenye kikosi Thomas Partey na Oleksandr Zinchenko, ambao walikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.