Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kane aipeleka Bayern Robo Fainali UEFA

Kane Two Goals Kane ipeleka Bayern Robo Fainali UEFA

Wed, 6 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mabao mawili ya mshambuiliaji nyota kutoka Engand, Harry Kane yameiwezesha Bayern Munichi kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kuzima Lazio ya Italia kwa mabao 3-0 na kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 3-1.

Katika mechi ya awali ugenini, Bayern ilichapwa bao 1-0 na usiku wa jana ikiwa Uwanja wa nyumbani wa Allianz Arena, iliingia ikiwa na kazi ya kusaka ushindi ili kupoza presha kubwa aliyonayo kocha Thomas Tuchel baada ya mambo kqenda harijojo katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) ikiwa imeachwa pointi 10 na Bayer Leverkusen.

Mabao hayo mawili yamemfanya Kane kufikisha jumla ya mabao sita katika michuano hiyo akiwa na kikosi hicho kilichomsajili msimu huu kutoka Tottenham Hotspur, lakini yamemfanya afikishe 33 aliyoifungia Bayern tangu ajiunge nayo, yakiwamo 27 ya Bundesliga akiwa ndiye kinara kwa sasa. Mabao hayo sita yamemfanya alingane na Kylan Mbappe wa PSG ambaye usiku wa jana pia alifunga mabao mawili wakati timu hiyo ya Ufaransa ikiifumua Real Sociedad ya Hispania.

Kane alifunga bao la kwanza dakika ya 38 akisindikiza kwa kichwa mpira uliopigwa na Raphael Guerreiro na katika dakika za majeruhi kabla ya mapumziko wenyeji waliandika bao la pili kupitia Thomas Muller aliyesindikiza shuti kali la Matthijs de Ligt.

Kipindi cha pili kilianza kwa wenyeji kuanza na kasi huku wageni Lazio wakipambana kutaka kurejesha mabao hayo, lakini alikuwa ni Harry Kane tena aliyekwamisha bao la tatu lililowazima kabisa vijana wa Maurizio Sarri katika dakika ya 66 akiuwahi mpira uliotokana na shuti la Leroy Sane kuokolewa na kuipa wa Lazio na yeye kuutumbukiza wavuni.

Bayern imeingia robo fainali ikiwa ni msimu wa tano mfululizo na ndilo taji inayoweza kulibeba msimu kama italikomaliza kwani kwenye Bundesliga mambo ni magumu na tayari imeshatema mataji mengine ya ndani huko Ujerumani.

Nayo PSG ya Ufaransa ikiwa ugenini huko Hispania ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Real Sociedad na kuifanya ifuzu robo kwa jumla ya mabao 4-1 kwani katika mchezo wa kwanza jijini Paris, wababe hao walishinda 2-0.

Katika mechi ya jana usiku, mabao yote ya PSG yaliwekwa kimiani na Kylan Mbappe katika dakika za 15 na 56. Mechi za mkondo wa pili kwa hatua ya 16 Bora zinaendelea leo kwa Manchester City ya England kuikaribisha FC Copenhagen ya Denmark, huku Real Madrid ikiwa wenyeji wa RB Leipzig. Katika mechi za mkondo wa kwanza Man City ilishinda ugenini mabao 3-1 ilihali Madrid ikishinda 1-0. Matokeo yoyote mazuri kwa wenyeji yatawafanya ziungane na Bayern na PSG kutinga robo fainali na kusikilizia timu nyingine nne za mwisho zitakazopatikana katika mechi za wiki ijayo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live