Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kambole awasha moto Zesco United, aanza na Hat-Trick

Lazar Lazarious Kambole

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga ambaye hakupata nafasi ya kucheza mechi hata moja tangu amejiunga na timu hiyo kutoka Kaizer Chiefs hadi alipoachwa na kujiunga na Zesco, Lazarous Kambole anaendelea kuonyesha makali yake baada ya kuifungia timu hiyo mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Kambole hakupata nafasi ya kuitumikia timu hiyo kwenye mechi za mashindano kutokana na kupata majeraha kwenye mechi ya kirafiki kujiandaa na msimu mpya dhidi ya Namungo mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Avic Town Kigamboni hadi alipoondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Tuisila Kisinda.

Mshambuliaji huyo wa Zesco ambaye amesajiliwa dirisha dogo la usajili tayari amehusika kwenye mabao manne akiwa na timu hiyo ambayo ameitumikia kwenye michezo miwili hadi sasa.

Mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo ilikuwa Januari 28 ugenini dhidi ya Lumwana Radiants aliisaidia timu yake kuambulia pointi moja baada ya sare ya bao 1-1 akiifungia timu yake dakika ya 34.

Jumamosi alishuka tena dimbani kuipambania timu yake kupata matokeo dhidi ya Green Eagles mchezo ambao ulichezwa siku mbili baada ya mvua kubwa kunyesha na kukatisha mchezo huo.

Siku ya kwanza ilichezwa dakika 55 huku Zesco wakifunga bao 1-0 huku Kambole akihusika kutoa pasi ya bao na mchezo huo uliendelea siku iliyofuata (Jumapili) ambapo timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 mawili yakifungwa na Kambole.

Mabao ya Kambole yalifungwa dakika ya 61 na la pili alifunga dakika za nyongeza akiisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kuasisti moja.

Akizungumza Kambole alisema ni mwanzo mzuri kwake na umemjengea kujiamini zaidi huku akisisitiza kuwa anaamini ataendelea kufunga kila anapopata nafasi ya kucheza.

"Mchezaji yeyote ambaye amesajiliwa kwenye timu mpya anakuwa na presha lakini mara baada ya kupata nafasi na kufunga nimeweza kupunguza kwasababu nina imani na nimekuwa nikiamini katika kufunga kwenye kila mchezo."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live