Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kally afikia rekodi ya Cioaba

Kally Ongala Big Match Kocha wa Azam FC, Kally Ongala

Thu, 1 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Azam FC, Kally Ongala amefikia rekodi tamu ya Mromania Aristica Cioaba kuliongoza chama hilo kushinda michezo saba mfululizo Ligi Kuu Bara.

Kally ambaye alikabidhiwa kukaimu nafasi hiyo tangu Oktoba 2022 kutoka kwa Mfaransa Denis Lavagne aliyefutwa kazi baada ya Azam kufungwa na KMC bao 1-0 ameifikia rekodi hiyo baada ya kuiongoza timu juzi kushinda mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union.

Licha ya kufikia rekodi hiyo, Kally alisema hilo halikuwa kichwani mwake lakini ambacho alikuwa akifanya ni kutoa mchango wake wa kiufundi kuhakikisha wanafanikisha malengo ya klabu kufanya vizuri kila mchezo.

“Jambo muhimu ilikuwa ni kushinda kila mchezo, bado tuna safari ndefu kwa sababu kushinda michezo saba mfululizo haikufanyi kuwa bingwa. Ni hatua moja kuelekea kwenye lengo tunatakiwa kuongeza juhudi na maarifa,” alisema.

Mchezo wa kwanza kwa Kally ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa timu hiyo kuiongoza Azam ni dhidi ya Simba ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0, tangu hapo amekuwa akitoa dozi dhidi ya Ihefu (1-0), Dodoma Jiji (2-1), Mtibwa Sugar (4-3), Ruvu Shooting (1-0), Namungo (1-0) kabla ya Coastal Union ya Tanga.

Cioaba aliweka rekodi hiyo tamu kwa Azam msimu wa 2020/21 ambapo ndani ya michezo minne ya kwanza sawa na dakika 360, hawakuruhusu bao huku golini akiwa na David Kissu ambaye kwa sasa anaidakia KMC.

Ndani ya msimu huo Azam iliitandika Polisi Tanzania kwa bao 1-0 na ilishinda mabao 2-0 mbele ya Coastal Union zikichezwa Uwanja wa Azam Complex.

Mechi zake mbili ugenini ilishinda zote ilikuwa mbele ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine na ilishinda pia mbele ya Tanzania Prisons kwa bao 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela.

Michezo mingine ilikuwa dhidi ya Kagera Sugar (4-2), Mwadui (3-0) na Ihefu (2-0), mfululizo huo wa ushindi kwa Cioaba ulisitishwa na Mtibwa Sugar ambao waliwatandika kwa bao 1-0 hivyo Kali anakibarua kwenye mchezo wake ujao Desemba 5 dhidi ya Polisi Tanzania kuhakikisha anaweza rekodi yake.

Chanzo: Mwanaspoti