Mastaa wa Simba, kipa Ally Salim, beki David Kameta 'Duchu' na kiungo Sadio Kanoute ambao sio sehemu ya kikosi cha timu hiyo kinachoivaa Jwaneng Galaxy ya Botswana wamekutana na sapraizi ya aina yake Kwa Mkapa baada ya kuzuiwa kuingia jukwaani kwa dakika kadhaa kabla ya kuruhusiwa.
Mastaa hao ambao walikuwa wanataka kuingia jukwaa la Plutinum lakini wakajikuta wakipigwa 'stop' na walinzi na kuwafanya walazimike kusubiri kwa muda, licha ya juhudi zilizokuwa zikifanywa na kipa Salim kuwaelewesha walinzi na maaskari waliokuwa wamesimama sehemu ya kuingilia eneo hilo.
Baada ya majadiliano ya muda, hatimaye ilipatikana suluhu na wakaruhusiwa kuingia wakisubiri kuwashuhudia wenzao watakaokiwasha na Jwaneng kuwania nafasi ya kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nne ndani ya misimu sita ya michuano hiyo tangu 2018-2019.
Simba inakutana na Jwaneng katika mchezo huo wa mwisho wa Kundi B, ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya misimu miwili iliyopita kwenye uwanja huo kwa mabao 3-1 baada ya awali kuzima ikiwa kwao kwa mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani na John Bocco.
Simba ilianza michuano msimu huo na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuangushwa na kanuni ya bao la ugenini kwani, matokeo ya mwisho yaliyokuwa ni sare 3-3.
Ushindi wa aina yoyote utaivusha Simba kwani itafikisha pointi tisa ikiwa nyuma ya Asec iliyotangulia robo fainali mapema, ambayo nayo usiku huu itavana na Wydad CA ya Morocco.