Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kamati ya saa 72 iundiwe mwongozo wa maamuzi

Refa T438 Kamati ya saa 72 iundiwe mwongozo wa maamuzi

Tue, 20 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utumiaji wa kanuni zozote ni lazima ufanyike kwa umakini, busara na maarifa kwa kuwa unafanyika kwa kutafsiri hiyo kanuni na kutoa uamuzi.

Na wakati mwingine huwa kuna mwongozo wa matumizi ya kanuni, kwa hiyo inakuwa ni tatizo kubwa pale kanuni inapokuwa haina maelezo ya kutosha (blanket statement), kama ilivyo kanuni ya 12:8 ya Kanuni za Ligi Kuu Bara.

Kanuni hii, ambayo imekuwa maarufu kati ya kanuni zinazotumiwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, imewapa wajumbe wake hadhi ya refa asiye uwanjani, lakini mwenye mamlaka makubwa kuliko yule ambaye misingi ya mpira wa miguu imekubali kuwa maoni yake ndiyo yatawale tafsiri za sharia za soka.

Katika taarifa yake ya wiki iliyopita, kamati hiyo maarufu kwa jina la Kamati ya Masaa 72 (kwa dhana kwamba itapitia michezo yote ya raundi moja inayotakiwa ichezwe ndani ya siku tatu), kadi ya pili ya njano aliyopewa mchezaji wa Tanzania Prisons, imefutwa.

Katika tukio hilo, beki wa Yanga, Bakari Mwamnyeto anaonekana kupambana na mshambuliaji wa Prisons, Khamis Zabona Mayombya na baadaye mshambuliaji huyo kuonekana akidondokea mbele na kuukamata mpira.

Inaonekana, kwa maoni ya refa wa mchezo huo, Mayombya alitaka kumdanganya refa alisukumwa na hakusubiri filimbi na badala yake akaudaka mpira na kutaka kumwonyesha refa kuwa amechezewa vibaya.

Kwa kosa la kushika mpira kwa makusudi, refa akamwonyesha kadi ya pili ya njano iliyomaanisha anatolewa nje kwa kadi nyekundu.

Lakini wale wataalamu wetu, ambao kanuni zinawapa mamlaka hadi ya kushughulikia vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo hutakiwa kupelekwa Kamati ya Nidhamu, wameona kosa la kukamata mpira alilofanya Mayombya lilitokana na kusukumwa na hivyo kufuta “kadi ya pili ya njano”.

Kamati imesema uamuzi huo umezingatia kanuni ya 12:8 ya Kanuni za Ligi Kuu inayosema: “Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi inaweza kufuta adhabu ya kadi yoyote iliyotolewa uwanjani na mwamuzi na kuondoa inayoambatana na kadi hiyo endapo inathibitika bila mashaka mtuhumiwa hakustahili kadi hiyo.”

Hayo ndiyo maelezo yanayochukuliwa yamejitosheleza ambayo hutumiwa na kamati kubatilisha maamuzi ya mwamuzi wa kati kutokana na maoni ya wajumbe ambao nadhani wengi wao hawana ujuzi wa uamuzi.

Pamoja na kwamba kufuta adhabu zilizotolewa na mwamuzi wa kati ni kitu kikubwa katika mchezo, kanuni haielezi mazingira ambayo kamati inaweza kuyatumia kufuta adhabu iliyotolewa uwanjani.

Pamoja na maendeleo ya teknolojia yaliyoleta Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R), bado haijafikia tukio linaloadhibiwa kwa kadi ya njano likarudiwa kwenye video, kiasi cha mwamuzi kuitwa pembeni ya uwanja kwenda kujiridhisha kwa kuangalia picha za marudio za tukio hilo.

Bado ni maamuzi makubwa tu yanayostahili kadi nyekundu ya moja kwa moja ndiyo yanayoweza kuangaliwa vizuri na V.A.R na inapotokea tukio lina utata, ndipo mwamuzi hutakiwa kwenda kujiridhisha kwenye runinga.

Hata kama kadi ya njano anayopewa mchezaji ni ya pili inayosababisha atolewe uwanjani, bado V.A.R haiwezi kulirudia tukio hilo kwa kina kiasi cha kumtaka refa wa kati aende kujiridhisha kwenye picha za marudio.

Mechi imeisha na mwamuzi hawezi kurudi kwenye runinga, kwanza haipo, nani mwingine anafanya uamuzi unaohusu kadi ya njano?

Kanuni inasema “endapo inathibitika bila mashaka kuwa mtuhumiwa hakustahili kadi”. Imethibitishwaje bila ya shaka kuwa mtuhumiwa hakustahili kadi? Hadi sasa, kamera zinazoweza kutumiwa na Azam TV kwa matukio ya golini hazizidi mbili.

Kuona tukio kutoka pande zote kwa mechi za Ligi Kuu ni tatizo kubwa kiasi kwamba ukitumia kama ushahidi utakuwa na mapungufu. Sasa imethibitikaje “bila mashaka” Mayombya alisukumwa?

Picha zinaonyesha wawili hao wakiwa sambamba kuufuata mpira na ghafla Mayombya anadondokea mbele. Alijirusha au alisukumwa kutokea nyuma? Ni kamera gani ilitumiwa na kamati kuona mkono ukimsukuma Mayombwa kutokea nyuma?  

Hapa ndipo kuna umuhimu wa kuwepo mwongozo wa jinsi ya kutumia kanuni hiyo kwa kuwa ni pana na inaingilia kanuni kuu ya mpira wa miguu inayompa refa uamuzi wa mwisho uwanjani.

Kwani kadi gani zinaweza kufutwa na kamati na ni katika mazingira gani. Kama itaonekana ni udhaifu wa mwamuzi, yafaa aadhibiwe mwamuzi kwa kuwa mpira wa miguu umempa mamlaka yote uwanjani.

Kanuni ieleze kamati inaweza kufuta kadi katika mazingira gani. Hii itasaidia kuondoa uhuni katika maamuzi mengine huko mbele. Inawezekana kabisa mchezaji ambaye kamati inataka acheze mechi muhimu, akaonyeshwa kadi ya pili ya njano huko mbele na hivyo kutakiwa kukosa mechi inayofuata.

Kwa kutumia marejeo ya tukio hilo, kamati inaweza kukaa na kufuta kadi hiyo kwa maelezo madogo tu kwamba “imezingatia kanuni ya 12:8” na hivyo kumpa mchezaji huyo haki ya kucheza mechi inayofuata.

Huko nyuma kanuni ya kusogeza mbele adhabu ya kukosa mechi baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu, iliwahi kutumika katika mechi moja tu, halafu ikafutwa wakati msimu uikiendelea. Huu ni uhuni unaoweza kujitokeza huko mbele kama matukio kama haya ya kuchezesha mechi kutokea Karume Stadium yataendelea kufanyika kiholela namna hii.

Pia ukiangalia kuanzia Kanuni ya 12 inahyoanzisha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji Ligi, utasona imepewa majukumu makubwa na mengi yanayoondoa umuhimu wa kamati nyingine zote za TFF, yaani kamati za maadili, nidhamu na hata hadhi za wachezaji.

Hawa ni watu wa namna gani wanaoweza kutekeleza majukumu mengi ya aina tofauti na baadhi yakihitaji utaalamu katika uamuzi na sheria?

Pengine mamlaka hayo ndiyo yanasababisha wajichukulie uamuzi wowote ule kama mamlaka ya kufuta kadi yanavyowaelekeza kwamba wanaweza kufuta kadi yoyote ile.

Bodi ya Ligi haina budi kuangalia upya kanuni zake na pia majukumu ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi na ikiwezekana itoe mwongozo wa jinsi ya kufanya uamuzi badala ya kufanya maamuzi kuridhisha hisia za mashabiki.

Niliandika shauri la Aucho kuhusu kujichukulia maamuzi ya kuonyesha kadi nyekundu wachezaji baada ya mechi kuisha, kitu ambacho hakijawahi kutokea duniani, na leo nimezungumzia hili la kufuta kadi ya pili ya njano, ambalo halipo.

Kadi ya njano hufutwa na mwamuzi uwanjani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live