Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kama wewe Chelsea, usisome hii

Enzo Fernandez To Potter Enzo Fernandez

Sun, 27 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita ililipa Pauni 100 milioni kusajili kiungo mwingine wa kati, Moises Caicedo.

Hapohapo wakaibwaga Liverpool kwenye mbio za kumnasa kiungo mwingine, Romeo Lavia.

Hao ni Chelsea na bado kiliikuta kilichoikuta ilipokwenda kukwaana na West Ham wikiendi iliyopita.

Mechi hiyo ilikutanisha timu mbili zilizokuwa na matumizi tofauti sana kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Chelsea ilianzisha kikosi cha kwanza kilichokuwa ghali kwelikweli, wakati West Ham United ilikuwa ya kawaida tu na ilikosa pia huduma ya kiungo wake mahiri, Declan Rice - aliyeuzwa Arsenal.

Kwenye kikosi chao kulikuwa na huduma ya James Ward-Prowse, aliyecheza mechi yake ya kwanza, akaasisti mara mbili na kumpa Kocha David Moyes ushindi ambao kimsingi hakuwa umeutarajiwa kabisa.

Vijana wa Chelsea chini ya Kocha Mauricio Pochettino walicheza soka tamu sana, hasa kipindi cha kwanza kabla ya mfungaji wa bao lao Carney Chukwuemeka hajatolewa uwanjani kutokana na kuumia.

Mchezaji aliyeingia kuchukua nafasi yake, Mykhailo Mudryk hakuwa na wakati mzuri katika mechi hiyo.

Udhaifu wa Chelsea kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo huo ilikuwa kusukumia mpira kwenye nyavu na kumaliza mechi, mfano kiungo wake Enzo Fernandez alivyokosa penalti, ambapo kama angefunga pengine ingewaleta kwenye wakati mzuri wa kushinda mechi.

Haishangazi kwa mchezaji mzuri na mwenye rekodi nzuri ya kufunga penalti akikosa mkwaju wake. Ubora wake kwenye kufunga penalti ndicho kitu kilichomfanya Enzo kupewa kipaumbele kwenye kupiga mkwaju huo mbele ya Nicolas Jackson na Raheem Sterling.

Kitu kibaya kwa Enzo ni kwamba alipoteza fursa ya kufunga bao lake la kwanza kwenye kikosi hicho tangu aliposajiliwa kwa Pauni 108 milioni katika dirisha la Januari.

Jackson ameonyesha kiwango kizuri hadi sasa kwa kasi yake na ubora kwenye kukukota mipira ulikuwa tishio kwa mabeki wa timu za Liverpool na West Ham United ambazo amekabiliana nazo kwenye Ligi Kuu.

Lakini, tatizo anafanya kazi kubwa nje ya boksi na mbali ya goli kitu ambacho kinamfanya ashindwe kupasia mipira kwenye nyavu kitu ambacho ndicho Chelsea inachohitaji.

Wakati alikuwa moto kwa kufunga alipokuwa Manchester City, Sterling ameshindwa kuonyesha makali tangu alipotua Stamford Bridge. Alikuwa na kiwango cha dunia huko Man City, lakini Chelsea amekuwa tofauti sana.

Armando Broja anakaribia kupona, lakini bado hajaonyesha jambo la maana uwanjani, wakati staa mpya, Christopher Nkunku, mfungaji wa mabao 58 kwa misimu miwili alivyokuwa RB Leipzig, naye ni mgonjwa. Naye pia si Namba 9 halisi. Kuhusu Romelu Lukaku, hana maisha ya kudumu Stamford Bridge.

Straika huyo Mbelgiji ni kama ameshatanguliza mabegi yake kwenye geti la kutokea Stamford Bridge.

Mapengo hayo yanayoonekana kwenye kikosi cha Chelsea ndiyo yanayoibua maswali imekuwaje tajiri Todd Boehly ametumia zaidi ya Pauni 950 milioni, kusajili wachezaji 24, akivunja rekodi ya uhamisho ya Uingereza mara mbili ndani ya mwaka mmoja, lakini bado hakuna straika wa kiwango cha dunia.

Hata msimu wake wa kwanza akiwa tajiri mpya wa timu hiyo, Chelsea haikuwa timu yenye kufunga mabao mengi. Ilifunga mara 38 tu, ikiwa ni nusu ya misimu iliyopita na ilikuwa kiwango kidogo zaidi cha mabao tangu msimu wa 1923/24. Hakuna mchezaji wake yeyote aliyefunga mabao yanayoanzia tarakimu mbili, hata Kai Havertz - aliyekuwa kinara wa mabao, aliishia kufunga mara saba tu.

Hata huko nyuma, mabao yake mengi yaliyofungwa yalitoka kwa viungo wao Frank Lampard na Eden Hazard. Hakuna straika kwenye orodha hiyo. Kwenye ile misimu miwili ya mwisho ya umiliki wa bilionea wa Russia, Roman Abramovich waliokuwa vinara wa mabao ni viungo, ambao ni Mason Mount, aliyefunga mabao 11 katika msimu wa 2021/22 na Jorginho mabao saba msimu mmoja kabla, huku yote alifunga kwa mikwaju ya penalti.

Straika Tammy Abraham msimu wake mmoja alipokuwa mshambuliaji pekee kwenye kikosi hicho alifunga mabao 15 kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa haraka sana akaondolewa baada ya ujio wa Havertz, Timo Werner na wengineo, hivyo akaachana na maisha ya Stamford Bridge.

Kilichowakuta Havertz na Werner wanaingia kwenye kundi la wachezaji wa hovyo kwenye kikosi cha Chelsea, sambamba na Lukaku, Fernando Torres, Alvaro Morata, Gonzalo Higuain, Radamel Falcao, Alexandre Pato, Andriy Shevchenko na Mateja Kezman - ambapo washambuliaji wote hao hakuna aliyekuwa na maajabu.

Mastraika hao wote walikuwa moto kwenye timu nyingine akiwamo Morata, lakini walipofika Chelsea ni kama walisahau buti zao za kufungia huko kwingineko na kuonekana washambuliaji wa kawaida.

Kwa kifupi, mastraika wawili tu walioongoza safu ya ushambuliaji ya Chelsea kwa mafanikio makubwa katika misimu yao huko Stamford Bridge ambao ni Didier Drogba na Diego Costa. Wao ni mastraika pekee waliofunga mabao 20 na zaidi kwenye Ligi Kuu England kwa upande wa Chelsea kwa misimu 20 iliyopita, licha ya kwamba Frank Lampard naye alifikisha idadi kama hiyo katika msimu wa 2009/10.

Drogba alikuwa mshambuliaji chaguo la pili mbele ya Costa katika msimu wa 2014/15, ambapo Jose Mourinho alinyakua taji lake la tatu la Ligi Kuu katika awamu yake ya pili kuinoa timu hiyo. Hata hivyo, washambuliaji hao waliotamba na Chelsea, hakuna aliyekuwa akivaa Namba 9 mgongoni, huku waliowahi kuvaa namba hiyo na kufanikiwa walau kwa uchache ni Abraham katika msimu wa 2019/20 na Hernan Crespo 2005/06.

Nicolas Anelka, kama ilivyotokea kwa Drogba mara mbili, walishinda Kiatu cha Dhahabu wakiichezea The Blues, licha ya kwamba jezi yake ilikuwa na Namba 39. Hao ndio washindi pekee wa Kiatu cha Dhahabu kwenye kikosi cha Chelsea tangu alipofanya hivyo Jimmy Floyd Hasselbaink msimu wa 2000/01.

Mabao yanashinda mechi na hilo linaonyeshwa na Manchester City na straika wake Erling Haaland. Msimu huu, Chelsea ipo chini ya Kocha Mauricio Pochettino, ikijaribu kurudi kwenye ubora wake. Lakini, shida yake haina straika wa kuwapigia mabao.

Hilo linaweza kuwasukuma kwenye usajili wa straika mpya kabla ya dirisha kufungwa, ambapo kwenye rada zake kuna vichwa viwili matata kabisa vya mastraika wa viwango vya juu, Dusan Vlahovic na Victor Osimhen. Je, tajiri Todd atafungua pochi na kuifanya Chelsea kufikisha matumizi ya Pauni 1 bilioni kwenye usajili wa mastaa wapya ndani ya mwaka mmoja? Chelsea inahitaji mabao. Ngoja tuone.

Chanzo: Mwanaspoti