Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kambi ya kishua Yanga Morocco hii hapa

Yanga Pic 2 Data Kambi ya kishua Yanga Morocco hii hapa

Sat, 14 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

JESHI la Yanga lenye wachezaji 28 limekamilika hii ni baada ya Jesus Moloko, Heritier Makambo na Djuma Shaban kutua usiku wa kuamkia jana kutoka DR Congo na kesho wataondoka na wenzao kwenda Rabat, Morocco kwa ajili ya kambi ya maandalizi msimu wa 2021-2022.

Nyota hao na wenzao waliosajiliwa na waliokuwapo msimu uliopita wataenda Morocco katika kambi ya siku 12 itakuwepo kwenye Kituo cha Soka cha Mohammed VI, kilichopo kilomita 12 kutoka pale ambapo watani wao, Simba wameweka kambi tangu mapema wiki hii katika hoteli ya Dawliz Resort & SPA.

Kituo hicho ambacho ndipo kutakapokuwa kambi ya wachezaji 28 wa Yanga na viongozi wasiopungua sita mbali na kocha Nasreddin Nabi kinamilikiwa na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) na ni bonge ya kambi ya kisasa.

Kituo hicho cha kisasa zaidi kilijengwa kwa msaada wa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI kwa lengo la kuibua vipaji na kuendeleza michezo.

Ni mwendo wa dakika zisizopungua 20 kutoka mji mkuu wa Morocco, Rabat kufika kitongoji cha Sale ambacho kituo hicho kipo. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 30 na miundombinu ya michezo mbalimbali.

Kutembelea eneo lote hilo unahitaji usafiri wa ndani ambao ni gari maalumu na ili kufika katika kila miundombinu, utahitaji sio chini ya saa tatu. Mwandishi wa makala haya alitembelea kituo hicho mwaka jana kushuhudia yafuatayo:

KITUO KILIVYOANZISHWA

Ujenzi wa Kituo cha Michezo cha Mohammed VI ulianza 2016 na kumalizika mwaka jana. Kujengwa kwa kituo hicho kunalenga kuinua michezo Morocco na kuwa namba moja Afrika na duniani.

Kutokana na kuwa na kiu ya maendeleo, Mfalme Mohammed VI alianzisha mradi huo kwa kushirikiana na washauri wake. Ukosefu wa wachezaji wenye vipaji na kituo cha kisasa cha michezo, pia kulichochea mfalme huyo kuanzisha mradi mkubwa na namba moja Afrika.



Pamoja na kuwa na washauri wake, Shirikisho la Soka la Morocco kwa kushirikiana na mfalme liliwaita wataalamu wa ndani kubuni mchoro na mradi mzima wa kituo ambacho mpaka sasa kimeanza kuiletea matunda nchini hiyo.

Moja ya mikakati ni kuhakikisha kuwa nguvu kazi zote katika ujenzi wa kituo hicho unafanywa na wataalamu wa Morocco wenyewe. Mradi huo umegharimu Euro 62 milioni (zaidi ya Sh150 bilioni) kukamilika na kutoa ajira kwa watu sio chini ya 200. Watalaamu wa uchoraji majengo, ujenzi na miundombinu mingine walipewa kazi ya kubuni aina ya mchoro ambao utakuwa wa aina yake ili kukamilisha hitaji la mfalme.

Wataalamu na wadau wa soka walishirikishwa katika mradi huo ili kupata kitu sahihi ambacho kinakidhi mahitaji. Kulikuwa na wataalamu wa soka, makocha, madaktari, waamuzi na wengine wengi ambao kila mmoja alitoa hitaji lake. Haikuwa kazi ndogo kwani ilichukua sio chini ya miezi sita kukamilisha mchoro wa kituo.

Mpaka sasa kituo hicho kinapokea wageni wa kutembelea na vilevile mikutano Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na Afrika (Caf) imefanyika hapo.

NDANI YA KITUO

Kituo cha Mohammed VI kina uwezo wa kuwalaza watu 400 kwa wakati mmoja.

Eneo hilo lina hoteli nne na katika kila hoteli ina eneo la mikutano, chumba cha habari, eneo la kupumzika, mgahawa, eneo la michezo mbalimbali ya kuburudisha kama pool table na gym ya mazoezi.



Pia, kila hotel ina sauna na mabwawa ya kuogelea madogo ambayo yanatumiwa na wachezaji na makocha.

Mbali ya vitu hivyo, kuna eneo la mkutano wa makocha na wachezaji lenye vifaa vya kisasa vya kufundishia na televisheni ambayo unaweza kuitumia pia kufanyia marejeo ya mechi na vilevile kupata taarifa za timu pinzani.

Vilevile kuna vyumba vya makocha na wakurugenzi wa ufundi ambao wanaweza kukutana na kujadili mambo ya timu. Pia kuna eneo la matibabu lenye vifaa vya kisasa vya kuchukulia vipimo na kutibu.

Hapa kuna chumba cha kupima masuala ya moyo na magongwa mengine, na kuna bwala la kuogelea kwa ajili ya matibabu (rehabilitation swimming pool) lenye baiskeli ya mazoezi, maji yanayowenda kinyume na mwelekeo wako.

Eneo hilo la bwawa la kuogelea limewekwa kwa ajili ya kutibu wagonjwa mikono, mabega, mbavu na miguu.

Mchezaji atatakiwa kunyonga baiskeli akiwa kwenye maji, kutembea akipingana na maji, kuogelea akipingana na maji huku eneo la chini lina kioo maalumu ambacho wataalamu wa tiba na chakula wanakaa kuangalia jinsi anavyofanya zoezi hilo kwa kutumia vifaa maalumu.

Kwa sababu wanamichezo wana magonjwa ya aina nyingi, wataalamu wa kituo pia wameweka chumba kwa ajili ya kupata ubaridi (cryo air) ambapo mchezaji mwenye kuhitaji hutakiwa kukaa sio chini ya dakika tatu, huku chumba kikiwa na sentigredi hasi inayohitajika kwa mujibu wa maelezo ya tabibu. Chumba hiki kina ubaridi hadi hasi joto 110.

VIWANJA VYAKE SASA

Kituo cha Michezo cha Mohammed VI kina viwanja vinane vya mpira wa miguu. Viwanja hivyo vina urefu zaidi ya mita 120 na vinapunguzwa kutokana na mahitaji ya timu. Kuna uwanja wa ndani ambao umejengwa kwa ajili ya timu kufanya mazoezi pamoja na hali ya hewa kubadilika.

Kwa hali ya hewa ya Morocco, sio mvua tu inasababisha mazoezi kutoendelea, bali hata jua nalo linasababisha. Hivyo hali hiyo ikitokea timu itafanyia mazoezi kwenye uwanja wa ndani. Uwanja huo pia unatumika kwa ajili ya kozi za makocha, waamuzi na wengineo. Unaingiza zaidi ya watu 1,000.

Pia, kuna uwanja wenye nyasi mchanganyiko - zile za asili na bandia ambao eneo la kuchezea pia linapunguzwa kutokana na mahitaji.

Kuna uwanja wa mpira wa ndani (futsal), uwanja wa soka la ufukweni na viwanja vingine vinne ambavyo kila kiwanja kina jengo linaloweza kukaliwa na timu mbili.

Pia, kuna uwanja wa tenisi na bwawa la kuogelea lenye urefu wa mita 50 na vilevile kuna shule ya michezo ambayo mpaka sasa ina wanafunzi 120 ambao mbali ya kusoma masomo ya michezo, pia wanasoma masomo mengine.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz