Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamwe, Ahmed Ally waita mashabiki Taifa Stars

Ahmed Ally X Ally Kamwe Kamwe, Ahmed Ally waita mashabiki Taifa Stars

Mon, 2 Sep 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Maofisa habari wa timu za Yanga, Simba na Azam FC wamewaita mashabiki wajitokeze kwa wingi katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afvon) dhidi ya Ethiopia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jumatano, Septemba 4 kuanzia saa 1:00 usiku.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa Taifa Stars katika mashindano hayo ya kufuzu Afcon na baada ya kuikabili Ethiopia itasafiri hadi Ivory Coast kukabiliana na Guinea, Septemba 10.

Wakizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam, Ally Kamwe wa Yanga, Ahmed Ally (Simba) na Hasheem Ibwe (Azam) walisema kuwa mashabiki wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili kuipa hamasa Taifa Stars ipate ushindi dhidi ya Ethiopia kwani mechi hiyo ndio itatoa muelekeo wake kwenye mashindano hayo.

“Tunazungumzia makundi ya kufuzu Afcon kwenda Morocco 2025. Kwenye makundi zinakuwa timu nne. Bila kupepesa pepesa macho zote tunazimudu. Huyu Ethiopia pengine watu wote ndio wanampigia hesabu kupata pointi sita hivyo na sisi tunapaswa kupigia hesabu pointi zao sita.

“Hii mechi ujumbe wetu Watanzania kwa wachezaji, haya mambo Tanzania kila tunapokwenda kwenye hizi mechi za kufuzu, mechi za mwanzo tumekuwa tukisuasua hivi halafu tunasubiri sandakalawe mwishoni, safari hii turekebishe. Huyu anatakiwa apigwe nyingi,” alisema Kamwe.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa mchango wa hamasa ya mashabiki una nafasi kubwa ya kuifanya Stars iibuke na ushindi katika mechi hiyo.

“Tunafahamu jambo ambalo liko mbele yetu kwa maana ya mchezo husika. Mchezo ambao unahitaji nguvu, sauti na sapoti ya kila Mtanzania. Tukumbuke kwamba ni mchezo wa kwanza kuwania kufuzu Afcon 2025. Tunapaswa kuanza vizuri na kupata ushindi katika mchezo huu.

“Ni mchezo ambao utatoa taswira ya kundi letu katika mashindano haya. Ni vyema tukashinda mchezo huu ili tuepuke presha kama za misimu iliyopita. Yote ni kwa sababu hatukuanza vizuri kampeni yetu ya kufuzu na kuanza vizuri ni kushinda dhidi ya Ethiopia. Hadi sasa tumeshatengeneza mazoea yaliyotengeneza tabia ya kufuzu Afcon,” alisema Ahmed Ally.

Ofisa habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema kuwa atatoa tiketi za Shilingi 600,000 kwa mashabiki ili kuunga mkono Taifa Stars.

“Ni jambo la kujivunia na jambo la kujifaharisha nalo. Tiketi za mzunguko ninazo za kutosha za laki sita (Sh 600,000). Zitakabidhiwa kwa Ndimbo halafu yeye atajua hao watu wanaingia vipi.

“Lakini tunajua nguvu ya mashabiki. Wao ndio wanacheza kwa nafasi kubwa pengine kuliko hata wachezaji pale uwanjani. Kwa ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki na Kati, muitikio wetu kwenye mpira wa miguu kuanzia klabu zetu, jina ambalo limetengenezwa kwenye mpira wetu na vingine vyote ambavyo vinahusiana na mpira wa miguu, kwenye stori za michezo sisi ni namba moja kwa hiyo tunatengeneza ukubwa wa soka letu kwenye mashindano kama haya,” alisema Ibwe.

Timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu fainali za Afcon ambazo zitafanyika Morocco katika miji yake sita kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2016.

Miji hiyo sita ambayo itaandaa mechi za Afcon huko Morocco ni Agadir, Casablanca, Fez, Marrakesh, Rabat na Tangier.

Taifa Stars inawania kushiriki Afcon kwa mara ya nne baada ya kufanya hivyo mwaka 1980, 2019 na 2023.

Chanzo: Mwanaspoti