Mbali ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kusema hakuna vikwazo kwa Simba kutumia Uwanja Mpya wa New Amaan Complex kwa mechi za Ligi Kuu Bara, kanuni za Bodi ya Ligi (TPLB) zinapinga suala hilo.
Awali, Simba ilikuwa inatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam ambao unaendelea na ukarabati unaotarajiwa kukamilika Agosti, mwaka huu na kwa sasa umefungwa kabisa kwa shughuli zote.
Ingawa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na Simba kuhusiana na mpango wa kuhamishia mechi kwenye Uwanja wa Amaan, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmad Vuai amethibitisha kupokea barua kutoka kwa wababe hao wa Mtaa wa Msimbazi wakiomba kuchezea mechi za ndani na zile za kimataifa kwenye uwanja huo.
Hata hivyo, kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na TPLB zinaonekana kuweka kikwazo kwa Simba kuhamia Zanzibar kucheza mechi za ligi.
Kifungu cha 9(4) cha kanuni hizo kinasema: “Iwapo timu yoyote haina uwanja wa nyumbani unaofaa kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaweza kuchagua uwanja mwingine katika jiji au mkoa wa jirani ndani ya Tanzania Bara wenye sifa zinazokubalika na lazima uthibitishwe au kupitishwa na TFF.”
Kutokana na kanuni hiyo, ni wazi kwamba Simba itakuwa na wakati mgumu wa kuutumia Uwanja wa New Amaan au mwingine wowote ambao uko nje ya Tanzania Bara.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo amekaririwa akisema watazungumza na Simba, na baadaye kutoa uamuzi wa mwisho.
“Kanuni za ligi ni kwa manufaa ya klabu na si vinginevyo, na ndiyo maana huwa tunakutana nazo (klabu) kabla ya ligi kuanza na kuzijadili. Tumepokea barua ya Simba, tutalijadili na kutoa uamuazi kwa mujibu wa kanuni,” amekaririwa Kasongo.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa ZFF, Vuai amesema kimsingi hawana tatizo na Simba kutumia Uwanja wa New Amaan Complex ilimradi wafuate taratibu.
“Tumepokea barua kutoka kwa Simba wakiomba kutumia uwanja mpya wa Amaan Sports Complex kwa mechi zao za ligi. Hatuwezi kuwakataza, kwani uwanja huo ni huru kutumiwa na klabu za Tanzania ambazo zitakuwa tayari kufuata taratibu zetu,” amesema Vuai.
"Kuhama kwa Simba hakutaathiri mechi zetu za ligi (Zanzibar) kwa sababu tuna viwanja vingine kama Mao Tse Tung na vingine karibu na Amaan Sports Complex. Tukiwa chombo kinachosimamia soka tutapanga namna mechi za Simba na ligi ya Zanzibar zitakavyoendeshwa bila kuingiliwa.”