Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kanuni yagoma Singida kupeleka sita Ihefu

Wachezaji Singida FG.jpeg Kanuni yagoma Singida kupeleka sita Ihefu

Mon, 15 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku mbili baada ya kutoka kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Singida Fountain Gate mambo yamebadilika kabisa. Ikiwa kwenye michuano ya Mapinduzi, timu hiyo ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri hasa baada ya msimu uliopita kufika fainali, lakini baada ya kuondolewa katika nusu fainali msimu huu, mambo yakawa tofauti huku kila mchezaji akisema lake na kuelekea njia yake.

Taarifa ya kwanza ambayo ilionekana kuwashtua wengi ni ile ambayo ilikuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa timu hiyo imemuacha mshambuliaji wake Meddie Kagere visiwani Zanzibar baada ya kukosa penalti kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Simba.

Lakini kabla hilo halijapoa, ilionekana taarifa kuwa kuna wachezaji watano wa timu hiyo hawajalipwa mishahara ya miezi miwili na wameomba kuondoka kwenye timu hiyo, mmoja akitajwa kuwa ni Aziz Andambwile.

Na kali kuliko zote ni taarifa inayoonyesha kuwa mmoja kati ya wamiliki wa Singida  Fountain Gate ameinunua Ihefu na sasa anafanya kazi ya kuijenga upya.

Hadi sasa tayari wachezaji sita wa kikosi cha kwanza cha Singida wameshaachana na timu hiyo na kujiunga na Ihefu, mastaa hao ni Bruno Gomes, Marouf Tchakei, Kelvin Nashon, Joash Onyango, Elvis Rupia na Abubakar Khomeney.

Mshtuko mkubwa ni kuondoka kwa Rupia, Tchakei na Khomeney ambao walikuwa wanatajwa kuwa nguzo muhimu zaidi kwa Singida msimu huu.

Mastaa hao ni wale ambao timu yenye malengo makubwa haiwezi kuwaacha, kumuacha Rupia kwa sasa ni sawa na Yanga kumuacha Stephen Aziz KI au Pacome Zouzoua.

Kwanini ghafla? Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Singida kinasema kuwa kumekuwa na mgogoro wa chinichini kati ya wamiliki wa timu hiyo.

Hali hiyo imesababisha mmoja kati ya mabosi wakubwa wa Singida kususa na kuamua kuinunua Ihefu ambayo ilikuwa sokoni kwa siri.

"Jamaa ana hela, baada ya kuinunua Ihefu aliwachukua wachezaji sita wale ambao walikuwa chini yake na kuwapeleka kwenye timu yake mpya.

"Hao unaowaona ni wake yaani yeye ndiye alikuwa kila kitu kwa hiyo anaweza kuwapeleka kokote, mambo mengine ni magumu kaka, lakini hata timu hapo itahama na Singida pale itaondoka.

Ni kifo cha Singida? "Kweli Singida itakuwa kwenye wakati mgumu kwa kuwa jamaa ndiye alikuwa kila kitu, akiondoka hawa wanaobaki sidhani kama wanaweza kuendesha timu kwa kuwa hawana mtaji wa kutosha.

"Hii timu matumizi yake ni makubwa, hivyo inahitaji watu wenye fedha za kutosha, siamini kama kwa muda uliobaki wanaweza kusajili wachezaji sita ambao wameondoka.

"Hata ukitazama hawa wachezaji wanaoomba kuondoka kwa kuwa hawajalipwa mishahara ni muendelezo wa sakata ambalo lilianza huku nyuma.

Vipi kuhusu kina Kijili! Chanzo kinasema kama kuna timu inahitaji mchezaji yeyote pale Siginda kwa sasa ambaye hayupo chini ya huyo bosi mkubwa itafanikiwa kumpata kwa kuwa wanasaka fedha.

"Mastaa kama Kelvin Kijili, na wengine wengi wanaweza kuondoka wakati wowote wakipata dili kwa kuwa pia mabosi wanahitaji fedha kwa sasa kuendesha timu," kilisema chanzo.

Kanuni inasemaje! Kanuni ya Ligi Kuu Bara inazitaka klabu zisipokee wala, kutoa wachezaji watano kwa dirisha moja la usajili, lakini inaruhusu hivyo endapo wachezaji hao wamesajiliwa kwa mkopo tu."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live