Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kama PSL inaikomalia CAF, TPLB inashindwaje kusimama kidete?

Tplboard Kasongo Afisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almas Kasongo

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 2011 tuliialika timu ya taifa ya soka ya Afrika Kusini kuja kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya taifa hilo la Kusini mwa Afrika kuandaa fainali za Kombe la Dunia.

Wakati huo, Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana, ilikuwa moto na ilipata jina kutokana baadhi ya wachezaji wake nyota kama Siphiwe Tshabalala kung’ara, akiwa amefunga bao safi la kwanza kwenye fainali hizo za kwanza kufanyika barani Afrika.

Ingawa Chama cha Soka cha Afrika Kusini (Safa) kilikubali ombi letu na kuahidi kuleta timu, kocha wa nchi hiyo hakuweza kupata wachezaji wake nyota kwa ajili ya safari ya Tanzania.

Kwa nini? Kwa sababu Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) ilizuia wachezaji hao nyota kuacha klabu zao zikiendelea na mechi na kwenda kuchezea timu ya taifa, ikisema kampuni zimewekeza fedha ili klabu zicheze kiushindani kwa kiwango cha juu na mashabiki wanataka wazione timu zao zikiwa na nyota wao.

Kweli. Tshabalala na wenzake hawakuja Tanzania na timu ya taifa ya Afrika Kusini.

Kwa mara nyingine, PSL imetishia kuizuia Mamelodi Sundwons kushiriki michuano mipya ya Ligi ya Soka Afrika (AFL), ikisema waandaaji wamechelewa kutuma barua ya uthibitisho wa kuwepo kwa mashindano hayo na tayari Ligi Kuu imeshapanga ratiba ya ngwe ya kwanza ya ligi, hivyo haiwezi kuivuruga kwa kuiondoa Mamelodi kwa siku takriban 30 ili ishiriki ligi hiyo mpya ya klabu nane.

Pili, PSL inahoji sababu za barua ya uthibitisho wa mashindano hayo kutokea Kigali, Rwanda badala ya Cairo Misri yaliko makao makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Habari zinasema CAF imeipa kampuni moja ya Italia kuratibu mashindano hayo. Kampuni hiyo imeamua kuweka ofisi zake jijini Kigali ndio maana mawasiliano yanatoka Rwanda.

Pia, wiki iliyopita klabu za England ziliidhinisha mpango wa Ligi Kuu (Premier League) wa haki za matangazo ya televisheni ambao utawezesha mechi nyingi zaidi kurushwa moja kwa moja na hivyo kuchangia kuongezeka kwa mapato katika mkataba mpya ambao ligi hiyo itaingia na kampuni nyingine.

Klabu zote 20 za Ligi Kuu zilipiga kura kwa njia ya mtandao kupitisha mpango huo Alhamisi ya Septemba 28 na sasa mpango huo utasambazwa kwa kampuni za televisheni kwa ajili ya kujua mahitaji ya Ligi Kuu kabla ya kupeleka zabuni za kuomba kununua haki hizo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya England, mpango huo utakuwa na mabadiliko makubwa kulinganisha na huu wa sasa ambao thamani yake ni Paundi 5.1 bilioni za Kiingereza (sawa na Sh15.6 trilioni za Kitanzania), huku haki za matangazo ya moja kwa moja zikimilikiwa kwa pamoja na Sky, TNT Sport na Amazon ambazo kila moja huonyesha mechi 200 kila msimu.

Nimeweka hayo mambo matatu kujaribu kuonyesha ni jinsi gani Ligi Kuu ambayo ni huru inaweza kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuzuia uwezekano wowote wa viongozi wa vyama vya soka vya nchi au mashirikisho kuingiza ubinafsi au siasa katika kuendesha mpira wa miguu.

Kama chama cha soka au shirikisho la nchi linataka kuipa mazoezi timu yake ya taifa nje ya tarehe zilizotengwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ni lazima mechi hiyo isiingiliane na uendeshaji wa Ligi ya nchi kwa kuwa kinaweza kuvuruga ratiba nzima ambayo huhusisha wadau tofauti kama kampuni za televisheni, program za wadhamini wa klabu na wa ligi, wafanyabiashara na hata program za klabu.

Chombo chenye wajibu wa kulinda maslahi hayo ya wadau wa Ligi Kuu ni kama Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB). Lakini TPLB inaweza kuikomalia TFF isisimamishe ligi kwa ajili ya kuipa timu ya taifa nafasi ya kwenda Burundi kushiriki mechi za kirafiki zilizo nje ya kalenda ya Fifa?

Kama ambavyo Bodi ya Utawala ya PSL ilivyoamua, TPLB inaweza kuizuia Simba isishiriki Ligi ya Soka Afrika (AFL) eti kwa sababu ushiriki wake utavuruga Ligi Kuu ya Bara? PSL imeiambia Mamelodi kuwa kama inataka kushiriki michuano hiyo mipya basi itafute kikosi kingine kitakachopewa jina lake na si ile yenye wachezaji nyota wanaofuatwa na maelfu ya watu viwanjani Afrika Kusini.

Sisi huku tunaona ufahari kuwa Simba inashiriki, bila ya kuhoji kwa undani michuano hiyo ambayo barani Ulaya ilizuiwa baada ya mashabiki kufanya vurugu, kiasi cha kusababisha mchezo wa Manchester United wa Ligi Kuu ya England uahirishwe.

Kama Ulaya walizuia mashindano hayo kwa sababu za kimpira—lazima ushiriki utokane na ushindani wa wakati huo--, inakuwaje Afrika ikubali kirahisi mashindano yenye sura kama hiyo? Ni kwa sababu ligi nyingi za Afrika hazijawa na uhuru huo na wala watu wenye maono ya kuhoji kila jambo, hasa lile linalokuja na utamu mwingi.

Wahenga wanasema ukiona kitu kinakuja kwa uzuri sana, fikiria mara mbili.

Pia katika suala la Ligi Kuu ya England, tumeona ni kiasi gani chombo kilichoundwa vizuri cha kuisimamia ligi kinavyoweza kujipanga na kutengeneza mpango utakaozinufaisha timu na ligi yenyewe kimapato. Andiko limeandaliwa na Premier League na kuwasilishwa kwa klabu zote ili lisomwe na kueleweka, kabla ya kupigiwa kura kuidhinishwa.

Hapa ni kwamba macho ya Premier League hayako pekee kwa Sky, wala TNT Sport au Amazon ambao kwa sasa ndio wanaomiliki haki za matangazo ya moja kwa moja, bali kwa kampuni zozote zenye nia ya kuzinunua. Ni dhahiri kuwa ni muhimu kumlinda mmiliki wa sasa wa haki hizo, lakini si vibaya kupanua wigo.

Kwa hiyo, TPLB inabidi iimarishwe ili iwe na watendaji wanaoweza kuwa na maono, stadi na ufahamu wa kuweza kuwasilisha Azam Media na pengine kama kuna wadai wengine, mpango wao unaoeleza mambo ya kuzingatia katika mkataba mpya wa matangazo ya moja kwa moja ya mechi zake, badala ya kusubiri kuletewa sahani iliyojaa mezani.

Najua kila wakati napozungumzia uhuru wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania naudhi watu wengi walio katika mamlaka za soka, lakini ili mpira wetu ukue, ni muhimu sana chombo hicho kikawa na uhuru uliokusudiwa awali na uliowekwa kwenye maandiko ya uhusiano kati ya TFF na Ligi Kuu.

Hivi sasa si Premier League ya England pekee iliyo na uhuru kamili wa kuendesha mambo yake, bali hata waamuzi ambao sasa wanasimamiwa na Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Ligi ya Kulipwa (PGMO) ambayo huhusika na masuala yote, ikiwemo mafunzo, kuadhibu na kuwajibika kwa wadau kama klabu na mashabiki. Hapa tunasubiri nini?

Chanzo: Mwanaspoti