Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kante, Pogba kutojumuishwa Ufaransa 2026

Pogante Pic Paul Pogba na Ng'olo Kante

Fri, 11 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Siku, saa, dakika, sekunde na milisekunde hazigandi, zimebaki siku 10 kufikia Novemba 20, ili ufunguzi rasmi wa Kombe la Dunia FIFA kuanza kutumia vumbi nchini Qatar.

Wakati ufunguzi ukikaribia bingwa mtetezi wa taji hilo la dunia, Ufaransa ‘Les Blues’ chini ya Kocha Didier Deschamp imepata pigo baada ya kiungo wa kati, Paul Pogba kupata majeraha mapya.

Taarifa rasmi ya wakala wake, Rafael Pimenta alisema Pogba hatakuwepo katika fainali za Kombe la Dunia FIFA 2022 badaa ya kupata majeraha mapya.

Pogba ambaye msimu wa 2022 alitua bure Juventus akitokea Manchester United alisema kiungo huyo hatakuwepo katika fainali hizo kutokana upasuaji goti aliofanyiwa.

Alieleza tathimini ya majeraha aliyofanyiwa jijini Turin na Pittsburgh inaumiza sana kuwaleza kuwa Paul atahitaji muda wa uuguzi na kupona kutokana na upasuaji huo.

Upasuaji ulifanyika kwa lengo la kukarabati jeraha la goti alilopata ndio unaomfanya kukosekana kwani mkadirio ya uponaji na kurudi uwanjani unaonesha kuwa atakua nje hadi mwakani.

Pigo la kwanza kubwa ambalo tayari mabingwa hawa watetezi wamelipata ni kumkosa kiungo mwingine mkabaji, N’Golo Kante ambaye amepata majeraha ya misuli ya nyuma ya paja tangu Agosti 14, Chelsea ilipocheza na Tottenham na kufanyiwa upasuaji.

Jeraha alilopata linamweka nje kwa miezi minne linajulikana kama ‘hamstring injury’na kumfanya afanyiwe upasuaji ili kukarabati misuli na tendoni iliyojeruhiwa.

Wakati Pogba akipata jeraha jipya la paja lijulikanalo kitabibu kama ‘thigh injury’ wiki mbili zilizopita wakati akiwa katika kipindi cha uuguzi na uponaji wa jeraha la goti la zamani lijulikanalo kama Torn Miniscus.

Jeraha la zamani lilijeruhi kijifupa bapa cha plastiki kujulikanacho kitabibu kama miniscus ambacho kipo katikati ya goti kikiwa na kazi ya kusaidia mifupa mikubwa ya goti kujizungusha pasipo kukwanguana na huku kikiwa kama ni kinyonya mawimbi ya uzito

Wakati Ufaransa ikipata pigo la pili kwa wachezaji wake muhimu waliowezesha kupata ubingwa wa dunia mwaka 2018, Kocha Deschamps amesema atatua Qatar na wachezaji watakao kuwa na utimamu tu.

Amesema anaelewa vyema mchango wa Pogba na N’Golo katika eneo la kiungo waliposhinda Kombe la Dunia mwaka 2018 lakini hana jinsi itamlazimu kuangalia wachezaji wengine wa kuziba mapengo hayo.

Kwanini hawakujumuishwa?

Hakuna mtu ambaye hajui kiwango cha viungo hawa wawili ambao uwepo wao katika Timu ya Taifa ya Ufaransa na katika klabu zao huwa na msaada mkubwa sana.

Hata kama pengo lao litazibwa na viungo wengine wa timu hiyo, kukosekana kwao katika eneo la katikati ni pigo katika eneo la ulinzi na ushambuliaji.

Kutokuwepo kwao ni kama vile umeondoa mpiga dramu na mpiga keyboard wa bendi, hivyo vyombo vingine vitapiga ila muziki hautanoga kama ilivyozoeleka.

Hii ni dhahiri N’Golo na Pogba hawatajumuishwa katika kikosi cha Ufaransa kwa kuwa hawatakuwa fiti kwani bado watakua wana vidonda kwa ndani ambayo havijapona kwa zaidi ya asilimia 90%.

Uponaji wa majeraha waliyopata wawili hao ambao wamefanyiwa upasuaji una malengo ya kukarabati na kurudisha utimamu wa viungo hao, hivyo kama hapo awali, hii itachukua muda mrefu.

Misuli ya nyuma ya paja aliyojeruhiwa N’Golo ni ile ambayo iko nyuma ya paja ambayo ndio kwa mwanasoka inafanya kazi sana ikiwamo kukimbia kasi, kupiga mashuti, kuteleza na daluga na kukaba.

Wakati Pogba ambaye ameumia paja na goti ni eneo ambalo kwa mchezaji ndilo linamfanya kukunja mguu na kunyumbulika ili kuweza kudhibiti mpira, kupiga mpira na kupiga chenga.

Maeneo haya ni nyeti sana kwa mchezaji kumwezesha kufanya hekaheka mbalimbali za uwanjani, kila yanapopata majeraha yanaweza kuchukua muda mrefu kupona.

Aina hii ya majeraha yote yanawezekana yameangukia katika majeraha ya tishu laini daraja la tatu ambayo mara nyingi yanahitaji upasuaji ili kukaratabati na kuondoa tishu zilizoharibika kwa kujeruhiwa.

Tayari kocha ameweka wazi anataka kwenda na wachezaji ambao wana utimamu kiafya, hivyo haitaji wachezaji wenye majeraha.

Majeraha ya Pogba

Historia ya majeraha kwa Pogba ni moja kati ya sababu ambazo zinashindilia kutokuwepo kwake Qatar kwani amekua na wakati mbaya katika msimu wa 2022/23 alipotua Juventus akitokea Man United.

Tangu atue katika timu hiyo ya Seria A hakuweza kucheza katika mechi za ligi zaidi ya kucheza mechi za kirafiki kabla ya msimu kuanza ambako ndipo alipopata majeraha ya goti.

Vilevile Pogba aliandamwa na majeraha kuanzia mwaka 2017 akiwa mchezaji wa Manchester United, kipindi ambacho Ufaransa ilikuwa ikipambana kupata tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia 2018 na alikosa mechi 12 za kimataifa kutokana majeraha ya paja.

Baada ya kupona na kurudi kikosi cha Ufaransa na kusaidia kutwaa Ubingwa wa Dunia wa FIFA 2018. Lakini baada ya mashindano haya alikosa mechi 39 wakati wa msimu wa 2019/20 baada ya kupata majeraha ya enka.

Kati ya mwaka 2020/21 na 2021/22 jumla ya michezo 26 hakucheza kutokana na majeraha ya misuli ya nyuma ya paja kabla ya kuachana na Manchester United.

Alitua Juventus msimu huu 2022/23 lakini akapata majeraha ya kifupa bapa cha plastiki kilichopo katikati ya goti wakiwa katika mechi za maandalizi ya msimu huu nchini Marekani.

Jeraha hilo ndilo alilodumu nalo akiliuguza mpaka alipopata hili jingine la paja wakati akiuguza jeraha la zamani.

Alijaribu kuchagua matibabu ya bila upasuaji katika vituo maalum vya mazoezi tiba ya viungo akiwa katika uangalizi maalum kwa malengo ya kumwezesha kujumuishwa katika kikosi kitakachokwenda Qatar lakini matibabu haya hayakusaidia.

Timu ya madaktari ya mifupa inayomtibu Pobga inayoongozwa na Profesa Volker Musahl ambaye ndiye daktari mkuu wa mifupa wa timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Pittsburgh nchini Marekani ilieleza mteja wao kwa sasa anahitaji kuendelea kufanyiwa tathimini ya kina ya majeraha yote aliyonayo na ataendelea kuwa katika uangalizi maalum wakati wa uuguzi wa majeraha hayo.

Matamko haya yameelezwa katika taarifa ya Juventus iliyotolewa Oktoba 31 ikieleza kuwa muda wa kurudi uwanjani siyo hivi karibuni, hivyo kuthibitisha kuwa hatashiriki fainali hizo za FIFA 2022.

Bado Ufaransa haijataja kikosi chake kitakachokwenda Qatar ingawaje kuna asilimia 99 kuwa mastaa hao hawatashiriki fainali hizo.

Tusubiri kuona hatima ya viungo hao wenye umri wa miaka chini 30 kama watapona na kuwa katika kiwango kilekile ambacho kitawawezesha kucheza tena Kombe la Dunia la FIFA 2026.

Chanzo: Mwanaspoti