Dirisha kubwa la usajili wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa klabu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) na Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) kwa msimu ujao limefungwa Agosti 31 mwaka huu.
Tayari michezo ya raundi ya kwanza imeshachezwa na Yanga na Singida Big Stars zimeungana na Simba kwenye raundi ya pili na zitacheza Septemba 16 na 17 mwaka huu, huku Singida pekee ndiyo ikiwakilisha kwenye Kombe la Shirikisho.
Wakati hayo yakitarajiwa kuendelea tayari kuna baadhi ya mastaa na makocha wamelamba dume baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.
Mastaa hao wanasubiriwa kuona watafanya nini kwenye timu zao mpya huku wakitarajiwa wengine msimu ujao kwenye michuano hiyo. Wataweza?
Mwanaspoti linakuletea wachezaji na makocha waliotoka timu moja kwenda nyingine kutokana na ubora waliouonyesha msimu uliopita.
FISTON MAYELE
Baada ya kuitumikia Yanga miaka miwili na kufanikiwa kuifungia mabao 33 ya Ligi Kuu Bara akianza na 16 msimu wa kwanza na 17 msimu uliomalizika kabla ya kutimkia Pyramid ya Misri.
Staa huyo ambaye alikuwa chaguo la kwanza Yanga kabla ya kutimkia Misri alionyesha kiwango kizuri kwenye mashindano ya kimataifa akiifungia Yanga mabao saba Kombe la Shirikisho na ndio siri ya kuonekana na kupata ofa hiyo.
Mayele akiwa Pyramid ambayo inaendelea na maandalizi ya msimu mpya tayari ametupia mabao matatu kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Varsak Antalya.
NASREDDINE NABI
Kaitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu na kuipa mataji sita ngao ya jamii mara mbili, Kombe la Azam (ASFC) mara mbili na Ligi Kuu Bara mara mbili huku akiifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mafanikio ya Nabi katika mashindano ya ndani na kimataifa yamemtengenezea CV kubwa ambayo ilimpa mwanya wa kupata ofa mbalimbali kutoka timu kubwa na sasa amejiunga na FAR Rabat ya Morocco.
Nabi amejiunga na FA Rabat wakiwa mabingwa wa Morroco tayari ameshaiongoza timu hiyo kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa hatua ya awali na kuisaidia kutinga hatua ya pili baada ya kuanza na ushindi mwembamba ugenini wa bao 1-0 dhidi ya ASKO Kara ya Togo kisha kushinda nyumbani mabao 7-0.
HERMY GUELDICH
Ni kocha wa viungo ambaye ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na kusaidia wachezaji kuwa na ubora kiwanjani wakitumika dakika 90 bila kuchoka.
Ubora alioujenga kwenye kikosi cha Yanga akiiongoza kutwaa mataji sita kama ilivyokuwa kwa Nabi umempa shavu la kutimkia Orlando Pirates.
Gueldich alisomea ukocha wa viungo ‘Fitness coaching’ kwa takribani miaka minne katika chuo kikubwa cha sayansi ya mazoezi, Tunisia akapata Shahada ya Uzamili ya mambo ya viungo na utendaji katika michezo. Baadae alipata pia leseni ya (CAF) B na mwisho akapata (PHD) ya sayansi ya mazoezi ya viungo.
AIMEN MAHIOUS
Kasajiliwa Yverdon Sport FC akitokea USM Alger aliyoichezea mechi 15 za mashindano ya kimataifa na kufanikiwa kufunga mabao manne ubora wake ndio umemfanya anekane na kupewa mkataba.
Mshambuliaji huyo baada ya kupewa mkataba na timu yake hiyo katika mashindano yopte waliyocheza hadi sasa kafanikiwa kupata nafasi ya kucheza mechi mbili na katika michezo hiyo katupia kambani mabao mawili.
HAITHEM LOUCIF
Anakipiga nafasi ya beki wa kulia ametua Yverdon Sport FC akitokea USM Alger mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika ubora aliouonyesha kwenye mashindano hayo akicheza mechi 12 na kutoa pasi moja ya bao ndio siri ya kutua kwenye timu yake hiyo mpya.
Beki huyo wa kulia akiwa USM Alger amekipiga mechi zote mbili za fainali dhidi ya Yanga ameshatua kwenye klabu yake hiyo mpya tayari amecheza mechi moja.
REDA SLIM
Ni winga aliyekuwa anakipiga FAR Rabat ya Morocco sasa ametua El Ahly kwa dau la Sh5 billion akiunzwa Euro 2 milioni.
Staa huyo ameonekana kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na timu yake ya zamani FAR Rabat ambayo imecheza hatua ya nusu sainali na kutolewa na mabingwa wa mashindano hayo USM Alger. Slim amecheza mechi 10 kwenye mashindano yote ya kimataifa na kufanikiwa kuingia kambani mara mbili.
RANGA CHIVAVIRO
Straika huyo mwenye mwili jumba, aliupiga mwingi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita akiwa na Marumo Gallants ya Afrika Kusini na kuanza kumezewa mate na timu mbalimbali ikiwamo Yanga.
Mkali huyo aliyecheza mechi 10 za CAF na kufunga mabao sita hadi timu yake ilipotolewa nusu fainali na Yanga, kwa soka alililopiga kwenye michuano hiyo ilimpa ulaji kwa kusajiliwa Kaizer Chiefs iliyoizidi akili Yanga iliyokuwa ikimwona Chivaviro kama ndiye mrithi sahihi wa Fiston Mayele aliyekuwa njiani kutimka.