Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya usimamizi isigeuke chaka la nia ovu

Auchoooa Kamati ya usimamizi isigeuke chaka la nia ovu

Mon, 25 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna shaka kwamba Khalid Aucho alionekana akimpiga na kiwiko kiungo wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

Na hakuna shaka kwamba mwamuzi wa mchezo huo alimuonyesha Aucho kadi ya njano kwa tukio ambalo mpuliza filimbi huyo hakuliona zaidi ya kuelezwa na mwamuzi msaidizi wa kwanza ambaye pia aliona tukio hilo kwa mbali kwa kuwa lilitokea upande wa pili wa uwanja tofauti na eneo lake analoruhusiwa kukimbia kufuatilia mchezo.

Na kwa kuwa baada ya maelezo yale, mwamuzi Emmanuel Mwandembwa aliona adhabu iliyostahili ilikuwa ni kadi ya njano, usingetegemea chombo kingine kifanye uamuzi mwingine dhidi ya Aucho zaidi ya ule wa Mwandembwa.

Na kama Mwandembwa, ambaye uamuzi wake uwanjani ni wa mwisho isipokuwa katika mazingira machache yaliyo katika teknolojia, alifanya makosa kutoa adhabu ndogo, basi adhabu ingekuwa kwake na si kwa mchezaji.

Lakini Kamati ya Usimamizi wa Ligi, ambayo ndiyo imeibuka kuwa kamati muhimu kuliko nyingine zote za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikamuadhibu Aucho kwa kumfungia kucheza mechi tatu na faini ya Sh500,000 juu.

Niliandika takriban wiki mbili zilizopita kuhusu uamuzi huo mbovu wa Kamati ya Usimamizi wa Ligi, na leo nimesukumwa tena kuandika baada ya kukataa ombi la Yanga la kutaka iangalie upya uamuzi wake. Hili ni suala ambalo linaweza kutumiwa vibaya zaidi endapo halitakemewa na hasa jinsi Kamati ya Usimamizi wa Ligi ilivyochezea kanuni kwa kuacha ile inayomuepusha Aucho na adhabu ya kufungiwa mechi tatu na faini kwa kuwa refa alishahukumu, hivyo hakuna chombo kingine kinachoruhusiwa kuhukumu, na kuchukua ile isiyoendana na tukio.

Kamati ya Usimamizi wa Ligi ilipata wapi hoja ya kuadhibu mchezaji kwa tukio la uwanjani ambalo limeshafanyiwa uamuzi na refa? Haikupata kanuni yoyote ya kuhalalisha nia hiyo, ndio maana ikaacha kanuni ya 41:5 (2) inayohusiana na kupiga au kupigana na badala yake ikatumia kanuni nyingine.

Kamati imekariri kanuni ya 41:5 (5.3) ya Ligi Kuu kuwa ndio iliyotumika kumuadhibu kiungo huyo wa kimataifa wa Uganda.

Kanuni hiyo inasema “Mchezaji atakayefanya jambo lolote kati ya yafuatayo atafungiwa michezo mitatu (3) na faini isiyopungua Sh500,000 mpaka Sh 2 milioni”. Katika kipengele cha 5.3 kinachotaja kosa ambalo kamati ilimtuhumu na kumuadhibu Aucho kinataja kosa hilo kuwa ni ‘Kumshambulia mwamuzi, kiongozi, mtazamaji au mtu yeyote kwa namna yoyote ile, iwe kwa matusi au vitendo’ .

Ni dhahiri kuwa kamati iliacha kosa la msingi kwa sababu lilishaadhibiwa na mwamuzi na kwenda kuibua kosa jingine ambalo kwa kweli halionekani kama linahusu hasa tukio la Aucho. Kwa mujibu wa kanuni hiyo ya 41, kipengele ambacho kingemtia hatiani Aucho ni 5.2 kinachotaja kosa lake kuwa ni ‘kupigana/kupiga kabla, wakati wa mchezo au mara tu baada ya mchezo kumalizika’.

Lakini Kamati ya Usimamizi wa Ligi iliamua kukwepa kipengele hiki kwa sababu tayari mwamuzi alishaona kosa la Aucho halikufikia kiwango cha kupiga au kupigana na kama mwamuzi msaidizi alimwambia kuwa alipiga, Mwandembwa aliona hakukuwa na ukubwa wa kitendo hicho unaostahili kadi nyekundu kwa kuwa alienda kumuangalia Ajibu na kuridhika na maoni yake.

Kwa maana hiyo unaona kabisa kuwa kilichotakiwa ni Aucho kuadhibiwa, pengine kwa fikra kwamba kila mtu aliona tukio hilo. Lakini bado mchezo wa mpira wa miguu unasimamiwa na kanuni ambazo ndio busara kuu na si maoni mengine yoyote. Na kanuni kuu ya uamuzi ni maoni ya refa wa kati ndiyo yanayotawala na hivyo akikosea, yeye ndio hubebeshwa mzigo na si kikundi cha watu kumpunguzia uzito mwamuzi.

Kamati ikiendelea hivi itakuwa chaka la hila na uovu na uamuzi huu utakuja kurejewa baadaye katika tukio jingine kama hilo iwapo kamati itatetereka. Na isipoterereka ndio mbaya zaidi kwa kuwa ndio utakuwa mwanzo wa kuvuruga maamuzi ya refa kwa kutafuta vikanuni vya kuhalalisha nia ovu. Haitaishia hapo.

Kamati ya Usimamizi wa Ligi isijibebeshe majukumu ambayo haistahili. Kuna makosa ambayo ni lazima yaende Kamati ya Nidhamu ambayo ndio hasa iko karibu na dakika 90 za mchezo. Matukio yote yanayotokea kabla, wakati na baada ya mchezo, ambayo hayahusiani na uamuzi wa refa, kikanuni unatakiwa uende Kamati ya Nidhamu.

Ndio maana unasikia Ligi Kuu ya England imemshtaki mchezaji au kocha au shabiki kwa Chama cha Soka. Ni kwa sababu kuna mfumo huo unaokipa chombo fulani mamlaka ya kushughulikia matukio fulani yasiyohusiana na uamuzi wa refa.

Kamati ya Usimamizi wa Ligi imekabidhiwa majukumu ambayo yalitakiwa yafanywe na Kamati ya Nidhamu, hasa yale yanayohitaji haki ya msingi ya kusikilizwa. Na uamuzi ambao refa huufanya, hauna haki hiyo ya asili ya kusikilizwa.

Maana yake, kama Kamati ya Usimamizi wa Ligi ilianzisha kosa tofauti na yale yaliyoonwa na mwamuzi, ilitakiwa imshtaki Aucho na apewe haki ya asili ya kujitetea kabla ya kumuadhibu. Kimsingi, Kamati ya Usimamizi wa Ligi haitakiwi kuanzisha kosa, isipokuwa yale ambayo yalitokea wakati mchezo umesimama na mwamuzi hakuyaona na kamati ina ushahidi wa picha za marudio.

Lakini hapa kwa Aucho kamati imechemka na si vibaya kama itajirudi na kusahihisha uamuzi wake kwa kuwa uamuzi huo unajenga marejeo mabaya kwa mpira wetu huko mbele. Hatujui nani atatafsiri nini huko mbele na hatujui kama wajumbe wa kamati hiyo watakuwa haohao huko mbele. Kwa hiyo ni muhimu kusahihisha dosari zinazoweza kuvuruga mpira wetu.

Bila ya kujisahihisha, Kamati ya Usimamizi wa Ligi inaweza kugeuzwa chaka la hila na nia ovu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live