Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kapombe; Nyakati zinakuja, zinapotea

Kapombe: Tunataka Kushinda Magoli Mengi Kesho Shomari Kapombe

Sun, 7 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kikosi cha Taifa Stars kipo Misri kikijiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika zinazofanyika Ivory Coast kuanzia wiki ijayo na jioni ya leo itashuka uwanjani kuvaana na Misri katika pambano la kirafiki la kimataifa. Hiyo ni mechi yakutesti mitambo kabla ya kesho Jumatatu kuanza safari ya kwenda Ivory Coast kwenye vita ya Afcon 2013 ikipangwa Kundi F na Morocco, Zambia na DR Congo.

Hata hivyo, wakati kikosi cha wachezaji 31 kikielekea kwenye kambi, beki bora zaidi wa kulia kuwahi kutokea nchini, Shomari Kapombe yupo pale Zanzibar na Simba akishiriki Kombe la Mapinduzi. Inafikirisha sana.

Kapombe ni miongoni mwa mabeki wa kisasa ambao tumejaaliwa kuwaona katika nyakati hizi. Beki anakaba, anashambulia, ana utulivu. Anaweza kucheza nafasi nyingi Uwanjani. Ni mchezaji kamili.

Nini kimetokea kwa Kapombe? Ni kawaida kwenye soka. Nyakati zinakuja na nyakati zinapita.

Kama nchi kuna wakati tulimpigia Kapombe magoti kumuomba acheze Timu ya Taifa. Alisusa wakati fulani na kutangaza kustaafu. Alilalamika kuwa kila akiitwa timu ya taifa alikuwa anaumia. Kulikuwa na imani za mambo mengi kuhusika. Kapombe akasusa.

Baada ya vilio vingi kutoka kila maeneo ya nchi, Kapombe alikubali kurejea katika kikosi cha Taifa Stars. Kwanini watu walimuomba? Ni kwa sababu katika nafasi yake hakukuwa na mchezaji bora kumzidi. Ungewezaje kuwa beki wa kulia halafu ucheze kwa ubora kuliko Kapombe? Hakuna.

Mabeki wote wa kulia waliosajiliwa Simba ama Yanga walipimwa ubora wao na Kapombe. Alikuwa ni kipimo halisi. Hata hivyo, nyakati zimebadilika sasa. Kuna sababu nyingi za Kapombe kuachwa.

Kwanza, Kapombe huyu sio yule. Umri umekwenda na ameanza kuchoka. Siku hizi hakabi vizuri tena kama zamani. Akipanda kushambulia anachelewa kurudi. Analaumiwa hadi pale Simba kwa kushindwa kufanya majukumu yake vyema.

Yawezekana bado miaka yake sio mingi sana, lakini ukweli ni kwamba alianza kucheza akiwa na umri mdogo. Amecheza mfululizo kwa miaka mingi. Amepata majeraha mengi sana katika maisha yake ya soka. Ni lazima achoke.

Hii ndiyo sababu timu ya taifa ikaanza kutafuta mbadala wake mapema. Kocha wa sasa wa Taifa Stars, Adel Amrouche anaona ni bora akamtumia Dickson Job au Novatus Dismas katika nafasi hiyo kuliko Kapombe aliyechoka.

Ndiyo soka lilivyo. Kuna nyakati utakuwa tegemeo, halafu kuna nyakati zitakuja hutakuwa na nafasi tena. Ndiyo kama ilivyo kwa Kapombe. Ndiyo kama ilivyo kwa John Bocco.

Nani angewaza kuwa leo Taifa Stars ingekuwa inakwenda Afcon halafu kina Bocco na Kapombe wapo Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi? Hakuna, ila nyakati ndiyo zimeamua. Nyakati zao zinaelekea ukingoni.

Tunakubali walicheza kwa ubora wa juu katika nyakati zao, ila ndiyo mwisho umekaribia. Imeanza hivyo katika timu ya taifa kisha itakuja pale Simba. Leo kila mtu anasema Simba inatakiwa kuwa na mbadala wa Kapombe na Mohamed Hussein. Kwanini? Kwa sababu inapaswa kujiandaa na maisha mapya.

Baada ya muda utaona Kapombe akianza kuwekwa benchi pale Simba kisha baadaye wataachana naye. Ndiyo nyakati zilivyo. Hakuna maisha ya kudumu kwenye soka. Unafurahia wakati wako, kisha watakuja wengine kukupokea kikombe.

Ni kama ilivyo kwa Bocco sasa. Hana nafasi tena katika kikosi cha kwanza cha Simba. Ukimtazama amechoka. Hana kasi tena. Hana uchu wa mabao tena. Simba inahitaji kuwa na straika wa namna hii? Hapana. Inahitaji straika aliyechangamka zaidi.

Ni kweli Bocco ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa Ligi Kuu Bara. Amekuwa mfungaji bora mara kadhaa. Amekuwa mchezaji bora. Lakini ubaya ni kwamba soka halitazami historia, linatazama unachofanya leo.

Hii ndiyo sababu tunawashauri wachezaji kujiwekeza mapema. Maisha ya soka ni mafupi mno. Fikiria unamaliza ajira yako ukiwa hata hujafikisha miaka 40. Unarudi mtaani. Huna ajira. Hukuwahi kufanya kazi nyingine tofauti na soka. Utaishije? Ni ngumu sana.

Nyakati ndiyo zimeamua leo Meddie Kagere awe Singida Fountain Gate. Katika ubora wake nani hakumuogopa Kagere. Alikuwa straika tishio. Katika misimu yake miwili tu ya mwanzo kwenye Ligi yetu alifunga mabao 45. Huyu ndiye Kagere.

Alikuwa tegemeo kwa Simba katika mechi za ndani na kimataifa. Nini kimetokea. Kagere alianza kuchoka. Umri umekwenda. Hakuweza kwenda na kasi ya Simba tena na wakaamua kuachana naye. Ndiyo sababu hata leo hii huko Singida bado hajawa na maajabu sana.

Amekuwa ni chaguo la pili katika kikosi cha Singida. Nani angewaza kuwa ingefika wakati Kagere angekaa benchi kwenye timu kama Singida? Hakuna. Ni nyakati zimeamua.

Ni kama ilivyokuwa kwa Paschal Wawa. Alikuwa beki katili kweli kweli. Kuna wakati Azam FC walitoa fedha ndefu kumsajili. El Merrikh ya Sudan ikatoa fedha ndefu kumsajili. Simba ikawa inamlipa mshahara mkubwa. Kwanini? Alikuwa bora kuliko mabeki wengi nchini. Nini kimetokea? Amekwenda Singida na kushindwa kufanya vizuri. Mwisho wa msimu wakaamua kuachana naye. Ndiyo kama ambavyo moshi mweupe unafuka kwa Joash Onyango. Huenda naye akaachwa tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live