Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kane amewasoma Man United

HARRY KANE M 1140x640 Harry Kane

Sun, 30 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Harry Kane amesema amewasikia mashabiki wa Manchester United kile walichokuwa wakiimba wakijaribu kumhamasisha atue kwenye kikosi chao cha Old Trafford mwishoni mwa msimu huu.

Kutokana na hilo, straika Kane sasa amepanga kukutana na mwenyekiti wa Tottenham Hotspur, Daniel Levy kwa ajili ya kuweka mambo sawa, huku bosi huyo wa miamba hiyo ya London akipanga pia kukutana na mastaa wa timu hiyo kujadili baadhi ya mambo.

Nahodha huyo wa England alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Spurs wakati aliposaidia timu hiyo kutokea nyuma na kupata matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Man United nyumbani juzi Alhamisi usiku.

Na wakati wa mapumziko ya mchezo huo, wakati Man United ilipokuwa mbele kwa mabao 2-0, mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford walisikika wakiimbia: “Harry Kane, tutaonana Juni.”

Kocha wa Man United, Erik ten Hag anasaka mshambuliaji wa kati kwa udi na uvumba huku akitaka kufanikisha hilo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi ili kuanza msimu ujao akiwa na Namba 9 wa maana kwenye fowadi yake.

Man United kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili Kane, huku straika mwingine anayeripotiwa kuwa kwenye rada za miamba hiyo ambao ni mabingwa mara 20 wa England ni mkali wa Napoli, Victor Osimhen.

Alipoulizwa kama alikuwa akisikia nyimbo zilizokuwa zikiimbwa kutaja jina lake, straika huyo supastaa alisema: “Nimesikia walichokuwa wakisema, lakini kwa sasa nimeelekeza nguvu kwenye timu yangu nikijaribu kuisaidia imalize msimu vizuri.”

Kutoka nyuma na kupata sare kumewaokoa Spurs kupata kipigo cha pili mfululizo kwenye Ligi Kuu England baada ya wikiendi iliyopita kukumbana na na kipigo cha mabao 6-1 kutoka kwa Newcastle United, ambapo mashabiki wa timu hiyo walilazimika kurudishiwa viingilio vyao kama fidia baada ya timu kuruhusu kuwa nyuma kwa mabao 5-0 katika dakika 21 za mwanzo huko St James' Park.

Baada ya kipigo hicho, Spurs iliamua kumfuta kazi aliyekuwa kocha wa muda Cristian Stellini na sasa timu imekabidhiwa kwa Ryan Mason, ambaye ataisimamia hadi mwisho wa msimu na uamuzi huo uliofanyika baada ya mwenyekiti Levy kukutana na wachezaji.

Kane alisema: “Mwenyekiti aliomba tukutane. Siwezi kusema kilichozungumzwa, lakini kitu muhimu kwangu kilikuwa kuwafanya wachezaji watambua ni wapi tunaelekea kwa sasa. Ni wazi kutokea nyuma na kupata matokeo haya ni jambo kubwa. Hayakuwa matokeo tuliyopata.

“Yalikuwa mazungumzo mazuri kwa kila mtu na sasa kila mmoja atajaribu kujitolea kwa kadri yake anavyopata nafasi ili kumaliza msimu huu na kitu fulani. Bado tunashindania Nafasi ya nne, lakini kama si nafasi ya nne, basi iwe ya tano au sita, juu juu kwa kadri tunavyoweza.

“Kwenye hii ligi, kuna ushindani sana, unaweza kumaliza nafasi ya nane au tisa usipokuwa makini. Hilo ndilo ndilo linalotusukuma kufanya vizuri. Na nimefurahi kwa namna tulivyojibu mapigo.”

Spurs mchezo wao ujao kwenye Ligi Kuu England watakwenda Anfield kuwakabili Liverpool kesho Jumapili na straika Kane amewataka wachezaji wenzake kwenye kupambana kama walivyofanya dhidi ya Man United ili kurudi nyumbani na pointi zote tatu.

Alipoulizwa kama wanaweza kushinda Merseyside, Kane alisema: “Nafikiria hivyo. Tumezungumzia hizi mechi mbili ni kupata matokeo, tutatafuna namna ya kushinda, tutatafuta njia bora kwa sababu tutakuwa ugenini. Liverpool nao watahitaji kushinda.

“Anfield ni mahali pagumu sana pale. Nao wapo kwenye nafasi kama yetu ya kupambana kutaka nafasi ya juu, hivyo kutakuwa na vita kubwa. Ni juu yetu sasa kucheza kwenye viwango bora kama tulivyofanya kipindi cha pili dhidi ya Man United ili kumaliza mechi ya Anfield.”

Spurs kwenye Ligi Kuu England kwa sasa inashika nafasi ya tano ikiwa imekusanya pointi 54 katika mechi 33 ilizocheza, ikishinda 16, sare sita na vichapo 11, ikifunga mabao 60 na kufungwa 53.

SPURS MECHI ZAO TANO ZILIZOBAKI

-Aprili 30 vs Liverpool (ugenini)

-Mei 6 vs Crystal Palace (nyumbani)

-Mei 13 vs Aston Villa (ugenini)

-Mei 20 vs Brentford (nyumbani)

-Mei 28 vs Leeds United (ugenini)

Chanzo: Mwanaspoti