Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kane ashinda taji lake la kwanza katika soka

Azam Tajii Kane ashinda taji lake la kwanza katika soka

Sun, 11 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya ukame wa miaka 14, hatimaye mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane alishinda taji lake la kwanza katika maisha yake ya soka la kulipwa lakini alikataa kunyanyua kombe hilo.

Kane alishinda taji hilo mbele ya waajiri wake wa zamani Tottenham katika mchezo wa kirafiki wa mashindano ya Visit Malta Cup uliopigwa kwenye uwanja wa Tottenham.

Kane, 31, hajashinda taji lolote katika kipindi chake cha miaka 14 ya soka la kulipwa licha ya uwezo wake mkubwa wa kutupia uliomfanya awe mfungaji bora wa muda wote wa Tottenham na England.

Staa huyu ambaye aliingia katika mchezo huo akitokea benchi dakika 80, aliisaidia Bayern kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 uliowawezesha kuchukua ubingwa huo.

Wakati wachezaji wa Bayern wqanaenda kunyanyua kombe Kane hakuwa sehemu yao ikiwa ni katika kuonyesha heshima kwa Spurs ambayo aliitumikia kwa miaka zaidi ya 10 kabla ya kuondoka katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana.

Kamera zilimnasa Kane akifatwa na baadhi ya wachezaji wa Bayern waliokuwa wamebeba kombe wakimtaka kulishika lakini kapteni huyo wa kikosi hicho alikuwa akiwakatalia kwa kutikisa kichwa mara kwa mara.

Baada ya video hizo kusambaa katika mitandao ya kijamii mashabiki wengi walimsifia kwa uzalendo wake.

"Heshima kwa gwiji wa Tottenham aliyekataa kunyanyua kombe dhidi ya klabu yake ya zamani,"alisema shabiki mmoja na mwengine akafuatia kwa kuandika "Nzuri sana.", mwengine akaandika "Heshima!."

Mashabiki hao walitoa maoni hayo kupitia mtandao wa X zamani Twitter.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live