Kwa namna ambavyo Daktari wa Simba, Edwin Kagabo ametoa ripoti ya majeraha ya beki wa kulia wa timu hiyo, Shomari Kapombe, bila shaka kuna uwezekano mkubwa akacheza mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga, Aprili 16, mwaka huu.
Kapombe hakumaliza mchezo wa kutamatisha hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wikiendi iliyopita na kulazimika kutoka nje kipindi cha pili wakati wakifungwa mabao 3-1 dhidi ya Raja Casablanca, ugenini. Nafasi yake aliingia Israel Mwenda.
Kagabo amesema baada ya kuwasili Tanzania wakitokea Morocco, Kapombe atafanyiwa vipimo siku hizi mbili ili kubaini athari ya jeraha lake na kuona kama anaweza akarudi haraka au kwa kuchelewa, huku akibainisha kwamba beki huyo anaonekana hajaumia sana, hivyo anaweza kurudi uwanjani hivi karibuni.
“Kwa uchunguzi wa awali haionekani kama ni jeraha kubwa, anaweza kupewa matibabu ya kawaida na kurudi tena uwanjani. Tutamfanyia vipimo vya kina ili kubaini ni kwa wakati gani itabidi apumzike,” alisema Kabago.