Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kambi Yanga yanoga

E7247f453bd14e1dcdb755611b188bfa.jpeg Kambi Yanga yanoga

Mon, 5 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WACHEZAJI wawili wa kimataifa wa klabu ya soka ya Yanga, Saidi Ntibazonkiza na Haruna Niyonzima tayari wameripoti kwenye kambi ya timu hiyo iliyopo Avic Town Kigamboni kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezwa mwishoni mwa wiki hii.

Wawili hao walirudi makwao kujiunga na timu zao za taifa za Burundi na Rwanda katika kuwania kufuzu fainali za Afcon zitakazofanyika Cameroon mwakani.

Akizungumza na gazeti hili jana. Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema nyota hao wawili tayari wameripoti kambini na wameshaanza mazoezi na wachezaji wengine wakijiandaa na mchezo wao wa ligi dhidi ya KMC utakaochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

“Kikosi chetu kimekamilika mazoezini tulianza kuwapokea wachezaji waliokuwa timu ya taifa, Taifa Stars na juzi tukampokea Tonombe Mukoko aliyekuwa na timu yake ya Congo (Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo) na kundi la mwisho ni Niyonzima na Ntibazonzika,” alisema Bumbuli.

Alisema kukamilika kwa kikosi chao kunampa kocha wao Juma Mwambusi nafasi pana ya kuchagua wachezaji wa kutumia kwenye mchezo huo ambao wamepania kushinda ili kuendelea kuongoza ligi.

Alisema kocha Mwambusi amemhakikishia kwamba timu hiyo kwa asimilia kubwa ipo katika ubora wa hali ya juu baada ya kutumia vyema wiki tatu za mapumziko kwa mazoezi.

Yanga ambao ndio vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakiwa na pointi 50, hivi karibuni walilifuta kazi benchi lao la ufundi ambalo lilikuwa likiongozwa na kocha Cedric Kaze na linaongozwa na kocha mkuu wa muda, Mwambusi hadi mwishoni mwa msimu huu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz